Benki ya CRDB yawahakikishia dhamana ya kazi na mikopo Wakandarasi

November 08, 2017
Mkurugenzi wa benki ya CRDB, huduma kwa wateja wakubwa, Goodluck Nkini akizungumza kwenye semina kwa Wakandarasi iliyoandaliwa na benki hiyo kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanroad pamoja na kampuni ya uuzaji mitambo ya Mantrac.
Semina hiyo ilifanyika jana Jijini Mwanza na kuwakutanisha Wahandisi na Wakandarasi kutoka Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza.

Na Binagi Media Group
Benki ya CRDB imewahakikishia Wakandarasi upatikanaji wa mikopo pamoja na dhamana ya kazi, itakayowawezesha kuwa na vigezo vya kupata tenda na hatimaye kutimiza vyema shughuli zao.

Mkurugenzi wa CRDB mkoani Mwanza, Wambura Calystus alitoa ahadi hiyo jana kwenye semina kwa wakandarasi wa barabara, iliyoandaliwa na beki hiyo kwa kushirikiana na wakala wa barabara Tanroad mkoa wa Mwanza pamoja na kampuni ya uuzaji na ukodishaji wa mitambo ya Mantrac.

“Miradi ya ujenzi na miundombinu imekuwa mingi katika nchi yetu hivyo tumeona ni bora benki yetu ya CRDB iweze kukaa na wakandarasi ili tuone namna bora ya kuwafikishia huduma waweze kujenga miundombinu hiyo bila tatizo”. Alisema Calystus.

Naye Mkurugenzi wa CRDB huduma kwa wateja wakubwa, Goodluck Nkini alisema ushirikiano baina ya benki hiyo, Tanroad pamoja na kampuni ya Mantrac utawasaidia wakandarasi hususani wadogo kupata mitambo bora ya kufanyia kazi na hivyo kutimiza vyema majukumu yao.

“CRDB itawezesha wakandarasi kupata mitambo na kuondoa kero iliyokuwepo awali ya wakandarasi kukosa kazi kwa sababu ya kutokuwa na mitambo”. Alisema Meneja Mauzo kutoka kampuni ya Mantrac Kanda ya Ziwa, Eutachius Katiti.

Awali Kaimu Meneja wa Tanroad mkoani Mwanza, Joseph Mwami alikiri kwamba wakandarasi wengi walikuwa wakikumbana na changamoto ya kupata kazi kutokana na kukosa dhamana ya kazi hivyo imani yake ni wakandarasi kutumia vyema fursa hiyo.

Kwa upande wake Mhandisi Emmanuel Mapigano ambaye ni mmoja wa wakandarasi waliohudhuria semina hiyo kutoka kampuni ya MP Investment Ltd, alitoa rai kwa benki ya CRDB, Tanroad pamoja na kampuni ya Mantrac kuendeleza ushirikiano huo ili kuwawezesha wakandarasi kukua na kulijenga taifa kwa umoja.
Wakandarasi waliohudhuria semina hiyo wakimsikiliza Mkurugenzi wa CRDB Tawi la Mwanza, Wambura Calystus.
Mkurugenzi wa CRDB, wateja wadogo na wa kati, Elibariki Masuke (kushoto), akizungumza kwenye hafla hiyo. Kulia ni Mkurugenzi wa CRDB Tawi la Mwanza, Wambura Calystus.

Meneja Mauzo Kanda ya Ziwa kutoka kampuni ya uuzaji na ukodishaji mitambo ya Matrac, Eutachius Katiti akieleza huduma zinazotolewa na kampuni hiyo.
Kaimu Meneja wa Tanroad mkoani Mwanza, Mhandisi Pius Mwami akizungumza kwenye semina hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi CRD mkoani Mwanza, akizungumza kwenye semina hiyo.
Mkurugenzi wa kampuni ya MP Investment Ltd, Mapigano John akichangia mada kwenye semina hiyo.
BMG Habari, Pamoja Daima!

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »