Msimamizi
wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Kigamboni kilichopo jijini Dar
es Salaam, Sylvester Sikare (kulia) akielezea maendeleo ya ukamilishaji
wa kituo kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) mara
alipofanya ziara katika kituo hicho tarehe 27 Novemba, 2017.
Meneja
wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Kigamboni, Mhandisi
Richard Swai (kushoto mbele) akieleza jambo kwa Naibu Waziri wa Nishati,
Subira Mgalu (kulia) katika ziara hiyo.
Moja ya transfoma zilizopo katika kituo cha kupoza umeme cha Kigamboni kilichopo jijini Dar es Salaam.
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akisalimiana na baadhi ya watendaji
mara baada ya kuwasili katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga.
Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga.
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akisaini kitabu cha wageni,
mara baada ya kuwasili katika Kata ya Mkamba wilayani Mkuranga mkoani
Pwani kabla ya kuanza kuwahutubia wakazi wa Kata hiyo. Kushoto ni Mkuu
wa Wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga.
Sehemu
ya wakazi wa Kata ya Mkamba wilayani Mkuranga mkoani Pwani wakifuatilia
hotuba iliyokuwa inatolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
(hayupo pichani).
Mbunge
wa Mkuranga na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega
akifafanua jambo kwa wakazi wa Kata ya Mkamba wilayani Mkuranga mkoani
Pwani (hawapo pichani) katika mkutano wa hadhara.
Mkazi
wa Kata ya Mkamba wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Mohamed Masinike
akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo
pichani) katika mkutano wa hadhara.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa kata za Kigamboni,
Vijibweni, Tungi zinatarajiwa kupata umeme wa uhakika kufuatia
kukamilika kwa mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kigamboni
kilichopo jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mgalu aliyasema hayo tarehe 27 Novemba, 2017 kwenye ziara yake katika
kituo cha kupoza umeme Kigamboni na katika mikutano ya hadhara
aliyoifanya katika kata za Kisiju na Mkamba zilizopo wilaya ya Mkuranga
mkoani Pwani.
Alisema
kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wateja kutoka 6,000 hadi
12,000 na kuongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati
itahakikisha vituo vingine vya kuboresha hali ya umeme ndani ya jiji
la Dar es Salaam vinakamilika mapema Desemba 15, 2017 na kuondoa
tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara lililokuwa linajitokeza.
Aidha,
alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukamilisha vituo
vingine vilivyobaki vya Kurasini, Gongo la Mboto na Mbagala mapema ili
wakazi wa jiji la Dar es Salaam waweze kuondokana na tatizo la ukosefu
wa umeme.Katika
hatua nyingine, Mgalu aliwataka wandarasi waliopewa kazi ya kujenga
miundombinu ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) kukamilisha miradi mapema na kuongeza kuwa Serikali
haitamvumilia mkandarasi atakayezembea ukamilishwaji wa mradi wake.
“
Wananchi wanahitaji umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu, umeme ndio
uchumi wa nchi na kama Wizara ya Nishati tupo kwa ajili ya kuhakikisha
uchumi wa viwanda unakua kwa kuhakikisha nishati ya umeme ya uhakika
inapatikana sehemu zote hasa vijijini,” alisisitiza Mgalu
Vilevile,
Mgalu aliitaka REA kuainisha vipaumbele katika usambazaji wa umeme
vijijini, kipaumbele kikiwa ni vijiji vyenye wakazi wengi na taasisi
kama hospitali, makanisa na misikiti.
Akizungumzia
suala la fidia kwa wakazi wanaopisha ujenzi wa miundombiniu ya umeme
unaosimamiwa na REA, Naibu Waziri Mgalu alisema hakuna fidia kwa kuwa
serikali imekwishagharamia gharama zote na kinachohitajika kwa wananchi
ni kulipia gharama za Kodi (VAT) ambayo ni shilingi 27,000.Aliwataka
wakazi wa Kata za Kisiju na Mkamba wilayani Mkuranga kutandaza mifumo
ya nyaya (wiring) kwenye nyumba zao au kununua kifaa maalum cha Umeme
Tayari (UMETA) mapema kwa ajili ya kujiandaa na huduma ya umeme.
Akielezea
mikakati ya Serikali katika kuhakikisha umeme unapatikana hususan
katika wilaya ya Mkuranga yenye viwanda vingi, Naibu Waziri Mgalu
alisema Serikali inatarajia kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwa
kutumia gesi Somanga Fungu na kusambaza gesi nyingine kwenye viwanda
vitakavyohitaji.Aliongeza
kuwa Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa
kutumia maji wa Stieglers Gorge utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha
Megawati 2,100 na kukamilisha miradi ya Kinyerezi II na Kinyerezi III.
Alisema
kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 Megawati 5,000
zinapatikana na nchi kuingia kwenye uchumi wa viwanda utakaozalisha
ajira kwa vijana hususan kwa vijana waishio vijijini.
“
Tunataka mazao yasindikwe vijijini na kusafirishwa ndani na nje ya
nchi yakiwa kama bidhaa, tunataka mtumie fursa ya umeme kwa ajili ya
uchumi wa viwanda badala ya matumizi ya majumbani tu,” alisema Mgalu.
Naye
Mbunge wa Mkuranga ambaye ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah
Ulega alimshukuru Naibu Waziri Mgalu kwa ziara yake katika wilaya ya
Mkuranga na kuongeza kuwa wananchi wana matumaini makubwa ya umeme wa
uhakika kwani wilaya hiyo imekuwa na changamoto ya ukosefu wa umeme kwa
muda mrefu.
EmoticonEmoticon