📌*Wataalamu kutoka Asia na Afrika wakutana kutafuta suhulu za kilimo, lishe na afya*
📌*WHO yasema watoto na wanawake waendelea kukumbwa na ukosefu wa virutubisho*
📌*Serikali kuendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo, lishe na afya*
📌*Sekta ya kilimo yaajiri zaidi ya asilimia 65 ya watu*
📌*Serikali yaajiri watu 137,000 kuongeza mikakati ya afya ya kidijitali*
*Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati*
Serikali imesema kuwa inatambua kufikia usalama wa chakula na lishe si tu kuhusu kuongezeka kwa mavuno bali ni kuhakikisha kwamba kile kinacholiwa kinawaimarisha wananchi na kusaidia afya zao kwa kipindi kirefu.
Hiyo inatajwa kuwa njia jumuishi iliyopo katika sera za nchi na uwekezaji unaoenda sambamba na vipaumbele vya maendeleo ya Taifa na maono ya kufikia mifumo ya chakula endelevu inayosaidia ustawi na mafanikio ya watu kama lilivyo lengo la Kongamano la Kumi la Utafiti wa Kilimo, Lishe na Afya (ANH 2025).
Akifungua rasmi Kongamano hilo leo Juni 23, 2025 jijini Dar es salaam kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa nchini Tanzania kilimo kinabaki kuwa nguzo ya uchumi inayochangia takriban asilimia 29 ya Pato la Taifa, kikiajiri zaidi ya asilimia 65 ya watu na kuhakikisha usalama wa chakula kwa mamilioni.
“Tumeendelea kuwekeza kimkakati katika sekta hii. Kwa mwaka huu, bajeti yetu ya Wizara ya Kilimo imeongezeka kwa takriban asilimia 29. Kupitia programu za ruzuku za serikali na mipango mingine ya msaada wa pembejeo, tumefikia mamilioni ya wakulima wadogo nchini kwa mbegu bora na upatikanaji wa mbolea,” amesema Dkt. Biteko
Ameongeza kuwa kupitia Mradi wa Kujenga Kesho Bora (BBT), umewawezesha vijana kushiriki katika kilimo cha kisasa, kuboresha huduma za ugani, na kuwekeza katika miundombinu ya umwagiliaji ili kufanya kilimo kuwa na ufanisi zaidi, kiuchumi na lishe ili kuwa na maendeleo bora na afya.
![]() |
Kuhusu lishe amesema ni msingi muhimu wa ajenda ya maendeleo ya kiuchumi na ya binadamu, licha ya mafanikio yaliyopatikana amesema bado zipo changamoto kadhaa akitolea mfano Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ikionesha kwamba takriban asilimia 30 ya watoto barani Afrika wenye umri wa chini ya miaka mitano bado wanakabiliwa na ukosefu wa ukuaji, wakati kiwango cha kuwa na uzito kupita kiasi kinakua. Aidha, watoto wengi na wanawake wenye umri wa kuzaa wanaendelea kukumbwa na ukosefu wa virutubisho.
Amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imepunguza uratibu wa sekta nyingi kupitia Mpango wa Kitaifa wa Hatua za Lishe (NMNAP), ambao sasa upo katika awamu yake ya pili ili kushughulikia aina zote za utapiamlo katika makundi yote ya watu. Vilevile, Tanzania inakuza uzalishaji na matumizi ya mazao yenye virutubisho hasa katika maeneo ya vijijini na yasiyo na mvua kulingana na hali za kilimo kama sehemu ya mabadiliko ya mifumo ya chakula ya ndani na kuimarisha ajenda ya nchi.
Kwa upande wa afya, Dkt. Biteko amesema Serikali inaendelea na dhamira yake ya ushirikiano katika masuala ya afya ulimwenguni, huku ikifanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu, utoaji wa huduma, na mageuzi ya mifumo ya afya pamoja na kuongeza idadi ya vituo vya afya kwa takriban asilimia 7 tangu mwaka 2021.
“Serikali imeongeza idadi ya wafanyakazi wa afya kwa kuajiri takriban wafanyakazi wa afya wa jamii 137,000 katika ngazi za msingi na kuongeza mikakati ya afya ya kidijitali. Tunashughulikia changamoto zinazohusiana na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na magonjwa ya kuambukiza na afya ya mama na mtoto kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo kutumia wafanyakazi wa afya wa jamii, wadau wengine na kampeni za kitaifa ili kuongeza uelewa na kuongeza uwezo wa kugundua mapema na kuzuia katika ngazi zote, ” amesema Dkt. Biteko
Aidha, amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wengine katika sekta ya afya, lishe na kilimo sambamba na kufaidika na ushirikiano imara na wa kimkakati na washirika wa kimataifa na taasisi nyingine za kikanda na za kimataifa. Pia, Tanzania ipo tayari kujifunza na kuongoza pale inapowezekana huku akiwaasa washiriki wa Kongamano hilo kushiriki ipasavyo ili kuwa na hoja na sera ambazo zitabadilisha mifumo ya chakula kwa afya bora na ustawi.
Amesisitiza “Tanzania pia inaendelea kushiriki katika majadiliano ya mifumo ya chakula ya bara na kimataifa, ikichangia katika Ajenda ya 63 ya Umoja wa Afrika, Mfumo wa CAADP na UN.”
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Marianne Young amesema kuwa nchi yake itaendelea kuwa mshirika muhimu kwa Tanzania na kuwa na mafanikio ya muda mrefu katika sekta za lishe, afya na kilimo.
“ Tumesaidia wanawake wajawazito milioni 6.7 kwa kuwapatia virutubisho lishe, kubadili na mitazamo ya jamii kuhusu usafi na kusadia ukarabati wa miundombinu ya upatikanaji wa maji safi vijijini kwa watu milioni 5.5, ” amesema Balozi Young.
Naye, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kisayansi ya ANH (Agriculture, Nutrition and Health Academy) Bw. Joe Yates amesema kuwa kila mwaka Kongamano la ANH hufanyika katika nchi za Afrika na Asia ambalo huwaleta pamoja watafiti, wanasayansi, watunga sera na wadau mbalimbali wa masuala ya kilimo, lishe na afya.
Lengo likiwa ni kujadili kwa pamoja, kubadilishana fikra na uzoefu na kubaini masuala mbalimbali ya kisayansi kwa ajili ya kuchagiza katika kuunda sera za maendeleo ya kilimo, lishe na afya na kwa mwaka 2025 limefanyika nchini kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).
Mwisho.
EmoticonEmoticon