Meneja
Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Innocent
Mungy akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu tathmini ya hali halisi
kuelekea ukomo wa matumizi ya simu bandia nchini ifikapo mwezi june
2016 ambapo kiwango cha simu Bandia Kimepungua kutokana na Elimu
inayotolewa na Mamalaka hiyo kwa wananchi. Kulia ni Afisa Habari wa
Idara ya Habari Maelezo Bw. Frank Mvungi.
Kaimu
Naibu Mkurugenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Mawasiliano (TTMS) toka
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Injinia Gabriel Mruma akiwaeleza
waandishi wa habari Leo Jijini Dar es salaam kuhusu umuhimu wa kutumia
simu zenye ubora unaokubalika ili kuepuka athari zinazotokana na
matumizi ya simu Bandia. Kulia ni Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Innocent Mungy .
(Picha na Hassan Silayo- MAELEZO ).
……………………………………………………….
Frank Mvungi-MAELEZO
Serikali
imewataka wauzaji wa vifaa vya Mawasiliano vya mkononi (mobile devices)
kuacha mara moja tabia ya kubadilisha namba tambulishi (‘kuflash’) za
vifaa hivyo kwani watakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka 10 au
faini isiyopungua milioni 30 au vyote viwili.
Kauli
hiyo imetolewa na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) Bw. Innocent Mungy wakati wa mkutano na waandishi wa
Habari leo jijini Dar es salaam.
“Namba
tambulishi (IMEI) za vifaa vyote vya Mawasiliano ya mkononi ambavyo
vimeibiwa,vimeharibika,kupotea au visivyokidhi viwango vya matumizi
katika soko la mawasiliano havitaruhusiwa kuunganishwa kwenye mitandao
ya watoa huduma ifikapo tarehe 16 June 2016. “Aalisema Mungy.
Akizungumazia
kampeni ya kuelimisha umma kuhusu matumizi ya simu zote zisizokidhi
viwango, Mungy alibainisha kuwa idadi ya simu hizo imeshuka kutokana na
elimu ambayo wameitoa katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Alisema
lengo la elimu hiyo kwa umma ni kujenga uwezo kwa wananchi kutambua
simu zisizokidhi vigezo kabla ya kufika ukomo wa matumizi ya simu bandia
nchini.
Mungy
alifafanua kuwa uchambuzi wa IMEI unaonyesha kuwa hadi Februari,2016
idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa
na asilimia 3 ambapo namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa
na asilimia 18 na simu halisi zilikuwa sawa na asilimia 79.
“Kwa
mwezi Machi 2016 ulionyesha kuwa Idadi ya namba tambulishi ambazo hazina
viwango ni asilimia 4, na idadi ya zile zilizonakiliwa zilikuwa sawa na
asilimia 13 ambapo uchambuzi huu umehusisha taarifa za kampuni zote za
simu nchini’’. Alifafanua Mungy.
Aliongeza
kuwa matokeo hayo mazuri ni matunda ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya
Mamlaka hiyo, Shirika la viwango Tanzania (TBS),Tume ya ushindani
(FCC),kampuni za simu, pamoja na wadau wengine katika kuelimisha umma
juu ya uhakiki wa simu walizo azo ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya
kuzingatia wakati wa kununua simu ikiwemo kuzihakiki ubora wake.
Kwa
Upande Wake Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Kituo cha Usimamizi wa
Mawasiliano wa Mamlaka hiyo Injinia Gabriel Mruma amesema kuwa ni
vyema watanzania wakajenga utamaduni wa kununua simu zenye ubora
kuepuka usumbufu wakati Tanzania inapoelekea ukomo wa matumizi ya simu
bandia.
Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania ni Taasisi ya Serikali yenye Dhamana ya
kusimamia shughuli za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta hapa nchini.
Kuwepo
kwa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka
2010 na Kanuni zake za mwaka 2011 kumewezesha kutekelezwa kwa mfumo wa
rajisi ya namba za Utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi.
Mfumo
huu wa kielektroniki ulizinduliwa tarehe 17 Desemba 2015 na unahifadhi
kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi kwa
lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vilivyoibiwa,kuharibika au
kupotea,bandia vya mawasiliano katika soko.
EmoticonEmoticon