Taasi ya Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JMKF) na kampuni ya wanasheria NEXLAW Advocates ya Dar es salaam wamesaini rasmi makubaliano ya ushirikiano (MoU) yenye lengo la kuimarisha na kukuza ujasiriamali wa vijana nchini Tanzania kupitia Mpango wa JMKF wa Kuharakisha Wavumbuzi wa Kijamii wa Kijana Leo (Kijana Leo Social Innovator Accelerator).
Hafla ya
kusaini makubaliano hayo imefanyika leo Aprili 28, 2025, katika ofisi za makao
makuu ya JMKF zilizopo Masaki, Dar es Salaam, ikishuhudiwa na Mkurugenzi Mtendaji
wa JMKF, Bi. Vanessa Anyoti, na Mshirika Mwandamizi wa NEXLAW, Profesa Saudin
Mwakaje.
Ushirikiano huu
wa kihistoria unalenga kuwawezesha vijana wajasiriamali wa kijamii kwa
kuwapatia maarifa muhimu kuhusu masuala ya kisheria, rasilimali za kufanikisha
uzingatiaji wa sheria na zana za uongozi — ambazo ni msingi muhimu kwa ujenzi
wa biashara endelevu na zinazovutia wawekezaji.
“Hili ni tukio
kubwa sana,” alisema Prof. Mwakaje. “Tuna furaha kubwa kusaini rasmi
makubaliano haya na JMKF. Vijana wengi wana mawazo bora na yenye nguvu ya
mabadiliko — lakini mara nyingi hukosa mwongozo wa namna ya kulinda,
kurasimisha au kupanua mawazo yao kwa njia ya kisheria. Ushirikiano huu utaleta
suluhisho.”
Kupitia
makubaliano haya, wataalam wa NEXLAW Advocates waliobobea katika elimu ya
kisheria na uzingatiaji wa sheria kwa sekta ya kuanzisha biashara na SME,
wataendesha moduli muhimu ndani ya Accelerator iitwayo Sheria, Uzingatiaji,
Elimu ya Fedha na Ushirikiano na Mamlaka za Udhibiti.
Moduli hii
itawapatia vijana msaada wa kitaalam wa masuala ya kisheria, msaada wa usajili
wa hati miliki, na mbinu bora za kupita katika mifumo ya udhibiti.
Kwa mujibu wa
Bi. Anyoti, mpango huu umejikita moja kwa moja katika utekelezaji wa Mpango
Mkakati wa JMKF wa 2023–2030, ambao umebaini changamoto kubwa kwa vijana kupata
huduma za kisheria na maandalizi ya kupokea uwekezaji.
“Ushirikiano
huu wa kwanza wa aina yake tunaamini utazaa matunda,” alisema Bi. Anyoti.
“Huduma za ulinzi na ushauri wa kisheria zinazotolewa na NEXLAW zitakamilisha
juhudi zetu za kuwawezesha vijana na SMEs Tanzania. Tunataka vijana wetu wasiwe
tu waotaji, bali wachukua hatua — wenye nguvu ya kufanikisha ndoto zao.”
Programu ya
Kijana Leo ilianzishwa mwaka 2021 kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu –
Idara ya Maendeleo ya Vijana (PMO-LYED) na inarushwa kupitia AZAM TV kwa lugha
ya Kiswahili.
Tangu
kuanzishwa kwake, programu hii imekuwa nembo ya kitaifa ya ujenzi wa uwezo kwa
vijana, ikigusa sekta kama vile kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi,
elimu na uvumbuzi wa kidijitali.
Kijana Leo
imepata mafanikio makubwa kitaifa kwa wastani wa watazamaji zaidi ya milioni 4
kwa kila kipindi na kushinda Tuzo mbili za Umahiri katika Uandishi wa Habari
Tanzania (EJAT).
Kuanzisha na
kudumisha biashara changa ni safari ngumu. Kupitia makubaliano haya mapya, JMKF
na NEXLAW wamejipanga kuhakikisha kuwa biashara za vijana zinakuwa na uimara wa
kisheria, udhibiti na fedha tangu hatua za awali — jambo ambalo litasaidia
kuimarisha mfumo wa ujasiriamali Tanzania na kuufanya kuvutia zaidi kwa
uwekezaji.
Mbali na
malengo ya ndani ya nchi, washirika hawa wawili pia wana ndoto ya kupanua wigo
wao kikanda, wakilenga kuendeleza modeli ya Kijana Leo Accelerator kote Afrika
Mashariki, huku wakijenga mfumo mpana wa maendeleo ya vijana unaojumuisha
uwezeshaji wa kisheria.
“Nina shauku
kubwa ya kuona mustakabali ambapo vijana wavumbuzi hawatatiwa moyo tu kuanza
safari zao, bali pia kupewa vifaa sahihi vya kuvumilia na kustawi,” alisisitiza
Bi. Anyoti. “Mustakabali huo unaanza leo — kwa kutumia vifaa sahihi,
ushirikiano sahihi, na maono sahihi.”
JMKF na NEXLAW walitoa shukrani za dhati kwa washirika wote, wadau na wafuasi wanaoendelea kuunga mkono dhamira ya kuwawezesha vijana, wakieleza kuwa makubaliano haya ni zaidi ya hati tu — ni ahadi ya kulinda, kukuza na kusimama bega kwa bega na waanzilishi wapya wa Tanzania katika safari yao ya mafanikio
EmoticonEmoticon