Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa juhudi zake za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Prof. Kabudi alitoa pongezi hizo Julai 4, 2026, alipotembelea Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo pia aliwahimiza wananchi kutembelea banda hilo ili kujipatia elimu, ushauri wa kitaalamu na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo.
Akiwa katika banda hilo, Prof. Kabudi alijionea shughuli zinazotekelezwa na taasisi mbalimbali, ikiwemo DCEA, ambayo inaendelea kutoa elimu ya kinga dhidi ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na madhara yake kwa jamii.
Alisema Banda Jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu limeandaliwa kwa lengo la kuwapatia wananchi taarifa sahihi kuhusu majukumu ya ofisi hiyo na taasisi zake, pamoja na kuwawezesha kupata huduma mbalimbali, ushauri wa kitaalamu na mwongozo wa namna ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Aidha, alisema maafisa waliopo katika banda hilo wamepewa jukumu la kusikiliza maoni ya wananchi, kupokea changamoto zao na kuwapa maelekezo sahihi ili kuhakikisha wanapata huduma stahiki kwa wakati.
"Nawahamasisha wananchi wenye changamoto mbalimbali au wanaohitaji kupata ufumbuzi wa masuala yanayowakabili watembelee Banda la Ofisi ya Waziri Mkuu. Hapa watapata ushauri, maelekezo na huduma zitakazowasaidia kutatua changamoto zao," alisema Prof. Kabudi.
Prof. Kabudi alisema Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yamekuja wakati Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, jambo linaloyafanya kuwa jukwaa muhimu la kuonesha mafanikio ya Serikali na mchango wa taasisi mbalimbali katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa.
Alieleza kuwa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali inalenga kujenga taifa jumuishi lenye ustawi, haki, amani na uchumi imara unaojitegemea. Alisisitiza kuwa wananchi wana nafasi kubwa ya kuchangia utekelezaji wa dira hiyo kwa kushiriki kikamilifu katika kupata elimu na kutumia huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali za Serikali.
Katika maonesho hayo, taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu zinaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma wanazozitoa, kupokea maoni ya wadau na kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu yao, hatua inayolenga kuimarisha uwajibikaji na kuendelea kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

EmoticonEmoticon