Shaka awafunda Wagombea UVCCM

July 04, 2017


VMM/U.80/8/Vol.II/10       02/07/2017

*TAARIFA MUHIMU KWA WAGOMBEA WA UVCCM KATIKA DHAMIRA  YA KUJENGA HAIBA YA DEMOKRASIA YA KWELI NA KURUDISHA UPYA MAADILI NA NIDHAMU YA  UCHAGUZI HURU*

Demokrasia ni jambo muhimu linalohitajika kuheshimiwa na kuenziwa ndani na nje ya Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa miaka kadhaa kumekuwa na shutuma pia tuhuma zilizokaribia kuotesha mizizi ya kuwepo  rushwa ambazo nusra zivunje heshima ya chama chetu  na jumuiya zake. Jambo hilo sasa  halitaruhusiwa tena wala kuachiwa lifanyike .

Kiongozi wa UVCCM mahali popote atachaguliwa baada ya kufanyika chaguzi huru na za haki, kuzingatia Kanuni na Taratibu za Uchaguzi kama zilivyoagizwa na vikao husika bila ya kukiuka, kupuuzwa au kuvunjwa.

Nia ya UVCCM ni kujenga haiba mpya na njema ya kuheshimu misingi ya demokraia ya kweli, kuwa na adabu na kufuata nidhamu, miiko na maadili kwa kila anayetaka kuchagua au kuchaguliwa.

Jana Jumapili tarehe 02/07/2017 zoezi la utoaji fomu kwa Waombaji wa nafasi mbali mbali za Uongozi katika Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM lilianza rasmi ngazi ya Wilaya, Mikoa na Taifa.

• Kwa Ngazi ya Taifa nafasi zote fomu zinatolewa Dodoma ghorofa ya 3 chumba Na. 45, Ofisi Ndogo za UVCCM Dar es Salaam ghorofa ya 7 na Afisi Kuu ya UVCCM Gymkana Zanzibar.

Fomu zote zirejeshwe si zaidi ya tarehe 10/07/2017 Saa 10.00 Jioni katika maeneo yaliyoainishwa.

Ifahamike kuwa kila  Kijana wa Chama Cha Mapinduzi  ana haki ya msingi kugombea nafasi yoyote ile kwa mujibu wa Kanuni ya UVCCM na katiba ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM).

•Kama iliyo Haki na Wajibu wa mwanachama kugombea, kuchagua au kuchaguliwa, ndivyo inayostahili mwanachama kufuata taratibu na kuheshimu kanuni pamoja na taratibu za uchaguzi.

•UVCCM imekusudia kurudisha nidhamu ya Chama hasa katika suala zima la kugombea nafasi za uongozi na haki ya kuchagua au kuchaguliwa.

•Muomba nafasi anayo haki ya kutia nia, kuchukua fomu ya kuwania Uongozi bila ya kufanya mbwembwe, shengesha au mikogo ambayo kwa namna moja au nyingine itaonyesha hali ya kujinadi mapema, kujitangaza na kufanya kampeni.

•  Muomba nafasi yoyote ajaze fomu zake kwa uangalifu, azingatie tarehe na siku ya kurudisha mahali husika tena kwa kujali wakati uliopangwa kikanuni na kuheshimu taratibu.

•Sifa au wasifu wa kila muomba nafasi kwa kadri atakavyojaza fomu yake utajielekeza na kuandikwa kama ilivyo katika kitabu maalum cha wagombea wote ambacho kitasomwa na wajumbe wapiga kura siku ya uchaguzi husika hivyo ni vyema kuwa makini na taarifa zako.

•Ni marufuku na hatakiwi kabisa muomba nafasi yoyote ile Mara baada kuchukua au kurejesha fomu kuandika bango au kipepeprushi na kuvigawa, kuvieneza au kuwatuma wapambe wake wakati taratibu nyengine za vikao bado hazijakamilika.

*Kila muomba nafasi atapata nafasi ya kujieleza, kutoa wasifu wake, kutaja dhamira na malengo yake mbele ya wajumbe wa Mkutano husika wa kuchaguliwa si kinyume na hivyo baada ya taratibu za Vikao kukamilika.

•Kuanza mapema kampeni au wapambe kufanya ushabiki wa kisiasa na kumnadi, kumpiiga debe pia kwenda katika vyombo vya habari na kueleza wasifu, sifa au kutaja nafasi anayogombea na kujinadi kutahesabika ni kufanya kampeni mapema na kumfanya apoteze sifa.

•Ni marufuku na haitaruhusiwa kabisa muda ukifika kwa mgombea yeyote kufanya kampeni za kihuni kwa kutumia lugha chafu, siasa za maji taka, matusi, dharau kinyume na ubinadamu pia kushiriki kejeli dhidi ya wenzake.

•Muomba nafasi katika ngazi yeyote ambaye hatazingatia wala kuheshimu na kutofuata maelekezo haya anaweza kujipotezea sifa ya kuteuliwa na kushiriki kwake katika chaguzi huru na za kidemokrasia ndani ya UVCCM

*ANGALIZO:*

• Kuachia hayo yote yafanyike bila ya kuyadhibiti , kuyaasa na kuyakemea ni mwanzo wa kuiruhusu au kufungua milango atakayopita adui rushwa .

•Rushwa ni kikwazo cha maendeleo ya demokrasia na adui hatari wa haki, haitakubalika wala kuruhusiwa muomba nafasi  kutoa au kupokea na kugawa rushwa ndani ya chaguzi za jumuiya yetu.

•Chaguzi za jumuiya zitafanyika kwa njia huru na za  uwazi huku kila na mgombea akipitishwa jina lake na vikao husika vya Kikanuni na Kikatiba  baada ya kuonekana kuwa amekidhi masharti  na kufuata kanuni za uchaguzi katika kila hatua husika bila kukiuka.

•Uchaguzi ni kipimo cha ukomavu wa demokrasia ya kweli bila kufanyika mizengwe na hila ndani ya jumuiya kwa lengo la kusimamia shabaha na misingi sahihi itokanayo na miongozo, maelekezo na kuheshimu utaratibu unaohimizwa na  Chama Cha Mapinduzi na kutii maelekezo yanayotolewa mara kwa mara na Mwenyekiti wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

•Waomba nafasi hawaruhusiwa kutembea toka Wilaya au  Mkoa mmoja hadi mwingine, kukusanya wajumbe, kujinadi au kuelezea dhamira yake ya kuchukua fomu kabla ya siku ya uchaguzi kwani kuyaachia hayo na mengine yafanyike huko ni kuipalilia rushwa istawi ndani ya chaguzi zetu .

Ni matumaini yangu kuwa Vijana mtaendelea kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuomba Uongozi kutimiza haki yenu ya Kidemokrasia ndani ya Jumuiya yetu.

Nawatakia kila la heri.

*KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI*

*Shaka Hamdu Shaka* *(MNEC)*
*KAIMU KATIBU MKUU*

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »