BALOZI SEIF AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA NCHINI TANZANIA, PIA AKUTANA NA MABALOZI WA TANZANIA KATIKA NCHI ZA MISRI NA ZAMBIA

November 28, 2017

Balozi wa China Nchini Tanzania Bibi Wang Ke alisema kukamilika kwa utanuzi wa ujenzi wa Eneo la Maegesho ya Ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar utatoa fursa ya kuongezeka kwa huduma za usafiri wa anga baina ya Zanzibar na Mataifa mengine Duniani.


Alisema matayarisho ya ujenzi huo katika hatua za awali za Awamu ya Pili aliyoyashuhudia baada ya kushuka kwenye Uwanja huo wa Ndege wa Zanzibar yamempa faraja yeye pamoja na Uongozi mzima wa Benki ya Kimataifa ya Exim ya Nchini China iliyoridhia kugharamia Mkopo wa ujenzi huo.

Balozi Wang Ke alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo wa Kidiplomasia.

Alisema Zanzibar inaweza kurejesha Heshima yake ya kuwa Kituo cha Kibiashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki chenye uwezo wa kutoa huduma za Kibiashara kupitia mfumo wa kisasa wa Mawasiliano kupitia usafiri wa anga badala ya ule uliozoeleka wa Baharini.

Alieleza kwamba zaidi ya Watalii 70,000 kutoka Nchini Jamuhuri ya Watu wa China wanaweza kuitembelea Zanzibar kila Mwaka kupitia usafiri wa anga na hata ule wa Baharini iwapo yataandaliwa mazingira mazuri katika Sekta ya Utalii baada ya kuongezeka kwa huduma za Mawasiliano ya usafiri.

Bibi Wang Ke aliyeanza majukumu yake Nchini Tanzania Mwezi Mmoja sasa aliahidi kwamba Nchi yake iliyopiga hatua kubwa Kiuchumi ndani ya kipindi cha Miaka 30 itaendelea kuiunga mkiono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kuona maendeleo ya Kiuchumi yanakua na kushirikisha wananchi wote siku hadi siku.

Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza faraja yake katika kuona Viongozi wote waliiopo hivi sasa kati ya China na Tanzania bado wanaheshimu ushirikiano wa Mataifa hayo mawili ulioasisiwa na waanzilishi wake Marehemu Mwalimu Julius K. Nyerere na Hayati Mao Tse Tung.

Balozi Seif alisema mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na China kupitia Makampuni na Mashirikia yake mbali mbali umeiwezesha Tanzania kukuwa Kiuchumi na kustawisha Jamii mambo yanayokwenda sambamba na kupungua kwa kasi ya ukali wa Maisha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza na kumuomba Balozi huyo wa China Nchini Tanzania kwamba Zanzibar bado inaendelea kuhitaji Wawekezaji pamoja na Watalii kutoka Nchini China katika azma yake ya kuimarisha uchumi hasa kwenye Sekta ya Utalii.

Balozi Seif ameishukuru Serikali ya China kwa misaada yake mikubwa inayotowa na kumuhakikishia kwamba uhusiano wa Kihitoria uliopo wa Mataifa hayo rafiki utaendelea kudumu kila Mwaka.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Mabalozi Wapya Wawili wa Tanzania Nchini Misri na Zambia walioteuliwa hivi karibu na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli.

Mabalozi hao ni Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor anayeiwakilisha Tanzania Nchini Misri na Balozi Abdulrahman Kaniki anayekwenda Nchi jirani ya Kusini mwa Tanzania ya Zambia.

Katika mazungumzo yao Balozi Seif aliwakumbusha Mabalozi hao kuzingatia zaidi suala ya Doplomasia ya Kiuchumi ambalo kwa sasa limechukuwa nafasi ya pekee tofauti na lile ya Kisiasa lililozoeleka katika mabadiliko ya Kiuchumi yaliyopo Ulimwenguni.

Alisema matunda makubwa ya uwakilishi wa Mabalozi hao yataonekana katika kasi ya ongezeko la Miradi ya Uwekezaji kutoka katika Mataifa wanayokwenda kufanya kazi.

Mapema Balozi wa Tanzania Nchini Misri Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor kwa niaba ya Mwenzake Balozi Abdulrahman Kaniki anayekwenda Nchini Zambia alisema wanaahidi kuitanga Tanzania katika Mataifa hayo rafiki yenye Uhusiano wa muda mrefu.

Meja Jenerali Nassor aliziomba Taasisi zinazozimamia Sekta ya Utalii Nchini kuwa wazi kwa masuala yanayohitajika katika kuimarisha Sekta hiyo kupitia Wawekezaji na Mikataba ya uanzishwaji wa Miradi ya Hoteli.

Baadae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifanya mazungumzo na Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioongozwa na Naibu Waziri wake Dr. Suzan Kolimba.

Katika mazungumzo hayo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Suzan alisema wako Zanzibar kufuatilia Rasimu ya Matayarisho ya Ripoti ya Utawala Bora Barani Afrika kwa upande wa Zanzibar inayotakiwa kutayarishwa na Wizara zilizo chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dr. Suzan alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Ripoti ya Utawala Bora Barani Afrika itakuwa ndio Mpango Kazi kwa Maraisi wa Mataifa ya Bara la Afrika watakayoiwakilisha katika Kikao cha Umoja wa Afrika {AU} kinachotarajiwa kufanyika Mwezi Febuari mwaka 2018.

Alisema hatua ya awali ya matayarisho ya Ripoti hiyo imeonyesha mafanikio kwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mfano bora wa Rasimu yake ya Utawala Bora kiasi cha Wataalamu wa masuala ya Kisiasa wa Bara la Afrika kushauri iwe kigezo cha kuigwa na Mataifa mengine Barani Afrika.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
28/11/2017.

Balozi wa China Nchini Tanzania Bibi Wang Ke akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha Rasmi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Mabalozi wa China Nchini Tanzania na yule aliyepo Zanzibar.
  Balozi Seif akiagana na Ujumbe wa Kidiplomasia wa Ubalozi wa China Nchini Tanzania na Ule wa Zanzibar mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiagana na Balozi wa Tanzania Nchini Misri Meja Jegerali Issa Suleiman Nassor aliyekaa upande wa Kulia yake na Balozi Abdulrahman Kaniki aliyekaa upande wa Kushoto walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kushika nyadhifa hizo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Suzan Kolimba Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa Zanzibar na Ujumbe wake kufuatilia rasimu ya Utawala Bora Afrika kwa Wizara za SMZ.

  Balozi Seif akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhan Muombwa Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Kati kati yao ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Suzan Kolimba.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »