Waziri
wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (kulia)
akimkaribisha Balozi wa Ujerumani hapa nchini, Mhe. Egon Konchanke
alipomtembelea jana tarehe 11 Julai, 2016 ofisini kwake, Mpingo House,
Jijini Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali yanayohusu sekta ya
Maliasili nchini.
Waziri Maghembe (kulia) akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Balozi Konchanke (kushoto).
Balozi Konchanke (kushoto) akimueleza jambo Prof. Maghembe (kulia) katika mazungumzo hayo.
Balozi
Konchanke (kushoto) akimuonesha Waziri Maghembe (kulia) ramani ya
Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambayo Balozi huyo ameahidi kushirikiana na
Serikali ya Tanzania katika kuendeleza utalii wake kwa pamoja na ule wa
Mkoa wa Kigoma (Hifadhi ya Mahale)
Waziri Maghembe (kulia) akizungumza katika kikao hicho.
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii
imeweka wazi msimamo wake kuwa haitauza meno yake ya Tembo yaliyohifadhiwa kwa
kuwa kufanya hivyo ni kuongeza upatikani wa meno hayo kwenye soko hivyo kuchochea
biashara haramu ya ujangili.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof.
Jumanne Maghembe alipokuwa kwenye mazungumzo ya na Balozi wa Ujerumani hapa
nchini, Egon Konchanke ofisini kwake Mpingo House, Jijini Dar es Salaam.
Balozi Konchanke alimueleza Prof. Maghembe kuwa, mwezi
Septemba mwaka huu (2016), Wanachama wa Mkataba wa Kimataifa unaosimamia
biashara ya Viumbe vilivyo hatarini kutoweka vya wanyama na mimea (CITES) watakutana nchini Afrika ya
Kusini kujadili mambo mbali mbali ikiwemo baadhi ya nchi wanachama ikiwemo
Namibia kutaka kuuza Meno yake ya Tembo yaliyohifadhiwa ili kujipatia kipato.
Katika maelezo yake Balozi Konchanke alimuomba Prof. Maghembe
kutoa msimamo wa Serikali ya Tanzania kuhusu hoja hiyo ya kuuza meno ya tembo
yaliyohifadhiwa kutokana na matukio ya Ujangili na vifo asilia vya wanyama. “Ni
upi msimamo wa Tanzania katika kuelekea mkutano huo kuhusiana na uamuzi wa nchi
kama Namibia wa kuuza meno yake ya tembo yaliyohifdhiwa?” aliuliza Balozi Konchanke.
Katika majibu yake Prof. Maghembe alisema “Tanzania
tunaungana na mataifa mengine ambayo yanapinga uuzwaji wa meno ya tembo, Kama
tukiuza meno haya tutaongeza upatikanaje wake kwenye masoko, hivyo kuchochea
zaidi biashara hii haramu, hatuna sababu ya kuyauza wala kuyachoma moto,
ukiyachoma moto unakuwa umechoma kila kitu ikiwemo sampuli ambazo zingeweza
kutumika kwenye tafiti mbalimbali zikiwemo za kutengeneza madawa ya kutibu
maradhi ya wanyama hao”. Aliongeza kuwa nchi zitakazofanya hivyo zitakuwa
hazijafanya jambo la busara zaidi ya kuleta maafa kwa nchi jirani ya kuongezeka
kwa vitendo vya ujangili.
Wakati huo huo, Waziri Maghembe alimuomba Balozi Konchanke
kuleta wawekezaji kutoka Ujerumani kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya Utalii
na Uhifadhi hapa nchini. Balozi huyo aliahidi ushirikiano kwa Serikali ya
Tanzania ambapo alisema mwishoni mwa mwezi huu wa Julai Waziri wa Ushirikiano
wa Kiuchumi na Maendeleo wa Serikali ya Ujerumani Dkt. Gerd Muller atakuja nchini
na wafanyabiashara kutoka nchini humo wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya
Uhifadhi na Kilimo.
Balozi Konchanke ameahidi pia kushirikiana na Serikali ya
Tanzania katika kuendeleza Utalii kwenye Mikoa ya Kigoma na Katavi kwa
kuunganisha utalii wa Hifadhi ya Mahale na Hifadhi ya Katavi. Amesema kuwa eneo
hilo linahitajika kuwekewa miundombinu mizuri ya barabara ili liweze kufikika
kirahisi.
Kwa upande wake Waziri Maghembe amesema kuwa utalii katika
Mikoa hiyo unapewa nafasi kubwa ili uweze kukua na kuliingizia zaidi taifa
mapato. Ameeleza kuwa katika kukabiliana na changamoto ya usafiri zitaansishwa
safari za ndege za bei nafuu mara tatu kwa wiki kutoka Dar es Salaam kwenda Mikoa
ya Kigoma na Katavi kwa bei ya dola za kimarekani 150.
Akizungumzia kuhusu kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye
huduma za Utalii wakati akijibu hoja ya Balozi Konchanke juu ya malalamiko ya
watoa huduma hizo kuwa sheria hiyo imekuja ghafla na inapunguza ujio wa watalii
nchini, Waziri Maghembe alisema sheria hiyo imepitishwa na bunge na watoa
huduma hao walishataarifiwa toka mwaka jana (2015) juu ya mabadiliko ya sheria
hiyo kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mabadiliko yake. Aliongeza kuwa ili
Serikali ijiendeshe inahitaji mapato na kwamba watalii wanalipa kodi hivyo na watoa
huduma nao wanahitajika kulipa kodi.
Katika hatua nyingine Balozi Konchanke aliomba ufafanuzi kwa
Waziri Maghembe juu utaratibu mpya wa mashirika ya umma kupeleka fedha zote za
makusanyo hazina na kwamba kama wahisani wakichangia kuendeleza mashirika hayo
ikiwepo TANAPA na TAWA, pengine lengo lao litakuwa halijafikiwa na hivyo kuwa
vigumu kujiendesha. Akijibu hoja hiyo Waziri Maghembe alisema kumekuepo na
uelewa hafifu juu ya utaratibu huo ambao kimsingi Mamlaka hizo ikiwemo TANAPA
na TAWA zitapelekea fedha zao hazina na kuzitumia pale itakapohitajikwa kwa mujibu
wa mpango kazi wao.
EmoticonEmoticon