Na. Immaculate Makilika –MAELEZO
……………………………………..
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai,
Kamishna wa Polisi Diwani Athumani amesema hadi kufikia sasa zaidi ya
watu 150 wamejitokeza kuhakiki wa silaha zao, katika hatua ya kutii
agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
“Baada ya Mheshimiwa Rais John Pombe
Magufuli kufanya uhakiki wa silaha zake hivi karibuni, watu zaidi ya
150 wakiwemo viongozi mbalimbali waliopo Serikalini, Viongozi wastaafu,
Mabalozi wa nchi mbalimbali, wafanyabiashara na wabunge wamejitokeza
kuhakiki silaha zao, na wengine wameonesha nia ya kufanya hivyo, hata
hivyo tusingependa kutaja majina yao kwa sababu za kiusalama” amesema
Kamishna wa Polisi Athumani
Athumani amesema kuwa, lengo la kufanya
uhakiki wa silaha ni pamoja na kuboresha hali ya usalama na kuwajua
watumiaji, kuwatambua tena wamiliki wa silaha pamoja na kuwa
wanawatambua isipokuwa zinaweza kutokea sababu mbalimbali zitakazofanya
wasiendelee kumiliki silaha hizo ikiwemo vifo na ulemavu na kusema
kuwa wangependa kufahamu taarifa za namna hiyo, ameongeza kuwa zoezi
hili sasa ni la nchi nzima si kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee kama
ilivyokuwa hapo awali.
Aidha, wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam
wanaweza kuhakiki silaha zao katika vituo vya Osterbay Polisi, Temeke
Chang’ombe Polisi na Ilala central Polisi, ambapo wanatakiwa kwenda na
kitabu(firearm licence book), picha ndogo nne za mhusika, pamoja na
anwani sahihi ya mahali anapoishi mhusika.
Vilevile, amewataka viongozi mbalimbali na
wananchi wanaomiliki silaha kujitokeza kwa ajili ya kufanya uhakiki wa
silaha zao huku akisisitiza kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es salaam,
wanaweza kuonana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam,
Simon Sirro na kwa wakazi wa Mikoani waonanae na makamanda wa polisi wa
Mikoa yao kwa ajili ya kupewa msaada na maelekezo zaidi ya taratibu za
kufuata ili waweze kufanya uhakiki wa silaha zao.
EmoticonEmoticon