Mkuu wa Kitengo cha Tehama na mawasiliano kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) bwana Desderi Wengaa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakufunzi wa mfumo wa Uhasibu na utoaji taarifa za fedha.Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya wakufunzi wa mfumo wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha kutoka mikoa ya Ruvuma, Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga na Dar es salaam wakishiriki mafunzo hayo yaliyofunguliwa jana
Mtoa mada wa mafunzo ya wakufunzi wa mfumo wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha kwa njia ya kielektroniki kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI bwana Hamis Zikatimu akitoa mada wakati wa mafunzo hayo yanayofanyika mkoani Mtwara.
Mgeni rasmi Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara bwana Elias Nyamusami.(aliyeketi katikati akiwa katika picha ya pamoja na washiriki kutoka mkoa wa Tanga. Aliyeketi kushoto kwa Mgeni rasmi ni Mkuu wa Kitengo cha Tehama na mawasiliano kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) bwana Desderi Wengaa na kulia kwa Mgeni rasmi ni bwana Lucas Mrema ambaye ni mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI
Mgeni rasmi Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara bwana Elias Nyamusami.(aliyeketi katikati akiwa katika picha ya pamoja na washiriki kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).
……………………..
Na Mathew Kwembe,Mtwara
Serikali imesema kuanza kutumika kwa mfumo wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha kwa ngazi ya kituo cha kutolea huduma ifikapo julai mosi, 2017, kutapunguza changamoto za halmashauri kupata hati zenye mashaka pindi zinapokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Mfumo huo utaiwezesha Serikali kupeleka rasilimali fedha moja kwa moja kwenye vituo vya afya kwa ngazi za halmashauri. Vituo vya kutolea huduma ambavyo vitapokea fedha hizo vinajumuisha Zahanati, Vituo vya Afya, na Hospitali za Wilaya. Zoezi hilo litaenda sambamba na inavyotekelezwa kwenye sekta ya elimu, Serikali za Vijiji na Ofisi za Kata.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bwana Alfred Luanda ameyasema hayo jana mjini Mtwara wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakufunzi wa mfumo wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha kwa ngazi ya kituo cha kutolea huduma kwa wahasibu kutoka halmashauri za mikoa sita ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Tanga, Pwani na Dar es salaam.
Mafunzo kama hayo pia yanafanyika katika kanda nyingine za Mbeya, Dodoma, na Shinyanga ambapo jumla ya wakufunzi 490 kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma ujulikanao kwa Kiingereza kama Public Sector Systems Strengthening, (PS3) wanashiriki.
Alisema kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa taarifa sahihi za rasilimali fedha zilizopo katika vituo vya huduma na hivyo kusababisha halmashauri nyingi nchini kushindwa kutoa taarifa sahihi za matumizi ya ruzuku zinazotolewa katika vituo hivyo.
Katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Miundombinu bwana Elias Nyamusami, Katibu Tawala wa Mkoa aliongeza kuwa kukosekana kwa mfumo wa uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha umezifanya halmashauri zionekane kwamba zinasababisha kwa makusudi upotevu wa fedha.
“Ukweli ni kwamba hakukuwa na mfumo sahihi wa kuzisaidia halmashauri kulizuia hilo,” alisema.
Aliongeza kuwa mfumo huo mpya wa kupatiwa rasilimali fedha utatoa motisha kwa vituo vya kutolea huduma za afya na kuongeza kipaumbele cha utoaji huduma bora kwa wananchi wa Tanzania na kuongeza usawa na uwazi.
Alisema kuwa mfumo huo umeundwa kuweza kukidhi changamoto mbalimbali za miundombinu, ikiwemo umeme, na kutokuwa na upatikanaji wa mtandao kwa baadhi ya vituo vya kutolea huduma katika halmashauri mbalimbali na hivyo mfumo huo hautakuwa tu katika muundo wa kielektroniki, lakini pia kutakuwa na muundo wa kujaza kwenye vitabu.
“Mfumo wa kujaza katika vitabu na wenyewe umeboreshwa na kuwa rahisi kwa mtumiaji kujaza taarifa sahihi, na huu utatumika kwa vile vituo ambavyo changamoto ya upatikanaji wa miundombinu wezeshi katika matumizi ya kielektroniki,” alisema na kuongeza kuwa mara baada ya kujaza katika vitabu, takwimu hizo zitaingizwa katika mfumo kwenye ngazi ya halmashauri na vituo kupatiwa taarifa ya vituo vyao.
Alisema kuwa upelekaji wa Rasilimali Fedha moja kwa moja kwa vituo vya kutolea huduma utahakikisha kuwa Fedha zinazotolewa na Serikali zinatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa. Mkakati huo mpya wa kuboresha sekta za afya na elimu ni msaada kutoka Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).
Awali Mkuu wa Kitengo cha Tehama na Mawasiliano kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) bwana Desderi Wengaa alisema kuwa mfumo huo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS) unasaidia utekelezaji wa utoaji wa rasilimali fedha moja kwa moja kwa ngazi za vituo vya kutolea huduma kwa kuimarisha uhitaji wa kuwepo kwa usimamizi wa fedha katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma.
Alisema kuwa FFARS itawapatia watoa huduma mfumo sanifu uliorahisishwa ambao utawawezesha kutunza taarifa za fedha zinazotolewa na zilizopo katika vituo vyao.
Bwana Wengaa aliongeza kuwa FFARS itaweza kufuatilia matumizi ya fedha hizo katika kufikia malengo ya utoaji huduma na kuhakikisha yanaendana na sheria za manunuzi na utoaji taarifa.
“Taarifa hizi zitasaidia Serikali kuimarisha Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma na kuongeza uwazi, na hivyo watoa huduma wa afya kuwa na wajibu kwa jamii wanayoihudumia,” alisema.
Wakufunzi 490 wataweza kutoa elimu kwa watumiaji wa mwisho wa mfumo wa FFARS katika zaidi ya Vituo vya Afya 550, Zahanati 6800, Hospitali za Wilaya 135, na takribani Shule za Msingi na Sekondari 20,000 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, vikiwemo vituo vya kutolea huduma kutoka Mikoa 13 na Halmashauri 93 zinazotekeleza Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).
EmoticonEmoticon