BRIGEDIA JENERALI NDAGALA AFUNGUA KONGAMANO LA WADAU WA USIMAMIZI WA MAAFA JIJINI MBEYA

October 12, 2025


Wadau watakiwa kutoa mapendekezo yenye tija kuboresha usimamizi wa maafa nchini


NA. MWANDISHI WETU – MBEYA


MKURUGENZI wa Idara ya Menejimenti ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Brigedia Jenerali Hosea Ndagala amefungua Kongamano la Wadau wa Usimamizi wa Maafa linalofanyika kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Athari za Maafa kwa mwaka 2025.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo leo 12 Oktoba 2025 jijini Mbeya, Brigedia Jenerali Ndagala aliwataka washiriki kuja na mapendekezo yenye tija katika usimamizi wa maafa.

 “Kongamano hili limekusudiwa kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto, na kutoa mapendekezo ya kuboresha mifumo ya kitaifa ya usimamizi wa maafa.


Alisisitiza kuwa:”Nitoe wito kwa washiriki wote kushiriki kikamilifu katika mijadala, kwa sababu michango yenu ni muhimu katika kuhakikisha tunapata mapendekezo yatakayokuwa na tija katika usimamizi wa maafa.

Vilevile aliwataka washiriki kutumia fursa hiyo kuimarisha ushirikiano na kubuni njia mpya za kuongeza ustahimilivu wa jamii zetu ili kupunguza athari za maafa na kulinda maisha na mali.

Brigedia Jenerali Ndagala aliwashukuru wadau wote wanaoendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu katika juhudi za kujenga Taifa lenye ustahimilivu dhidi ya majanga.


Alisema mchango wao katika kupanga, kutekeleza, na kufuatilia mipango ya usimamizi wa maafa nchini umeendelea kuwa wa thamani kubwa.

Kwa upande wake, Inspector Damian Muheya kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji amesema kuwa, ili kufanikisha ustahimilivu endelevu usio na maafa, ni muhimu jamii kushiriki kikamilifu katika hatua za kinga na tahadhari dhidi ya majanga.



Naye Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Dkt. Barnabas Msongaleli ameeleza Taasisi yao imeendelea kutoa mchango katika kuzalisha wataalam wa kada ya usimamizi wa maafa nchini ili kuwa na wabobezi wa eneo hili na kuendelea kuleta tija katika masuala ya menejimenti ya maafa. 

“UDOM tumeendelea kutoa elimu, tunaendesha shahada ya awali ya menejimenti ya vihatarishi vya maafa ( Bachelor of Disaster Risk Management). Pia tunafanya tafiti mbalimbali zinazohusu kupunguza au kuzuia vihatarishi  vya maafa. Na kutoa huduma kwa jamii kwa njia ya kuwafikia jamii kuwapa elimu ya vihatarishi vya maafa na namna bora ya kukabiliana na maafa kabla hayajatokea,” alisisitiza Dkt. Msongaleli.


=MWISHO=

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »