Chalinze na kompyuta za Bayport

May 12, 2017
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri mpya ya Chalinze mkoani Pwani, Edes Lukoa mwenye koti jeusi, akipokea msaada wa kompyuta mbili kutoka kwa Mratibu wa Masoko wa Bayport Fiancial Services, Mercy Mgongolwa. Wanaoshuhudia ni Meneja wa Kanda ya Kati Christopher Kihwele kushoto kwa Mercy na Meneja wa wa Bayport Bagamoyo Francis Sumila na Katibu wa Mbunge wa Chalinze Ridhiwan Kikwete Idd Swala kulia kwa Mkurugenzi wa Chalinze.

Bayport yaikomboa Halmshauri mpya ya Chalinze kwa kuwapatia kompyuta

Na Mwandishi Wetu, Chalinze
TAASISI ya Kifedha ya Bayport Financial Services, jana iliikomboa Halmashauri mpya ya wilaya Chalinze kwa kuipatia kompyuta mbili kwa ajili ya kupunguza changamoto za upungufu wa vifaa vya kiutendaji, ikiwa ni miezi michache tangu kuanzishwa kwa Halmashauri hiyo mpya.

Kompyuta hizo zilipokewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Edes Lukoa katika ofisi yake, ikiwa na lengo la kuhakikisha kuwa Halmashauri hiyo inatimiza wajibu wake wa kuwatumikia wana Chalinze na Watanzania kwa ujumla kwa kutumia kompyuta hizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze Edes Lukoa akipokea kompyuta mbili kutoka kwa Taasisi ya Bayport Financial Services ikiwakilishwa na Mratibu wa Masoko Mercy Mgongolwa.
Akizungumza jana katika makabidhiano hayo wilayani Chalinze, Mratibu wa Masoko wa Bayport Financial Services, Mercy Mgongolwa, alisema kwamba lengo la kuipatia kompyuta hizo linatokana na dhamira ya kuona wilaya hiyo inasonga mbele kimaendeleo.

Alisema kugawa kompyuta hizo ni mwendelezo wa nia yao baada ya kuzindua ugawaji wa kompyuta hizo 205 zilizoanza kusambazwa katika ofisi mbalimbali za serikali baada ya kuzinduliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki.

“Tumefika katika Halmashauri hii kutoa kompyuta kwa Halmashauri ya Chalinze huku ikiwa tumeshafikisha msaada kama huu katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kama vile Morogoro, Mwanza, Mara, Mbeya, Kilimanjaro na kwingineko.

"Tunaamini kwamba msaada huu utakuwa na dira nzuri kwa watumishi wa umma wa Halmashauri hii ambayo ni mpya, hivyo ni madhumuni yetu kuona wanapata vitendea kazi vizuri ili wafanikiwe kuwatumikia Watanzania,” Alisema Mercy.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Edes Lukoa aliwashukuru Bayport kwa msaada wa kompyuta kwa ajili ya ofisi yao ambayo ni mpya baada ya kugawanywa kutoka katika Halmashauri ya Wilaya Bagamoyo.

“Tumepokea kwa furaha msaada wa kompyuta hizi na tunaamini kwa dhati kabisa itapunguza au kurahisisha utendaji kazi katika ofisi zetu za Halmashauri ya Chalinze kama wenyewe mlivyokusudia kwa kuanzisha utaratibu wa msaada huu.

“Tunaahidi kwamba tutazitumia vizuri kompyuta hizi pamoja na kufikisha huduma iliyokusudiwa kwa watu wote, ukizingatia kwamba kukua kwa sayansi na teknolojia kunalazimisha ofisi kutumia kompyuta ili kurahisisha utendaji kazi,” Alisema Lukoa.

Zoezi la kutoa msaada wa kompyuta katika ofisi mbalimbali za serikali lilianza mwishoni mwa mwaka jana, ambapo katika maeneo yote ambayo wamepeleka vifaa hivyo wamepokea vizuri na kuahidi utendaji kazi mzuri kwa utumia rasilimali hizo, huku Bayport ikiendelea kusambaza vifaa hivyo katika maeneo mengine yaliyopangwa na serikali kwa kupitia Wizara ya Utumishi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »