KAMISHNA KUJI AZINDUA JENGO LA UTAWALA, NYUMBA ZA WATUMISHI HIFADHI YA TAIFA MTO UGALLA

June 21, 2025


Na. Edmund Salaho, Kaliua -Tabora


Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Nassoro Kuji leo tarehe 21, Juni 2025 amefanya ziara ya kikazi katika Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla iliyopo Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora na kuzindua Jengo la Utawala pamoja na nyumba za watumishi kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini ya TANAPA.


Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa majengo hayo Kamishna Kuji alisisitiza kutunzwa kwa miradi hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa faida ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

“Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendeleza juhudi za kuboresha miundombinu katika hifadhi hizi mpya kwa kuboresha miundombinu ya barabara majengo ya Utawala hifadhi, Nyumba za Askari pamoja  na Vitendea kazi vingine, hivyo, nisisitize kuitunza miundombinu hii ili iweze kutumika kwa muda mrefu”.

“TANAPA tuna kila sababu ya kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anaendelea kuiboresha sekta hii ya Utalii na Uhifadhi hapa nchini. Uwekezaji wa miundombinu hii ni mwendelezo wa adhma kubwa ya Serikali katika Hifadhi za Taifa Nchini. Tuna kila sababu ya kujivunia uongozi wake kwani matokeo ya juhudi zake yanaonekana” alisema Kamishna Kuji.


Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo

Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Moronda Moronda ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla alibainisha kuwa, Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla ilipatiwa fedha za kutekeleza mradi wa Jengo la Utawala, Nyumba za watumishi tatu (3), pamoja na nyumba ya Mkuu wa Hifadhi vyote vikigharimu kiasi cha ShsT. milioni 701.9 ambapo kwa sasa miradi hii yote imekamilika na iko tayari kwa matumizi.

Pia, Kamishna Kuji alifanikiwa kufanya kikao na Menejimenti ya hifadhi pamoja na Maafisa na Askari Uhifadhi wa hifadhi hiyo na kujadili mikakati ya namna bora ya kukuza uhifadhi na kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za utalii ili kupata mapato mengi na kutoa mchango mkubwa wa mapato katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla ni moja ya Hifadhi mpya tano zilizopandishwa hadhi mwaka 2019 na kuwa Hifadhi ya Taifa. Hifadhi hii yenye sifa kedekede kwa mandhari yake nzuri na ya kuvutia ya Mto Ugalla, Misitu ya miombo yenye makundi makubwa ya wanyama ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 3,865 na ni ya sita kwa ukubwa kati ya Hifadhi 21 za Taifa Ilizopo hapa nchini.

Uboreshwaji wa miundombinu katika katika hifadhi za Taifa hasa zile zilizopandishwa hadhi mwaka 2019 ni suala muhimu ili kuweka mazingira mazuri ya kukuza utalii na kufanikisha shughuli za utawala na uhifadhi.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »