Mkuu wa Mkoa wa Singida
Dkt Rehema Nchimbi (katikati) akimkabidhi mmoja kati ya wa wakulima wa Pamba wa
kijiji cha Kinyangiri Wilayani Mkalama kilo kumi za mbegu za zao la pamba
zilizotolewa bure na Serikali kwa wakulima hao. Kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga.
Mkulima wa Pamba Bi
Johari kutoka kijiji cha Kinyagiri Wilayani Mkalama akibeba mbegu za Pamba kilo
kumi alizokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi, mbegu hizo
zimetolewa bure kwa wakulima wa Pamba Mkoa wa Singida.
Mama Devid Mkulima wa
Pamba wa Kijiji cha Kinyangiri Wilayani Mkalama akijifunza kwa vitendo namna ya
kuandaa kamba inayotumika kuonyesha vipimo vya upana na urefu katika kupanda
pamba badala ya kilimo cha mazoea cha kumwaga mbegu bila kufuata kipimo
chochote.
Wakulima wa Pamba wa
Kijiji cha Lyelembo Wilayani Mkalama wakiwasikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt
Rehema Nchimbi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini Marco
Mtunga (hawapo pichani) kabla ya kupewa mbegu za pamba zilizotolewz bure.
Wakulima wa pamba wa
kijiji cha Kinyangiri Wilayani Mkalama wakimfuatilia kwa makini mtaalam kutoka
Bodi ya Pamba Nchini akiwaelekeza namna ya kupuliza dawa ya kuuwa wadudu
waharibifu wa pamba, viuatilifu hivyo vitatolewa bure na serikali kwa wakulima
wote wa pamba Mkoani Singida.
Serikali
imeahidi kutoa bure pembejeo za kilimo kwa wakulima mbali mbali wa zao la pamba
mkoani Singida kuanzia msimu huu wa kilimo ikiwa ni moja ya juhudi za kuhamasisha
na kufufua kilimo hicho mkoani hapa.
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga ameeleza hayo juzi katika
vijiji vya Kinyangiri na Lyelembo wilayani Mkalama katika siku ya kwanza ya
ziara yake ya siku mbili kuhimiza Kilimo cha pamba mkoani Singida.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi huyo, Kampuni ya Biosustain iliyopo mjini hapa imepewa
jukumu la kuleta na kusambaza mbegu na madawa yote yahusuyo kilimo cha pamba
bure na kwamba gharama ya pembejeo hizo italipwa na Serikali.
Kutokana
na hilo, Mkurugenzi huyo amewataka Wakulima kutumia vyema fursa hiyo kwa kulima
mashamba makubwa zaidi lakini pia kwa kuzingatia tija na ubora wa pamba.
Amesema
kuwa Wakulima wataweza kufanya hivyo tu iwapo pia watawatumia kikamilifu
wataalamu wao wa kilimo na kufuata Kanuni na Taratibu za kilimo bora.
“Mmepewa
upendeleo maalum, kazi yenu sasa ni kulima tu, malipo ya mbegu na viuatilifu
vyote italipwa na Serikali. Hapa hakuna kisingizio cha kushindwa kulima”, amesema
Mtunga na kuongeza;
“Pandeni
vizuri ili wakati mnatumia dawa, kiwango kikubwa cha dawa kisipotee bure maana
kama hukupanda kwa mstari lazima kutakuwa na ugumu wa kupulizia mimea yako.
Jengeni utamaduni wa kuwatumia wataalamu wa kilimo kama ilivyo kwa wafugaji
mifugo yao inapopatwa na maradhi”.
Aidha,
amewataka wakulima wa zao hilo kuhakikisha wanang'oa masalia yote ya misitu ya
pamba na kuichoma moto kwa kuwa, kwa kuacha kufanya hivyo wanaruhusu wadudu
waliomo kwenye masalia kuendelea kunenepeana na hivyo kuhatarisha mazao mapya
yanayopandwa.
Mkurugenzi
huyo amewasihi wakulima kuacha kuchanganya kilimo cha pamba na mazao mengine
akisema kuwa tafiti zinaonesha pamba iliyochanganywa na mazao mengine hutoa
vitumba vitatu tu ikilinganishwa na vitumba 10 kwa kilimo cha pamba iliyolimwa
peke yake.
Wakulima
wa zao hilo wamemueleza Mkurugenzi huyo kuwa, moja ya sababu za kushuka kwa
uzalishaji pamba kwenye maeneo yao ni pamoja na bei kuwa ndogo kwa kisingizio
cha Soko la Kimatafa kushuka na kuchezewa mizani wanazotumia kupima mazao yao,
hali inayowapunja kimapato.
Hata
hivyo, wamejibiwa kuwa suluhisho la kuchezewa mizani lipo mikononi mwao ili
mradi tu wajenge tabia ya kuhoji mara moja wanapoona mambo yanaenda isivyo
badala ya kusubiri hadi siku ya vikao.
Wakati
huohuo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewataka watendaji wote wa
serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Singida kulima ekari moja ya pamba
kila mmoja ili kuamsha hamasa kwa wananchi wengine.
Dkt
Nchimbi ameongeza kwa kuwataka watendaji hao kuliweka zao la pamba kama ajenga
katika vikao vyao, huku akiwataka viongozi wa dini na vikundi vya kwaya
kuonyesha mfano kwa kulima vizuri pamba.
Ameongeza
kuwa vijana wanaocheza vijiweni ‘pooltable’ waache mara moja na kujikita katika
kilimo cha pamba kwa kuwa ni chanzo kikubwa na cha uhakika cha kujipatia fedha
na hivyo kuchangia kukuza uchumi.
Aidha
amewataka wakulima wa pamba kuwasikiliza wataalamu na sio kupanda kwa mazoea
huku akishauri kuwa mikutano yote inayohusu kilimo cha pamba ifanyike katika
mashamba ya wakulima.
Dkt
Nchimbi ameeleza kuwa kauli mbiu mpya ya kilimo cha pamba kwa Mkoa wa Singida
ni, ‘Singida Mpya, kwa Pamba yenye Tija’.
EmoticonEmoticon