UTORO NA VIGODORO VYATAJWA KUCHANGIA UFAULU HAFIFU, POLISI KATA YAISHUKURU TANGAYETU

July 12, 2026


Polisi Kata wa Kata ya Nguvumali, Jiji la Tanga, Inspekta Sharifu Kiswamba, amesema utoro wa wanafunzi na tabia ya kukesha kwenye vigodoro ni miongoni mwa sababu zinazochangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika shule za sekondari.

Inspekta Kiswamba alitoa kauli hiyo wakati wa mafunzo maalumu ya kuwajengea wanafunzi mbinu za kujifunza kwa ufanisi na kujiandaa vizuri kwa mitihani, yanayoendeshwa na Tanzania Centre for Education (TCE) kwa kushirikiana na Botnar Foundation na Inovex kupitia Mradi wa TangaYetu.


Alisema mradi huo unahusisha shule 10 zilizobainika kuwa na changamoto ya matokeo hafifu ya kitaaluma, ukiwa na lengo la kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujifunza kwa ufanisi na kuongeza kiwango cha ufaulu.


"Kama Polisi Kata tunaushukuru Mradi wa TangaYetu pamoja na wadau wake kwa kuanzisha mafunzo haya. Tunaamini yatasaidia kubadilisha mtazamo wa wanafunzi, kuongeza nidhamu na hatimaye kuinua ufaulu katika shule zetu," alisema.


Alieleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na viongozi wa kata, walimu na jamii kuhakikisha wanafunzi wanaotoroka masomo wanafuatiliwa na kurejeshwa shuleni ili wasikose haki yao ya elimu.


"Tunatoa onyo kwa wanafunzi wanaotoroka masomo. Tutakaowakuta wakizurura wakati wa vipindi vya masomo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu, ikiwemo kupelekwa ofisini kwa hatua zaidi za kinidhamu," alisema.


Inspekta Kiswamba alisema pia tabia ya wanafunzi kushinda vijiweni na kukesha kwenye vigodoro imeendelea kuwa changamoto inayochangia kuporomoka kwa nidhamu na kuathiri maendeleo yao kitaaluma.


"Hatutavumilia tabia hii. Tutaendelea kufanya doria na kushirikiana na viongozi wa mitaa pamoja na wazazi kuhakikisha wanafunzi wanazingatia masomo na kujiepusha na mazingira yanayoharibu mustakabali wao," alisisitiza.


Aidha, aliwataka wazazi na walezi kutekeleza wajibu wao wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao kwa kuhakikisha wanahudhuria masomo, wanapata muda wa kujisomea na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha elimu yao.


Alisema mafanikio ya sekta ya elimu yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, walimu, viongozi wa serikali za mitaa, Jeshi la Polisi na wadau wa maendeleo, akieleza kuwa jitihada zinazofanywa na Mradi wa TangaYetu ni sehemu ya suluhisho la changamoto zinazolikabili eneo hilo.


Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Mradi wa TangaYetu za kuboresha matokeo ya kitaaluma katika shule zenye changamoto kwa kuwajengea wanafunzi stadi za kujifunza, nidhamu na maandalizi bora ya mitihani.









Share this

Related Posts

Previous
Next Post »