Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, amempongeza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, kwa mchango mkubwa alioutoa katika kuendeleza Sekta ya Nishati wakati akiwa Waziri wa Nishati.
Akizungumza wakati wa kumuaga Makamu wa Rais leo, Septemba 09, 2026, katika Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma, Mha. Mramba amesema Mhe. Ndejembi ameiongoza sekta hiyo katika kipindi kilichokuwa na changamoto mbalimbali za kimataifa, ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Amesema, pamoja na changamoto hizo, kupitia weledi na uongozi bora, Mhe. Ndejembi alihakikisha upatikanaji wa mafuta nchini unaendelea kuwa wa uhakika na bei zinaendelea kuwa himilivu kwa wananchi.
Mha. Mramba amefafanua kuwa katika kipindi cha uongozi wa Mhe. Ndejembi, kumeshuhudiwa kasi katika utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi, sambamba na kuimarika kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya nishati, ikiwemo Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ambao utekelezaji wake umeongezeka kutoka takribani asilimia 79 hadi kufikia asilimia 92.
Aidha, amesema Mhe. Ndejembi ameacha alama katika kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini kuelekea lengo la Megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030. Vilevile, amewezesha utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme katika vitongoji 9,009 pamoja na kukamilika kwa Mradi wa Julius Nyerere Hydro Power Project (JNHPP), wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115.
Katika eneo la nishati safi, Mha. Mramba amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka na kufikia asilimia 28.9, huku idadi ya vituo vya kujaza gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) ikiongezeka kutoka 11 hadi 19.
Ameongeza kuwa hatua kubwa pia zimepigwa katika matumizi ya magari yanayotumia umeme, hatua ambayo inaendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania katika kukuza matumizi ya nishati safi na kuwa kitovu cha nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa niaba ya Wizara ya Nishati na taasisi zake, Mha. Mramba amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa uongozi, malezi na ushirikiano alioutoa kwa watendaji wa Wizara na taasisi zake, akiahidi kuwa Wizara itaendelea kulinda na kuendeleza misingi aliyoiweka ili Sekta ya Nishati izidi kusonga mbele.
Aidha, amemtakia Mhe. Ndejembi kheri katika majukumu yake mapya ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuongoza Taifa, huku akimuombea afya njema, maisha marefu na hekima katika kutekeleza majukumu hayo kwa manufaa ya Watanzania.





EmoticonEmoticon