Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais, Mhe. Januari Makamba (MB) akizungumza na waandishi wa habari
(hawapo pichani) alipokuwa akitoa uamuzi wa kutengua uteuzi wa wajumbe
saba wa Bodi ya Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) na uteuzi wa
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu
wa Ofisi ya Makamu wa Rais Profesa Faustine Kamuzola.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais, Mhe. Januari Makamba (MB) akifafanua jambo mbele yanwaandishi wa
habari (hawapo pichani) akitangaza uamuzi wa kutengua uteuzi wa wajumbe
saba wa Bodi ya Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) pamoja na uteuzi wa
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC ofisini kwake leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto
ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Profesa Faustine Kamuzola na
kulia ni Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Richard
Muyungi.
Baadhi ya waandishi wa habari
wakiwa kazini wakati wa mkutano wao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais, Mhe. Januari Makamba (MB) alipokuwa akitangaza uamuzi wa
kusitisha uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Mazingira
(NEMC) na wajumbe saba wa Bodi ya baraza hilo leo Jijini Dar es Salaam.
Picha na: Frank Shija – MAELEZO
………………………………………………………………………….
Frank Mvungi –Maelezo
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba (Mb) ametengua uteuzi
wa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Usimamizi wa
Mazingira (NEMC) na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ili kuongeza tija na
kutekeleza kwa vitendo dhana ya Ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Kwa kuzingatia mamlaka
aliyonayo Waziri chini ya Sheria ya Mazingira kifungu cha 19 (2) anaweza
kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Baraza hilo na wajumbe wake.
Akizungumza na vyombo vya Habari
leo Jijini Dar es Salaam Waziri Makamba amesema kuwa lengo la mabadiliko
hayo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na usimamizi na uzingatiaji wa Sheria
ya Mazingira na uharakishaji wa miradi ya maendeleo na uwekezaji hasa
ujenzi wa viwanda kama azma ya Mheshimiwa Rais John Magufuli
inavyoelekeza.
Kufuatia mabadiliko hayo Waziri
Makamba amemteua Dkt. Elikana Kalumanga ambaye ni Mhadhiri katika
Taasisi ya Usimamizi na Tathmini ya Rasilimali Asili,Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC hadi Rais atakapoteua
Mkurugenzi Mkuu.
“Utendaji wa NEMC umekuwa
ukilegalega sana na umekuwa hauridhishi na kumekuwepo na malalamiko
mengi kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuhusu
ucheleweshaji na urasimu usiokuwa wa lazima katika mchakato wa tathmini
ya athari kwa mazingira (EIA)” Alisisitiza Mhe. Makamba
Aliongeza kuwa ametengua uteuzi
wa wajumbe wote saba wa Bodi ya NEMC ili baadaye ateue wajumbe wapya
ambao wataendana na kasi na ari ya Serikali ya Awamu ya Tano katika
kuelekea uchumi wa Viwanda, ambapo Mwenyekiti wa Bodi ambaye mamlaka
yake ya uteuzi ni Mheshimiwa Rais,ataendelea kuwepo hadi Mheshimiwa Rais
atakapoteua mwingine.
Akifafanua Makamba amesema kuwa
changamoto nyingine zilizobainika ni kuwaelekeza wawekezaji kwa
makampuni ya kufanya Tathmini ya athari za mazingira ambayo yanamilikiwa
au yenye ubia na watumishi wa NEMC, bila kujali mgongano wa kimaslahi
jambo ambalo haliruhusiwi katika utumishi wa umma.
Jambo jingine ni kuwarundikia
maandiko ya miradi ya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) watumishi
wachache wakati wengine hawana kazi ili waelekeze miradi hiyo katika
makampuni ambayo baadaye huwapatia malipo yasiyo halali.
Hatua nyingine zilizochukuliwa na
Waziri Makamba ni pamoja na kuiagiza NEMC kufuta watu binfsi na
Makampuni yote ya ushauri wa EIA (Consultants) ambayo hayana sifa au
yameshindwa kutekeleza kazi zao vizuri na watangaze kwenye magazeti
orodha ya watu na makampuni yanayoruhusiwa kufanya kazi kama washauri
elekezi.
Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira NEMC ni muhimu katika kuhakikisha ustawi wa
mazingira na mustakabili wa maendeleo endelevu ya nchi tunapoelekea kuwa
Taifa la uchumi wa viwanda lazima usimamizi wa mazingira uwe thabiti.
EmoticonEmoticon