NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WAFANYABIASHARA na wananchi kwa ujumla wametakiwa kutumia Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutembelea banda la Tume ya Ushindani (FCC) ili kupata huduma mbalimbali za papo kwa papo pamoja na elimu kuhusu ulinzi wa mlaji, ushindani wa biashara na udhibiti wa bidhaa bandia.
Wito huo umetolewa leo Julai 6, 2026 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma wa FCC, Roberta Feruzi, ambapo ameongeza kuwa maonesho hayo yameipa tume hiyo fursa ya kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwaelimisha kuhusu haki zao pamoja na huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
Amesema mbali na kutoa elimu, FCC pia inatoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi wanaotembelea banda lake, ikiwemo kupokea na kushughulikia malalamiko, usajili wa mikataba na huduma nyingine zinazotolewa na tume hiyo.
"Tunawaalika wananchi wote kufika katika banda la Wizara ya Viwanda na Biashara, ambalo ni banda jumuishi lenye taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo, ikiwemo FCC, ili wapate huduma na elimu kuhusu masuala ya ushindani, ulinzi wa mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia," amesema.
Amebainisha kuwa FCC haijajikita kutoa huduma ndani ya banda pekee, bali imeandaa programu ya kuwafuata wafanyabiashara na wajasiriamali katika maeneo mbalimbali ndani ya viwanja vya Sabasaba kwa lengo la kuhakikisha elimu inawafikia wadau wengi zaidi.
Amesemakuwa FCC imekuwa ikiendesha semina kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara, ikiwapa mafunzo kuhusu sheria za ushindani, namna ya kufanya biashara kwa kuzingatia misingi ya ushindani wa haki pamoja na wajibu wao katika kulinda maslahi ya walaji.
Amesema tangu kuanza kwa maonesho hayo, FCC imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wajasiriamali 700, wakiwemo wazalishaji wadogo na wa kati, ambao wamepatiwa elimu kuhusu namna ya kulinda alama na nembo za biashara zao, kuendeleza ubunifu na kuongeza ushindani katika soko.
Aidha, amesema taasisi hiyo inaendelea kuwalea vijana wabunifu wanaoshiriki maoneshoni kwa kuwapatia mwongozo wa namna ya kukuza biashara zao katika mazingira ya ushindani wa haki.
Amesisitiza kuwa kampeni ya utoaji elimu haitakoma baada ya kumalizika kwa maonesho ya Sabasaba, bali itaendelea kupitia ofisi za FCC zilizopo Dar es Salaam na ofisi za kanda za Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi jumuishi kwa kuweka mazingira bora ya biashara, huku FCC ikiendelea kuwa mlezi, mwezeshaji na mdhibiti wa ushindani wa haki nchini.
Amewahimiza wafanyabiashara, wabunifu na wananchi ambao hawajapata nafasi ya kushiriki maonesho hayo kufika katika ofisi za FCC zilizo karibu nao ili kupata elimu, ushauri na huduma mbalimbali zinazotolewa na tume hiyo kwa maendeleo ya biashara zao.








EmoticonEmoticon