MKURUGENZI MKUU MSD AFANYA ZIARA HOSPITALI JIJINI DAR ES SALAAM

November 28, 2017
 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu (kushoto), akizungumza na viongozi mbalimbali wa Hospitali ya Sinza alipofanya  ziara ya kikazi katika Hospitali hiyo na  Mwananyamala jijini Dar es Salaam leo, ili kubaini changamoto zilizopo za  upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja. Kutoka kulia ni Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, Celestine Haule na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Sinza, Chrispin Kayola.
 Maofisa wa Hospitali ya Sinza wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu (hayupo pichani)
 Mkutano ukiendelea.
  Mganga Mkuu wa Hospitali ya Sinza, Chrispin Kayola, akizungumza katika mkutano huo.
 Laboratory Manager wa Hospitali ya Sinza, Emmanuel Kiponda, akichangia jambo kwenye mkutano huo.
 Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam, Celestine Haule, akizungumza kwenye mkutano huo.
 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu, akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa Hospitali ya Sinza baada ya kufanya nao mazungumzo.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu, akiwa katika picha ya pamoja na maofisa mbalimbali wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala.


Na Dotto Mwaibale

MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Laurean Bwanakunu amewatembelea wateja wa MSD wanaohudumiwa na Kanda ya MSD Dar e's Salaam ukiwa ni pamoja na Hospitali ya Mwananyamala na Sinza kubaini changamoto zilizopo katika upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ili kuzipatia ufumbuzi.

Katika ziara hiyo iliyofanyika jumanne jijini Dar es Salaam Bwanakunu amewataka wateja hao kufanya Maoteo ya mahitaji yao sahihi na kuyawasilisha Msd kwa wakati kwa mujibu wa sheria yaani tarehe 30 Januari kila mwaka,hasa dawa na vifaa tiba vinavyonunuliwa kwa Manunuzi maalumu.

Bwanakunu alihimiza watoa huduma katika hospitali hizo kutambua jukumu walilonalo katika usimamizi wa matumizi ya dawa na vifaa tiba kwa wananchi.

Akizungumza akiwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala Bwanakunu alisema anazitambua changamoto zilizopo za usambaji wa dawa na vifaa tiba na wamedata msaada wa magari kutoka Global Fund ambayo yataboresha usambazaji kutoka mara nne kwa mwaka hadi mara sita kwa mwaka.

Kuhusu vifaa vya Manunuzi maalumu Bwanakunu amesema hospitali zikiwa zinaomba kwa wakati mmoja ingerahisisha kuagiza vifaa hivyo mapema,badala ya kila hospitali kuleta kwa wakati wake.

"Vifaa hivi tunaagiza nje ya nchi na mchakato wake unachukua muda mrefu na changamoto kubwa " alisema Bwanakunu.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Sinza, Chrispin Kayola alisema hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali hiyo kwa sasa ni asilimia  80 .

"Changamoto iliyopo ni uhaba wa vitendanishi vya maabara na vifaa vya macho na meno ambavyo tunapata chini ya kiwango hivyo havikidhi mahitaji tuliyonayo," alisema.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Daniel Mkungu alisisitiza haja ya ushirikiano baina ya Hospitali hizo na MSD ili kuboresha huduma za afya hapa nchini.

Ziara hiyo ya mkurugenzi huyo itaendelea tena kesho katika baadhi ya hospitali zilizopo jijini Dar es Salaam.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »