Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ikwiriri-Mkongo iliyopo Wilayani Rufiji kwa kiwango cha lami yenye urefu wa km 27 pamoja na taa za barabarani, ambapo ujenzi utaanza hivi karibuni.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Mkongo na Ikwiriri leo Juni 23, 2025.
"Rais Samia alishaidhinisha fedha kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ikwiriri-Mkongo pamoja na taa za barabarani 180". Amefafanua Waziri Ulega.
Aidha, amesema dhamira ya Serikali ni kujenga barabara nyingine kutoka Chalinze- Mloka-Mkongo pamoja na ujenzi wa daraja la Kisasa, litakalounganisha Mkongo - Utete.
Vilevile amesema Rais Samia ameridhia ujenzi wa Barabara ya njia nne ya kutoa Ikwiriri -mpaka Mkuranga.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa amemshukuru Mhe.Rais Samia kwa kutoa fedha ya ujenzi wa barabara hizo, ambazo zinakwenda kuunganisha Rufiji na kukuza uchumi wa Wananchi.
Amesema Barabara za Rufiji zilikuwa hazipitiki hasa wakati wa mafuriko.
Katika hatua nyingine wana umoja wa wanawake wa CCM Wilaya ya Rufiji wamefanya maandamano ya amani ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kumchagua Rais Samia.
Pia wamempatia Mhe waziri Mchengerwa cheti cha pongezi kwa kutambua mchango wake katika kuwapatia wananchi wa Rufiji maendeleo.
Katika ziara ya leo Mhe. Mchengerwa alikagua miradi mbalimbali ikiwemo kituo Cha Afya Cha Mkongo, Soko la Mhe. Mchengerwa na Shule ya Sekondari ya Mkongo na kutoa maelekezo ya kuboresha huduma katika maeneo hayo.
EmoticonEmoticon