TANZANIA YAWA MFANO AFRIKA UTEKELEZAJI MIRADI SEKTA YA NISHATI

June 22, 2025


📌 *Ufanisi wake watambuliwa Jukwaa la Nishati Afrika*


📌 *Lesotho kujifunza Tanzania utekelezaji miradi ya Nishati*


📌 *Mhandisi Mramba aeleza umuhimu wa Sekta Binafsi katika ukuaji wa Sekta ya Nishati*


Ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya Sekta ya Nishati nchini ikiwemo ukamilishaji wa mradi wa usambazaji umeme katika Vijiji 12,318 umekuwa kivutio katika Jukwaa la Nishati Afrika linalofanyika nchini Afrika Kusini.


Kutokana na ufanisi huo unaojumuisha ukamilishaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere wa megawati 2, 115 na baadhi ya miradi ya kikanda ya usafirishaji umeme, imepelekea nchi ya Lesotho   kueleza nia yake ya kuja Tanzania ili kujifunza masuala mbalimbali yatakayoboresha hali ya umeme nchini humo.

Akizungumza katika Mkutano wa Jukwaa la Nishati Afrika jijini Cape Town nchini Afrika Kusini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba ameeleza kuwa  Watanzania wanapaswa kujivunia jinsi Sekta ya Nishati inavyofanya vizuri na kuwa nchi ya mfano barani Afrika.


"Watanzania wanaweza wasifahamu sana suala hili lakini Tanzania inatazamwa sana na mataifa mengine hasa katika eneo la nishati ambalo tunaendelea kufanya vizuri." Amesema Mhandisi Mramba

Amesema kutokana na sekta ya nishati nchini kufanya vizuri,  Wawakilishi wa Serikali kutoka  nchini Lesotho katika Jukwaa hilo la Nishati Afrika wameeleza nia ya kuhitaji Tanzania kusaidiana nao katika maeneo yatakayoboresha hali ya umeme nchini humo.


Mramba ameeleza kuwa sekta ya nishati ni sekta muhimu inayoshikilia uchumi wa nchi kwani kukua kwa uchumi kunategemea uwepo wa nishati ya kutosha na ya uhakika.


Katika Jukwa hilo la Nishati Afrika, Mramba ameeleza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi kwenye miradi ya Nishati.


Ametanabaisha kuwa,  kutokana na hali ya ukuaji wa uchumi nchini,  Tanzania kwa upande wake inaendelea kuongeza nguvu katika  maeneo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme hivyo ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu.

Katika ujenzi wa  miundombinu ya kusafirisha umeme, amewakaribisha wawekezaji kuwekeza kwenye eneo hilo akieleza kwamba Serikali pia imejipanga kuuendelea kuunganisha Tanzania na nchi nyingine ambapo kwa sasa gridi ya umeme ya Tanzania imeunganishwa na gridi za Kenya, Rwanda na Burundi na hatua zinazofuata ni kuzifikia Zambia na  Uganda.


Katika Jukwa hilo la Nishati Afrika, Watendaji kutoka Tanzania wamepata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na  wawekezaji mbalimbali walioonesha nia ya kuwekeza Tanzania katika sekta ya nishati.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »