HOTUBA
YA NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI
MHESHIMIWA DKT. DOTO MASHAKA BITEKO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO
YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA
NISHATI KWA MWAKA 2025/26
A.
UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika,
Naomba
kutoa hoja kwamba, kutokana na Taarifa iliyowasilishwa leo katika Bunge lako
Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Bunge
lako Tukufu sasa likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti
kwa Mwaka 2024/25 na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya
Nishati na Taasisi zake kwa Mwaka 2025/26.
Mheshimiwa
Spika,
Naomba
nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuendelea kuwajalia
afya njema Viongozi wetu Wakuu wa Kitaifa,
Waheshimiwa Mawaziri wenzangu, Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wengine
na hivyo kutuwezesha kuendelea kuwatumikia
Watanzania. Kipekee nimshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunijalia afya na uzima na kuniwezesha
kusimama leo mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara
ya Nishati kwa Mwaka 2025/26.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe
27 Novemba, 2024 Taifa letu lilimpoteza Mhe. Dkt. Faustine Engelbert Ndugulile
(Mb.), aliyekuwa Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika
na Mbunge wa Jimbo la Kigamboni. Aidha, tarehe 13 Aprili, 2025 Taifa lilimpoteza aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mha.
Boniface Gissima Nyamo-Hanga. Kwa masikitiko makubwa naungana na Wabunge wenzangu
kutoa pole kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, familia za marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa
ujumla kwa kuondokewa na viongozi hawa. Sisi tuliwapenda lakini Mwenyezi Mungu aliwapenda zaidi. Tunaomba
Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, Amina.
Mheshimiwa
Spika,
Mwezi
Novemba, 2024 Watanzania wenzetu walipatwa na majanga baada ya jengo la ghorofa
kuporomoka, Kariakoo Jijini Dar es Salaam. Tukio hilo lilisababisha athari
mbalimbali ikiwemo vifo, uharibifu wa mali na miundombinu. Nami naungana na
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Watanzania wote kwa ujumla, kutoa pole kwa Watanzania wenzetu walioondokewa na
ndugu, jamaa na marafiki pamoja na waliopoteza mali zao kufuatia kutokea kwa
tukio hilo.
Mheshimiwa Spika,
Kipekee napenda kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) kwa kufanikisha Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM uliofanyika Jijini
Dodoma tarehe 18 na 19 Januari, 2025. Katika Mkutano huo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipitishwa kwa kishindo
na Wajumbe kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa mgombea wa nafasi ya
Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa tiketi ya Chama cha
Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Aidha, nampongeza Komredi Balozi
Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa na kuthibitishwa
na Wajumbe kuwa mgombea mwenza wa nafasi
ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Stephen Masato Wasira
kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara.
Mheshimiwa
Spika,
Pia
nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa
Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa maelekezo na
miongozo wanayonipatia katika kutekeleza majukumu yangu ikiwemo
usimamizi wa Sekta ya Nishati. Nikiri kuwa maelekezo na miongozo ya Viongozi
wetu Wakuu hawa ni chachu na msingi wa mafanikio ya utekelezaji wa majukumu
yangu.
Mheshimiwa
Spika,
Nitumie
fursa hii pia kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa
kuliongoza Bunge letu Tukufu kwa weledi na umahiri mkubwa. Ni wazi kuwa, chini ya uongozi wenu Bunge letu limeendelea
kuwa mahiri zaidi katika kuisimamia na kuishauri Serikali kuhusu utekelezaji wa
shughuli mbalimbali ili kuboresha maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika,
Kipekee nampongeza Mhe. Dkt. David Mathayo David (Mb.),
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe
Shaban Ng’enda (Mb.), Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo pamoja na Wajumbe wote
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa ushauri na maoni yao
katika kuendeleza na kusimamia Sekta ya Nishati kwa manufaa ya kiuchumi na
kijamii kwa Taifa letu na watu wake. Napenda kuahidi kuwa Wizara ya Nishati
itaendelea kuzingitia ushauri wa Kamati wakati wa utekelezaji wa majukumu ya
Sekta ya Nishati kwa Mwaka 2025/26.
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuwapongeza Mawaziri wote walioaminiwa na kuteuliwa na Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania
kusimamia Wizara mbalimbali na ninawashukuru kwa ushirikiano mkubwa
wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati. Namshukuru pia Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga (Mb.), Naibu Waziri wa
Nishati kwa uchapakazi wake mahiri usio na kifani na ushirikiano mkubwa
anaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Aidha, namshukuru Mha. Felchesmi
Jossen Mramba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati kwa utendaji wake mahiri katika
kutekeleza majukumu ya kila siku ya Wizara. Vilevile, nawashukuru Dkt. James Peter Mataragio, Naibu Katibu Mkuu
anayeshughulikia masuala ya petroli
na Dkt. Khatibu Malimi Kazungu, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia
masuala ya umeme na nishati jadidifu kwa utumishi wao makini katika kufanikisha
kufikiwa kwa malengo ya Wizara.
Mheshimiwa Spika,
Nawashukuru pia Wakuu wa Idara na Vitengo, Wenyeviti na
Wajumbe wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara, Wakuu wa Taasisi zilizo
chini ya Wizara na Watumishi wote wa Wizara kwa ujumla kwa ushirikiano na
juhudi zao katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara.
Mheshimiwa Spika,
Napenda nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo
la Bukombe kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekeleza shughuli mbalimbali
za maendeleo ya Jimbo. Kutokana na majukumu ya kitaifa ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, kuna wakati wananikosa jimboni, lakini kwa wema na upendo
wao wanaendelea kunivumilia na kunipa ushirikiano mkubwa. Nawaahidi kuendelea
kuwa mtumishi wao mwaminifu na anayejituma katika kutekeleza shughuli za
maendeleo jimboni. Kipekee, namshukuru mke wangu mpendwa Benadetha Clement
Mathayo kwa maombi na upendo wake wa dhati kwangu na watoto wetu. Amekuwa mvumilivu katika kipindi chote ninapokuwa
natekeleza majukumu yangu ya Ubunge, Uwaziri na Unaibu Waziri Mkuu na kukubali
kubeba na kutekeleza baadhi ya majukumu ya kifamilia.
Mheshimiwa
Spika,
Natambua umuhimu wa vyombo vya
habari katika kuhabarisha na kuelimisha umma
wa Watanzania kuhusu maendeleo ya Sekta
ya Nishati. Napenda kuvishukuru na kuvipongeza vyombo hivyo vikiwemo redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii kwa
ushirikiano mkubwa waliotupatia Wizara ya
Nishati kwa Mwaka 2024/25. Ni matumaini yangu kuwa, ushirikiano huu
utazidi kuimarika katika Mwaka 2025/26 kwa manufaa ya Taifa letu na Wananchi
wake kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
Hotuba hii imeandaliwa kwa kuzingatia maudhui ya Hotuba ya Mheshimiwa Kassim
Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu
Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2024/25 na Mwelekeo wa
Kazi za Serikali kwa Mwaka 2025/26.
Mheshimiwa
Spika,
Baada ya utangulizi huo, naomba sasa kuwasilisha
Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa Mwaka 2024/25, pamoja
na Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2025/26.
B. UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA MWAKA 2024/25
Mheshimiwa Spika,
Utekelezaji wa majukumu ya Wizara
katika Mwaka 2024/25 uliongozwa na vipaumbele
mbalimbali vilivyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuendelea
kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme; kupeleka
nishati vijijini; kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya
mafuta na gesi asilia ikiwemo mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa
Kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG)
na ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga,
Tanzania (East African Crude Oil Pipeline - EACOP) na kutekeleza
shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya
kimkakati vya Songo Songo Magharibi, Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi – Wembere na
4/1B & 4/1C; pamoja na kusambaza gesi asilia viwandani, katika taasisi na
majumbani na kuimarisha matumizi ya CNG katika magari.
Mheshimiwa Spika,
Vipaumbele vingine vilivyowekwa
katika Mwaka 2024/25 ni kuendelea
kuimarisha upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia (clean cooking energy) nchini; kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa
upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli pamoja na ufanisi katika
kushughulikia upatikanaji wa bidhaa hizo; kuendelea
kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa Taasisi/Mashirika yaliyo chini ya Wizara
ambayo ni TANESCO, TPDC, EWURA, PURA, REA, PBPA pamoja na kampuni tanzu ili
yaimarishe tija, ufanisi, uwajibikaji na ubora katika uendeshaji na utoaji wa
huduma kwa wananchi; na kuendelea
kuimarisha ushiriki wa wazawa katika shughuli za mafuta na gesi asilia pamoja
na rasilimali watu ya Wizara na Taasisi zake.
Mheshimiwa Spika,
Sehemu
B ya Hotuba yangu ukurasa wa 7 hadi 124 inaelezea kwa kina kuhusu hatua
iliyofikiwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika mwaka 2024/25 na
mafanikio yaliyopatikana katika maeneo ya uzalishaji, usafirishaji na
usambazaji wa umeme; upelekaji wa umeme vijijini, kuwezesha wananchi kutumia
nishati safi ya kupikia pamoja na shughuli za utafutaji, uendelezaji,
usambazaji na matumizi ya mafuta na gesi.
Bajeti ya Matumizi ya Wizara na Mtiririko wa
Fedha kwa Mwaka 2024/25
Mheshimiwa Spika,
Katika
Mwaka 2024/25,
Wizara ya Nishati iliidhinishiwa kutumia jumla ya Shilingi Trilioni Moja,
Bilioni Mia Nane Themanini na Tatu, Milioni Mia Saba Hamsini na Tisa, Mia Nne
Hamsini na Tano Elfu (Shilingi 1,883,759,455,000) ambapo Shilingi
Trilioni Moja, Bilioni Mia Saba Tisini na Nne, Milioni Mia Nane Sitini na Sita,
Mia Nane Thelathini na Mbili Elfu (Shilingi 1,794,866,832,000)
sawa na
asilimia 95.3 ya Bajeti yote ya Wizara ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na Shilingi
Bilioni Themanini na Nane, Milioni Mia Nane Tisini na Mbili, Mia Sita Ishirini
na Tatu Elfu (Shilingi 88,892,623,000) sawa na asilimia 4.7 ni kwa ajili ya
Matumizi ya Kawaida.
Mheshimiwa Spika,
Hadi
mwishoni mwa mwezi Machi 2025, Wizara ilipokea jumla ya Shilingi Trilioni Moja, na Milioni Mia Tatu na Mbili, Mia Sita Ishirini
na Nne Elfu, na Sitini na Tisa (Shilingi
1,000,302,624,069) ambapo Shilingi Bilioni Kumi na Nane, Milioni Mia Mbili Kumi
na Nne, Mia Nane Sabini na Tatu Elfu, Mia Moja Tisini (Shilingi 18,214,873,190) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi
Bilioni Mia Tisa Themanini na Mbili, na Milioni Themanini na Saba, Mia Saba
Hamsini Elfu, Mia Nane Sabini na Tisa (Shilingi 982,087,750,879) ni
kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.
SEKTA NDOGO YA UMEME NA NISHATI JADIDIFU
Hali ya Uzalishaji wa Umeme
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na jitihada zinazotekelezwa na Serikali
katika kuimarisha uzalishaji wa umeme nchini kupitia utekelezaji wa miradi
mbalimbali, nchi yetu imeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la uzalishaji wa
umeme. Naomba kutumia fursa hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, katika
kipindi cha mwaka mmoja, uwezo wa mitambo ya kufua
umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa umeongezeka na kufikia MW 4,031.71
mwezi Aprili 2025, sawa ongezeko la asilimia 86.6 ikilinganishwa na Megawati 2,138 zilizokuwepo mwezi
Machi, 2024. Aidha, kutokana na Serikali
ya Awamu ya Sita kuendelea kuweka kipaumbele na msukumo madhubuti katika
kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha na uhakika, kumekuwepo na ongezeko
kubwa la uzalishaji wa umeme katika mfumo wa Gridi ya Taifa tangu Mwaka 2020/21.
Mheshimiwa Spika,
Wakati mwaka 2020/21 uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya
Taifa ulikuwa ni MW 1,601.84, kwa sasa mitambo iliyopo ina uwezo wa kufua
umeme wa MW 4,031.71, sawa na ongezeko la
asilimia 151.7 kama inavyoonekana katika Kielelezo
Na. 2 katika Hotuba yangu ukurasa wa 13. Aidha, hadi kufikia mwezi
Aprili, 2025, mitambo ya kuzalisha umeme ambayo haijaungwa katika Gridi ya
Taifa ina uwezo wa jumla ya MW 328.17 ambayo inajumuisha mitambo inayomilikiwa
na TANESCO yenye uwezo wa kuzalisha MW 20.19 na MW 307.98 zinazozalishwa na
kampuni binafsi kwa ajili ya matumizi ya kampuni hizo kama inavyoonekana katika
Kiambatisho Na. 2 cha Hotuba yangu, ukurasa wa 182.
Mheshimiwa Spika,
ni vyema
kutambua kuwa kutokana na jitihada hizi, nchi yetu imeweza sasa kuondokana na
mgao wa umeme ambao ulikuwa changamoto kubwa katika kipindi cha miaka mingi na
kuwa na ziada ya umeme. Aidha, kupatikana kwa umeme wa uhakika kumewezesha kupunguza
gharama za uzalishaji na kufanya biashara nchini; kuzimwa kwa mitambo ya
kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta ambayo uendeshaji wake ni wa gharama kubwa;
na kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika vijijini, katika uendeshaji wa
treni ya kisasa ya SGR na katika mikoa ambayo ilikuwa haijaungwa katika gridi
ya Taifa. Aidha, upatikanaji huu wa umeme wa uhakika umechangia kukua kwa Pato
la Taifa na kukabiliana na mfumuko wa bei kutokana na athari chanya za
upatikanaji wa umeme huo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na upatikanaji
wa huduma.
Mheshimiwa Spika,
Ongezeko hili limetokana na kukamilika kwa miradi
mbalimbali ya kuzalisha umeme katika kipindi husika, hususan mradi wa Kuzalisha
Umeme wa Maji wa Julius Nyerere ambapo hadi mwezi Aprili, 2025 mitambo yote
tisa (9) imekamilika. Aidha, Serikali pia imeendelea kuchukua hatua za
kukarabati mitambo mbalimbali ya kuzalisha umeme ambayo imechangia katika
kuimarisha uzalishaji wa umeme nchini.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na jitihada kubwa na za makusudi zinazotekelezwa na
Serikali ya Awamu ya Sita, hususan kukuza uchumi wa nchi yetu kunakoambatana na
mahitaji ya umeme, kuimarisha huduma za kijamii ambazo uendeshaji wake
unahitaji umeme; kukua kwa sekta ya usafirishaji (treni ya SGR); ongezeko la
matumizi ya nishati safi ya kupikia; na kuimarika kwa uunganishaji wa umeme kwa
wananchi mijini na vijijini, kumekuwepo na ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme
nchini.
Mheshimiwa Spika,
Mahitaji ya juu ya umeme katika Gridi ya Taifa yameongezeka
na kufikia MW 1,921.44 zilizofikiwa tarehe 09 Aprili, 2025 saa 3:00 usiku
ikilinganishwa na MW 1,590.10 zilizofikiwa tarehe 26 Machi, 2024 saa 3:00 usiku
sawa na ongezeko la asilimia 20.84. Aidha, tangu mwaka 2020 kumekuwepo na
ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme nchini la MW 740.91 kutoka MW 1,180.53 za mwaka
2020 hadi MW 1,921.44 zilizofikiwa tarehe 09 Aprili, 2025, kutokana na ukuaji
wa uchumi na kuimarika kwa utoaji wa huduma ya umeme kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine yaliyopatikana katika uzalishaji wa
umeme ni pamoja na:
a) Ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I
Extension MW 185 umefikia asilimia
98.4 ambapo
mitambo yote minne (4) kwa sasa inafua umeme wa kiasi cha MW 40 kila
mmoja, hivyo kuwezesha kiasi cha umeme wa MW 160 kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.
b) Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Rusumo (MW 80)
unaotekelezwa kwa ushirikiano wa nchi tatu (3) za Tanzania, Burundi na
Rwanda kwa mgawanyo sawa wa umeme umekamilika, na hivyo kuiwezesha Tanzania
kupata jumla ya MW 26.67 za umeme. Kukamilika kwa mradi huu kumeboresha
upatikanaji wa umeme katika mikoa ya kanda ya ziwa na kuunganishwa kwa Gridi ya
Taifa ya Tanzania na Gridi za nchi za Burundi na Rwanda na hivyo kutoa fursa ya
kuziuzia umeme nchi hizo endapo zitakuwa na mahitaji.
c)
Utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mradi wa kuzalisha umeme wa jua
Mkoani Shinyanga (MW 150) inayohusisha uzalishaji wa umeme wa MW 50 umefikia asilimia 51.
Aidha, mkataba wa ufadhili kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo
la Ufaransa (AFD) kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya MW 100
ulisainiwa tarehe 6 Desemba, 2024 na unatarajiwa kuanza utekelezaji mwezi wa
Julai, 2025 baada ya taratibu za zabuni ya kumpata mkandarasi kukamilika.
Mheshimiwa Spika,
Serikali
iliendelea pia kutekeleza miradi mingine ya kuzalisha umeme ikiwa ni pamoja na Malagarasi (MW 49.5),
Ruhudji (MW 358), Rumakali (MW 222) na Kakono
(MW 87.8) ambapo utekelezaji upo katika hatua mbalimbali. Aidha, miradi ya
kuzalisha umeme kwa kutumia jotoardhi ikiwa ni pamoja na miradi ya Ngozi (MW
70), Kiejo-Mbaka (MW 60) na Natron (MW 60) iliendelea kutekelezwa, lengo likiwa
ni kuhakikisha nchi yetu inakuwa na vyanzo mbalimbali vya uzalishaji wa umeme.
Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme
Mheshimiwa Spika,
Kuzalisha
umeme ni jambo moja lakini ili umeme huo uweze kuwafikia walaji na kutumika,
hauna budi kusafirishwa na kusambazwa. Serikali imeendelea na upanuzi wa
miundombinu ya kusafirisha umeme ambayo imefikia jumla ya urefu wa kilomita
8,140 ikiwa ni ongezeko la asilimia 5 ikilinganishwa na kilomita 7,745 za Mwaka
2023/24. Aidha, miundombinu ya
usambazaji umeme imeongezeka kutoka kilomita 176,750.9 mwezi Aprili 2024 hadi
kilomita 200,266.25 mwezi Aprili 2025 sawa na ongezeko la asilimia 13.3.
Mheshimiwa Spika,
Hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya kusafirisha umeme ni pamoja:
a) Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa
kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 160 kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha
Julius Nyerere hadi Chalinze mkoani Pwani umekamilika kwa asilimia 99.8 na
ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Chalinze umekamilika kwa asilimia
97.6. Aidha, kwa sasa mradi huu
upo katika hatua za uangalizi na miundombinu hiyo inaendelea kutumika kuingiza
umeme unaozalishwa katika bwawa la
Julius Nyerere kwenye Gridi ya Taifa.
b) Mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita
414 kutoka Singida hadi Namanga kupitia Babati na Arusha umekamilika na hivyo kuwezesha kuunganishwa kwa Gridi za Taifa za Tanzania na Kenya.
Kukamilika kwa mradi huu kuna manufaa mbalimbali kwa nchi yetu, ikiwa ni pamoja
na kuwezesha kufanyika kwa
biashara ya
umeme baina ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki kupitia East African Power Pool (EAPP).
![]() |
c) Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti
400 kutoka Iringa hadi
Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma (TAZA) umefikia asilimia 38 na unatarajiwa kukamilika Mei,
2026. Kukamilika kwa mradi huu kutaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa
ya nyanda za Juu Kusini pamoja na kuunganisha Gridi ya Taifa na Gridi za nchi
za Kusini mwa Afrika na hivyo kuwezesha kufanyika kwa biashara ya umeme baina
ya nchi hizo kupitia Southern African
Power Pool (SAPP).
d) Kukamilika
kwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka
Nyakanazi hadi Kigoma ambao umefanikisha kuunganisha Mkoa wa Kigoma katika
Gridi ya Taifa na kuwezesha kuzimwa kwa mitambo ya umeme wa mafuta. Aidha,
TANESCO itaokoa kiasi cha Shilingi bilioni 58.4 zilizokuwa zinatumika kwa mwaka
kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya dizeli.
e) Kukamilika kwa ujenzi wa njia ya kusafirisha
umeme ya msongo wa kilovoti 132 yenye urefu wa kilomita 115 kutoka Tabora hadi
Urambo na kuwezesha kuimarika kwa upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Urambo.
Aidha, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 132 yenye urefu
wa kilomita 383 kutoka Tabora hadi Katavi kupitia Sikonge, Ipole na Inyonga
umefikia asilimia 96 na unatarajiwa kukamilika katika mwaka huu wa fedha wa
2024/25.
Mheshimiwa Spika,
Serikali iliendelea kutekeleza miradi mingine ya usafirishaji na
usambazaji wa umeme kama inavyoelezewa kwa kina katika Hotuba yangu ukurasa wa
26 hadi 40, ikiwa ni pamoja na Mradi wa
Kuimarisha Gridi ya Taifa (Gridi Imara) na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo
wa kilovoti 220 kutoka Benaco
hadi Kyaka. Aidha, kutokana na jitihada za usafirishaji na usambazaji wa umeme
zinatekelezwa na Serikali, wateja waliounganishiwa umeme nchini wameongezeka kutoka 2,766,745
Mwaka 2020/21 hadi 5,449,278 mwezi Aprili, 2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia
97.
![]() |
Miradi ya Nishati Vijijini
![]() |
Mheshimiwa Spika,
Katika Mwaka
2024/25 Serikali iliendelea kutekeleza azma yake ya kuhakikisha huduma ya umeme
inafika katika vijiji vyote Tanzania Bara. Napenda kutumia nafasi hii
kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali imeweza kuvifikia vijiji vyote
12,318 vya Tanzania Bara kupitia miradi mbalimbali ya umeme inayotekelezwa
kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Aidha, kupitia utekelezaji wa miradi
ya umeme vijijini, jumla
ya taasisi na maeneo ya huduma 63,140
yameunganishiwa umeme kutoka 15,200 mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 315. Maeneo hayo ni vituo vya afya, taasisi za elimu, taasisi za biashara,
nyumba za ibada na pampu za maji kama inavyoonekana katika Kiambatisho
Na. 9 cha Hotuba yangu ukurasa wa 204.
Mheshimiwa
Spika,
Hatua hii ya
kufikisha miradi ya umeme katika vijiji vyote Tanzania Bara ina manufaa makubwa
kwa wananchi wa maeneo hayo, ikiwa ni pamoja na kutoa fursa za ajira kupitia
shughuli za uzalishaji mali kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda vidogo na
biashara; kuboresha huduma za jamii ikiwemo, afya na elimu pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama hasa
katika maeneo ya mipakani. Aidha, hatua hiyo imeimarisha huduma za mawasiliano
ya simu katika maeneo ya vijijini, huduma za kifedha pamoja na kurahisisha
upatikanaji wa habari kwa wananchi kupitia runinga, redio na mitandao ya
kijamii, na hivyo kufanya mazingira ya vijijini kuwa ya kuvutia na kupunguza
ushawishi kwa wananchi kuhamia mijini.
Mheshimiwa
Spika,
Pamoja na kukamilisha kazi ya kuunganisha
umeme vijijini, Serikali imeendelea kupeleka umeme kwenye vitongoji ambapo jumla ya vitongoji 33,657 kati ya 64,359 vya
Tanzania Bara sawa na asilimia 52 vimeunganishiwa umeme. Aidha, miradi mingine
ya nishati vijijini iliyotekelezwa ni pamoja na miradi wa ujazilizi; mradi wa kusambaza
umeme katika Vijiji-Miji; mradi wa kupeleka umeme kwenye maeneo ya migodi midogo,
viwanda na maeneo ya kilimo; na mradi wa kupeleka umeme katika minara ya mawasiliano
ya simu. Aidha, ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya nishati ya mafuta
vijijini, Serikali iliendelea kutekeleza mradi wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo
vya kusambaza bidhaa za mafuta ya petroli vijijini ambapo kiwango cha juu cha
mkopo kinachoweza kutolewa kwa kila mwendelezaji ni Shilingi 132,600,000
ambacho kinatakiwa kurejeshwa ndani ya miaka saba (7) kwa riba ya asilimia 5.
Uratibu
wa Mkutano wa Wakuu wa
Nchi za Afrika kuhusu Nishati (Africa
Heads of State Energy Summit)
Mheshimiwa Spika,
Serikali iliandaa na kushiriki Mkutano wa Wakuu
wa Nchi za Afrika wa Nishati (African Heads of States Energy Summit)
uliofanyika tarehe 27-28 Januari, 2025 Jijini Dar es salaam. Pamoja na mambo
mengine, kupitia mkutano huo Mpango wa Kitaifa wa Nishati wa Tanzania (National Energy Compact) ulizinduliwa,
ambao unalenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme nchini kufikia
asilimia 100 ifikapo mwaka 2030 kutoka cha sasa cha asilimia 78.4; kuongeza kasi ya kuunganisha umeme
nchini hadi kufikia asilimia 75 katika kipindi hicho kutoka asilimia 46 za
sasa; kuongeza kiwango cha matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia
6.9 ya mwaka 2021 hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2030; na kuongeza mchango wa
sekta binafsi katika Sekta ya Nishati kwa kiasi cha Dola za Marekani bilioni
4.39 sawa na takriban Shilingi trilioni 11.73 ifikapo mwaka 2030.
Mheshimiwa Spika,
Kupitia mkutano huo, Wakuu wa Nchi za Afrika walisaini Azimio la utekelezaji wa Mpango huo (Dar es Salaam Declaration by the African Heads of States Energy Summit),
ikiwa ni makubaliano ya pamoja ya Wakuu hao ya kuunganisha nguvu na jitihada za
pamoja za kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha zitakazowezesha upatikanaji
wa huduma ya umeme wa uhakika, endelevu na gharama nafuu kwa watu milioni 300
katika Bara la Afrika ifikapo 2030. Nitumie fursa hii kupitia Bunge lako
Tukufu, kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Nishati Afrika
(Mission 300) kwa Mwaka 2025. Aidha,
Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini yake inakamilisha
uandaaji wa Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Nishati (National Energy Compact) ambao
utekelezaji wake utaanza Mwaka 2025/26.
Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia
Mheshimiwa
Spika,
Serikali chini
ya uratibu wa Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na wadau mbalimbali,
inaendelea na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya
Kupikia (2024 - 2034) uliozinduliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 08 Mei 2024. Lengo la Mkakati huo ni
kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia
ifikapo mwaka 2034. Manufaa ya utekelezaji wa Mkakati huu ni pamoja na
kuwaepusha wananchi na athari za kiafya zitokanazo na matumizi ya nishati
zisizo safi za kupikia na kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaotokana na
matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia.
Mheshimiwa Spika,
Serikali kwa
kushirikiana na wadau imeendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa nishati safi ya kupikia
pamoja na kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika
Taasisi za Umma na binafsi zinazohudumia zaidi ya watu 100 kwa siku, ikiwemo Jeshi
la Magereza, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Shule za Sekondari. Aidha, zoezi la kusambaza mitungi 452,445
ya gesi ya kupikia (LPG) kwa bei ya punguzo la hadi asilimia 50 liliendelea, na
kupitia programu hii jumla ya mitungi 154,224 imesambazwa hadi kufikia Aprili
2025.
Mheshimiwa Spika,
Hatua nyingine
zilizochukuliwa ili kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ni
kuanza utekelezaji wa mradi wa kusambaza majiko
banifu 200,000 yaliyotengenezwa kwa teknolojia yenye ubunifu wa kupunguza
matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kuwezesha kupunguza uharibifu wa mazingira
katika maeneo ya vijijini na vijiji-miji. Hadi Aprili 2025, Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) imeshapata kampuni sita (6) za kusambaza majiko banifu 192,038
katika maeneo ya vijijini na vijiji - miji kwenye mikoa 23 kwa bei ya ruzuku ya
hadi asilimia 75. Aidha, REA ipo katika hatua za mwisho za kuwapata watoa
huduma watakaosambaza majiko hayo katika mikoa miwili (2) iliyobaki ya Njombe
na Katavi.
SEKTA
NDOGO YA MAFUTA NA GESI ASILIA
Mheshimiwa Spika katika Mwaka
2024/25 Serikali kupitia Wizara ya Nishati, iliendelea kusimamia na kuendeleza Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia katika maeneo ya
utafutaji, uendelezaji, uzalishaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa
bidhaa za mafuta na gesi, kwa lengo la kuhakikisha mchango wa Sekta hii katika
Pato la Taifa unaendelea kuimarika, ambapo utekelezaji ulikuwa kama ifuatavyo:
a) Shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia ziliendelea katika Vitalu vya Mnazi Bay Kaskazini; Eyasi Wembere; Songo Songo Magharibi; vitalu
Namba 4/1B na 4/1C; Mnazi Bay na Ruvuma (katika eneo la Ntorya) kama inavyofafanua katika Hotuba yangu
ukurasa wa 70 hadi 75 kuhusu kazi zilizotekelezwa.
b) Majadiliano baina ya Serikali na wawekezaji kuhusu utekelezaji wa
mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (Liquefied Natural Gas – LNG) yaliendelea kwa
kuzingatia maoni yaliyotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wadau
wengine katika mikataba ya awali, ambapo kwa sasa yapo katika hatua za mwisho.
c) Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania (East African Crude Oil Pipeline - EACOP) uliendelea
kutekelezwa ambapo umefikia asilimia 55. Kazi
zilizotekelezwa ni pamoja na kukamilika na kuanza kazi kwa karakana ya kuweka
mfumo wa joto kwenye mabomba (Thermal
Insulation System (TIS) Plant); kuwasili nchini kwa mabomba yenye uwezo wa
kujenga kilomita 900; kuwekwa mfumo wa kuhifadhi joto katika mabomba yenye
urefu wa kilomita 443.66; kupelekwa kwenye maeneo ya mradi kwa mabomba yenye
mfumo wa kuhifadhi joto yenye uwezo wa kujenga kilomita 364.3; kuendelea kwa
ujenzi wa matenki manne (4) katika eneo la Chongoleani ambao umefikia asilimia
74.2; na ujenzi wa jeti ya kupakilia mafuta ambao umefikia asilimia 69.1.
d)
Serikali kwa
kushirikiana na sekta binafsi iliendelea kuchukua hatua za kuimarisha
upatikanaji wa gesi asilia (CNG) nchini kwa ajili ya matumizi ya vyombo vya
moto. Aidha, ujenzi wa Kituo Mama cha CNG (CNG
Mother Station) katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umekamilika; na
ukamilishaji wa vituo vidogo viwili vya CNG (CNG
receiving and storage stations) vinavyojengwa
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Kiwanda cha Madawa cha Kairuki kilichopo
eneo la Viwanda Zegereni Kibaha, Pwani uliendelea. Vilevile, usanifu wa kina wa
Kihandisi (Detailed Engineering Design)
kwa ajili ya kuunganisha gesi asilia katika migahawa 12 katika eneo la Mlimani
City pamoja na maabara na migahawa mitatu (3) katika Chuo Kikuu Kishiriki cha
Elimu Dar es Salaam (DUCE) umekamilika.
Mheshimiwa Spika,
hadi Aprili, 2025 jumla ya vituo tisa (9) vya CNG vimekamilika na
vinatoa huduma, ikilinganishwa na vituo viwili (2) Mwaka 2020/21 na mwelekeo wa Serikali ni kuwa na angalau vituo 20 ifikapo Juni, 2026.
Aidha, Serikali imeendelea kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika utoaji wa
huduma za CNG ambapo kampuni 61 zimekwisharuhusiwa kufanya biashara ya CNG
nchini. Vilevile, Serikali kupitia TPDC inaendelea
na taratibu za ununuzi wa vituo sita (6) vya
CNG vinavyohamishika (Mobile CNG filling
stations) ambapo
vituo vitatu (3) vitakuwa katika Jiji
la Dar es Salaam, kimoja (1) Morogoro na viwili (2)
Dodoma. Hatua hii itaimarisha upatikanaji wa CNG kwa
ajili ya vyombo vya moto nchini na kuchochea matumizi ya nishati hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Kuimarika kwa matumizi ya CNG nchini katika vyombo vya moto, hususan
magari na bajaji kumekuwa na manufaa makubwa, ikiwemo kuwapa wananchi unafuu wa
gharama katika uendeshaji wa vyombo hivyo pamoja na kupunguza mahitaji ya fedha
za kigeni katika uagizaji wa mafuta.
Mheshimiwa
Spika,
Miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ya
kusafirisha na kusambaza gesi asilia iliendelea kutekelezwa ikiwa ni pamoja na usambazaji wa gesi asilia katika
Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara; ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia
kuanzia Kinyerezi - Dar es Salaam hadi Chalinze – Pwani; mradi wa bomba la
kusafirisha Gesi Asilia kutoka Tanzania hadi Uganda; na mradi wa kusafirisha
Gesi Asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa (Kenya).
e)
Serikali kupitia
Wizara ya Nishati iliratibu na kushiriki katika Kongamano la 11 la
Petroli la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la Mwaka 2025 (EAPCE’25)
lililofanyika nchini tarehe 5 – 7 Machi, 2025. Kongamano hilo lilihudhuriwa na
washiriki zaidi ya 1,000 kutoka nchi mbalimbali duniani ambapo nchi yetu
iliweza kutangaza fursa za uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mafuta na
gesi asilia ikiwemo CNG na kutangaza nia ya Serikali ya kunadi vitalu 26 vya
utafutaji wa mafuta na gesi asilia kupitia Duru ya Tano (5).
Mheshimiwa
Spika,
Mfumo
wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System - BPS) umeendelea
kutumika katika uagizaji wa bidhaa za mafuta ya petroli nchini, na hivyo
kuiwezesha nchi yetu kuendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za
mafuta. Aidha,
taarifa za kina kuhusu mwenendo wa bei za bidhaa za mafuta ya
petroli katika
soko la Dunia na soko la ndani ni kama inavyoonekana katika ukurasa wa 101 hadi
104 wa Hotuba yangu; na mwenendo wa uagizaji na upatikanaji wa bidhaa hizo nchini
ni kama inavyoonekana katika ukurasa wa 107 hadi 109 wa Hotuba hiyo.
USIMAMIZI NA
UDHIBITI WA SEKTA YA NISHATI KUPITIA PURA NA EWURA
Mheshimiwa
Spika,
Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Mamlaka ya Udhibiti
wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) iliendelea kutekeleza kazi
mbalimbali za usimamizi na udhibiti wa Sekta ya Nishati kama ifuatavyo:
a)
Serikali kupitia PURA iliendelea na
maandalizi ya Duru ya Tano (5) ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi
asilia ambapo maandalizi ya nyaraka muhimu zitakazotumika katika kunadi vitalu
ikiwemo Mkataba Kifani wa Ugawanaji wa Mapato (MPSA, 2025) yaliendelea. Aidha,
PURA ilikamilisha uwekaji wa mipaka katika vitalu 26 vilivyopendekezwa kuingia
kwenye mnada, kuandaa vifurushi vya data (data package) na taarifa za
kitaalamu kwa vitalu hivyo na kukamilisha nyaraka za zabuni zitakazotumika
wakati wa kunadi vitalu husika.
b)
PURA, iliendelea
na udhibiti wa shughuli mbalimbali za mkondo wa juu wa petroli ikiwa ni pamoja
na kusimamia shughuli za uzalishaji wa gesi asilia katika vitalu vya Songo
Songo na Mnazi Bay; na kukamilisha maandalizi ya rasimu ya Kanuni za
Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii katika Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi (The
Petroleum (Corporate Social Responsibility) Regulations) ambayo ipo katika
hatua za mwisho za uidhinishwaji. Kanuni hizo pamoja na mambo mengine, zitawezesha
utekelezaji wa CSR wenye tija katika maeneo ya mkondo wa juu wa petroli nchini.
c) EWURA iliendelea kusimamia shughuli za udhibiti katika Mkondo wa Kati na
Chini wa gesi asilia ambapo ilitoa vibali 10 vya ujenzi wa vituo vya CNG katika
Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro; kutoa leseni tano (5) za uendeshaji wa vituo vya CNG; vibali nane (8) kwa
ajili ya ujenzi wa mabomba ya kupeleka gesi asilia kwenye vituo vya CNG na vibali
sita (6) vya ujenzi wa mabomba ya kupeleka gesi asilia kwenye viwanda, taasisi,
migahawa ya chakula na majumbani.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na
ongezeko la ujenzi wa vituo vya CNG, unafuu wa gharama unaopatikana katika
matumizi ya CNG kama nishati mbadala ya mafuta katika vyombo vya moto, na
mwamko mkubwa wa wananchi katika kutumia nishati hiyo, nitumie fursa hii kutoa
wito kwa taasisi zote zinazohusika katika mnyororo wa matumizi ya CNG ikiwemo Bodi
ya Usajili wa Wakandarasi (CRB); Shirika la Viwango Tanzania (TBS); Baraza la
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na EWURA kuhakikisha wanasimamia ipasavyo
majukumu yao katika suala zima la matumizi CNG nchini, ikiwa ni pamoja na
usimamizi wa wamiliki wa karakana zinazohusika na ubadilishaji wa mifumo ya
magari ili kutumia CNG, kusimamia kwa karibu wakaguzi wa ufungaji wa mfumo wa
CNG kwenye magari (CNG inspectors),
kuharakisha utoaji wa vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA certificates) kwa wawekezaji wa
vituo vipya vya CNG na kuhakikisha karakana zote na wakaguzi wa mfumo wa CNG
wanawasilisha kwa mujibu wa sheria, taarifa za vyombo vya moto walivyovibadili
katika Mfumo wa Taifa wa Taarifa za Mafuta na Gesi Asilia (National Petroleum and Gas Information System).
Mheshimiwa
Spika,
EWURA pia ilitoa
leseni 580 za biashara ya mafuta, vibali 215 vya ujenzi wa miundombinu ya
mafuta na kusimamia ubora wa bidhaa za mafuta ambapo jumla ya sampuli 334
kutoka katika vituo vya mafuta na maghala zilipimwa ubora na sampuli 321 sawa
na asilimia 96.1 zilikidhi viwango stahiki vya ubora. Vilevile, EWURA ilikagua ubora wa miundombinu 569 ya
mafuta ambapo miundombinu 451 sawa na
asilimia 76.2 ilikidhi viwango vya ubora ikiwemo vigezo vya masuala ya afya,
usalama na mazingira. Pia mamlaka hiyo, ilifanya maboresho ya Kanuni nne (4)
ili kuimarisha shughuli za kiudhibiti na kuboresha utoaji wa huduma pamoja
na kutoa leseni 1,378 kwa mafundi umeme,
lengo likiwa ni kuwezesha upatikanaji wa mafundi umeme wenye ujuzi wa uwekaji
wa mifumo bora ya umeme na salama kwa wananchi, hususan maeneo ya vijijini.
CHANGAMOTO ZILIZOPO
NA UTATUZI WAKE
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Nishati
kama yanavyofafanuliwa kwa kina katika sehemu ya B.2.13 ya Hotuba yangu ukurasa
wa 117 hadi 124, ni vyema kutambua kuwa, miradi ya utafutaji, uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji wa umeme na gesi asilia inahitaji uwekezaji mkubwa katika
utekelezaji wake. Hivyo, pamoja na juhudi kubwa za kutenga rasilimali fedha
zitakazoendelea kutekelezwa na Serikali katika uendelezaji wa Sekta ya Nishati,
Serikali pia itaendelea kuhamasisha, kuvutia na kushirikiana na wadau
mbalimbali wa maendeleo ikiweno sekta binafsi ili kufanikisha upatikanaji wa
rasilimali fedha zitakazochangia katika uendelezaji wa Sekta hii kwa kuzingatia
mchango wake katika ukuaji wa uchumi, utoaji wa huduma na ajira.
C.
MPANGO NA BAJETI KWA
MWAKA 2025/26
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa
taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Wizara kwa Mwaka 2024/25, sasa napenda
kuwasilisha Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2025/26.
Mheshimiwa Spika,
Katika Mwaka 2025/26 Wizara itaendelea kuimarisha uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji wa umeme, ikiwa ni pamoja
na kufikisha Gridi ya Taifa katika mikoa iliyosalia ya Rukwa, Kagera, Lindi na
Mtwara. Aidha, Wizara itaanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Nishati wa Mwaka
2025
- 2030 (National
Energy Compact 2025 - 2030) kuhusu upatikanaji na
uunganishaji wa umeme kwa wananchi, kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika
uzalishaji wa umeme na ushiriki wa Sekta Binafsi katika maendeleo ya Sekta ya
Nishati. Vilevile, Wizara itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maendeleo ya
kiuchumi na kijamii kwa kutekeleza Mradi wa Kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid
Stabilization Project) pamoja na kufanya
matengenezo na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme.
Mheshimiwa Spika,
Maeneo
mengine ya kipaumbele katika Mwaka 2025/26 ni kuendelea na usambazaji wa nishati katika vitongoji,
maeneo ya migodi, kilimo, viwanda na pampu za maji pamoja na vituo vya afya ili
kuwezesha shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi; pamoja
na kuhamasisha na kuwezesha watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni
utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia
(2024-2034) na Mpango wa Taifa wa Nishati wa Mwaka 2025 - 2030. Wizara pia itaendelea kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za mafuta vijijini
kupitia ujenzi wa vituo vya mafuta katika maeneo hayo; pamoja na kutekeleza shughuli za utafutaji, uendelezaji na usambazaji wa mafuta na gesi asilia na kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya mafuta na gesi asilia ikiwemo
Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi – Wembere, mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi
Asilia kuwa Kimiminika (Liquefied Natural
Gas – LNG Project) na ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka
Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania (East African Crude Oil Pipeline - EACOP).
Mheshimiwa Spika,
Jitihada zitaelekezwa pia katika kusimamia na kuhakikisha
nchi yetu inakuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli
pamoja kuimarisha matumizi ya gesi asilia (CNG) katika vyombo vya moto.
Vilevile, Wizara itaendelea kutekeleza shughuli za kiudhibiti; kuimarisha
ushiriki wa wazawa katika Sekta ya Nishati pamoja na kuimarisha nguvu kazi na kuwezesha
upatikanaji wa vitendea kazi ili kuimarisha tija na ufanisi katika utendaji
kazi. Pia, Wizara itaendelea kuimarisha utendaji wa Taasisi/Mashirika yaliyo
chini yake ya TANESCO, REA, TPDC, PBPA, EWURA na PURA pamoja na Kampuni Tanzu
ili yaweze kuimarika zaidi katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi pamoja na
tija na ufanisi katika utendaji.
Mheshimiwa Spika,
Mpango na Bajeti ya Wizara kwa Mwaka 2025/26 pamoja na mambo
mengine, umezingatia Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, Dira ya Taifa
ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka
Mitano (2021/22 – 2025/26), maagizo na maelekezo
mbalimbali ya Viongozi wa Kitaifa yaliyohusu Sekta ya Nishati, Maoni na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na
Kamati nyingine za Bunge yaliyotolewa kwa nyakati tofauti, Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango Wake wa Utekelezaji,
Mkakati
wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024 - 2034), Mpango Mkakati wa Wizara ya Nishati wa Mwaka 2021/22-2025/26 na Mpango Mahususi wa Taifa wa Nishati
wa Mwaka 2025
- 2030 (National Energy Compact 2025 - 2030). Miongozo mingine iliyozingatiwa
ni Sera, Mikakati na Programu mbalimbali za Kisekta na Kitaifa pamoja na
Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) ya mwaka 2030 kuhusu
masuala ya nishati.
Mheshimiwa Spika,
Sehemu C ya Hotuba yangu ukurasa wa 125 hadi 175 inatoa ufafanuzi na maelezo ya kina kuhusu mikakati,
programu, miradi na kazi zitakazotekelezwa katika mwaka 2025/26. Kwa ufupi
Wizara itatekeleza yafuatayo:
SEKTA NDOGO YA UMEME NA NISHATI JADIDIFU
Uzalishaji wa Umeme
Mheshimiwa
Spika,
Serikali itaendelea kuelekeza nguvu katika uzalishaji wa
umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa
na umeme wa kutosha; na ziada kutumika kuuzwa nje ya nchi na kulipatia Taifa
fedha za kigeni na hivyo kunufaika ipasavyo na rasilimali za asili ambazo nchi
imebarikiwa.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali itaendelea kusimamia na
kuratibu utekelezaji wa Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius
Nyerere-MW 2,115) kwa kuhakikisha kunakuwepo na utunzaji wa vyanzo vya maji katika Bonde la Rufiji ili kuwezesha
upatikanaji endelevu wa maji kwa ajili ya mradi huu; uendeshaji na ufanisi wa
mitambo; kukamilisha ujenzi wa ghala la kuhifadhia vifaa katika kituo cha
kupoza umeme cha Chalinze; na kulipa malipo ya “retention” kwa Wakandarasi na Washauri Elekezi wa mradi wa
kuzalisha umeme JNHPP pamoja na njia ya kusafirisha umeme kutoka JNHPP hadi
Chalinze na kituo cha kupoza umeme cha Chalinze.
Mheshimiwa
Spika,
Miradi mingine ya kuzalisha umeme
itakayotekelezwa katika mwaka 2025/26 ni Malagarasi (MW 49.5); Kakono (MW
87.8); Ruhudji (MW 358); Rumakali (MW 222) na Mradi wa Kuzalisha Umeme Jua Shinyanga – MW 150.
Usafirishaji
na Usambazaji wa Umeme
Mheshimiwa Spika,
Katika kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana katika maeneo yote
nchini, Serikali itaendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya usafirishaji na
usambazaji umeme kwa kutekeleza miradi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ujenzi
wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze – Dodoma; ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze –
Kinyerezi – Mkuranga; ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme
wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Rufiji – Mkuranga; na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti
400 kutoka Dar es Salaam – Tanga –
Arusha.
Miradi mingine itakayotekelezwa ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma
(TAZA); na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo
wa kilovoti 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma. Serikali pia itaendelea na
utekelezaji wa Mradi wa Kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization Project) – Gridi Imara pamoja na
kuendelea kufanya matengenezo kinga katika vituo vya kuzalisha
umeme, miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme pamoja na vituo vya
kupoza umeme.
Miradi ya Nishati Vijijini
Mheshimiwa
Spika,
Serikali kupitia REA itaendelea kutekeleza programu na
miradi mbalimbali ya nishati vijijini ili kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya
kijamii katika maeneo hayo. Programu na miradi itakayotekelezwa ni pamoja na miradi wa kupeleka
umeme katika Vitongoji; mradi wa ujazili
Awamu ya Pili B; mradi wa ufungaji wa mifumo ya umeme jua katika maeneo ya Visiwani
na Yaliyo Mbali na Gridi ya Taifa pamoja na kutekeleza Mkakati
wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa kushirikiana na wadau.
SEKTA NDOGO YA
MAFUTA NA GESI
Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka 2025/26, Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuendeleza na
kusimamia Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi, kwa lengo la kuhakikisha mchango wa
Sekta hiyo katika Pato la Taifa unaendelea kuimarika. Serikali itaendelea
kutekeleza miradi ya utafutaji na uendelezaji wa mafuta na
gesi asilia katika vitalu vya Mnazi Bay Kaskazini; Eyasi –
Wembere; Songo Songo Magharibi; Ruvuma (Eneo la Ntorya)
na kitalu cha Lindi-Mtwara.
Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea
pia na utekelezaji wa mradi
wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia kuwa kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG); mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta
Ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania (EACOP);
ujenzi wa vituo vya CNG; na
miradi ya usambazaji wa gesi asilia katika mikoa mbalimbali nchini pamoja na
nchi jirani.
Mheshimiwa Spika,
Serikali itaendelea
kuhakikisha pia nchi yetu inaendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa
za mafuta ya petroli pamoja kutekeleza masuala ya kiudhibiti katika Sekta ya
Nishati ili kuimarisha tija na ufanisi, pamoja na utoaji wa huduma bora kwa
wananchi.
D. USHIRIKIANO WA
KIKANDA NA KIMATAIFA KATIKA SEKTA YA NISHATI
Mheshimiwa Spika,
Serikali
kupitia Wizara ya Nishati inaendelea kushirikiana na washirika mbalimbali wa maendeleo, Jumuiya za Kikanda,
nchi wahisani na wadau wengine katika utekelezaji wa miradi ya nishati. Kwa
niaba ya Serikali, napenda kuwashukuru Washirika wa Maendeleo, Jumuiya na nchi
wahisani ambao wameendelea kushiriki katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu
ya Wizara na maendeleo ya Sekta ya Nishati kwa ujumla. Napenda kutambua mchango
wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB); Benki ya Dunia (WB); Arab Bank for
Economic Development in Afrika (BADEA); Economic Development Cooperation Fund
(EDCF - Korea); Geothermal Risk Mitigation Facility (GRMF) pamoja na Taasisi na
Mashirika ya JICA (Japan), KfW (Germany), AFD (Ufaransa); Shirika la Fedha
Duniani (IMF); Sida (Sweden), NORAD (Norway); Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la
Mitaji ya Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCDF), Shirika la Maendeleo la Umoja
wa Mataifa (UNDP), Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO),
Shirika la Maendeleo la Canada (CIDA); Saudi Fund for Development (SFD); OPEC
Fund for International Development; na Abu - Dhabi Fund for Development (ADFD).
Mheshimiwa Spika,
Nitumie
nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa Serikali za Afrika Kusini, Algeria,
Angola, Burundi, Canada, China, Ethiopia,
Falme za Kiarabu, Japan, India, Indonesia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo, Kenya, Korea Kusini,
Malawi, Misri, Morocco, Msumbiji, Namibia, Norway, Oman, Rwanda, Saudi Arabia, Sweden, Ufaransa, Uganda, Ujerumani, Urusi, Zambia
na nchi nyingine kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza Sekta
ya Nishati. Aidha, nazishukuru Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Afrika (AU) kwa ushirikiano
katika masuala ya kikanda yanayohusu Sekta ya Nishati.
E. HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Kwa kuzingatia umuhimu wa Sekta ya Nishati kiuchumi na kijamii na
mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Sekta nyingine mijini na vijijini,
katika mwaka 2025/26 Wizara itaendelea kutekeleza mikakati, programu na miradi mbalimbali inayolenga kuhakikisha
nchi yetu inaendelea kuwa na nishati ya uhakika, nafuu
na endelevu. Aidha, mwelekeo wa Serikali ni kuhakikisha shughuli za mafuta na
gesi asilia zinakuwa na kushamiri zaidi na mchango wake katika Pato la Taifa
unaendelea kuimarika. Katika kufikia azma hiyo, Wizara itaendelea kushirikiana
na Wadau mbalimbali katika uendelezaji wa Sekta hii muhimu na pia kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa programu
na miradi ya nishati inayotekelezwa ili malengo na manufaa yaliyokusudiwa
yaweze kupatikana kwa wakati na viwango stahiki.
Mheshimiwa
Spika,
Naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa liidhinishe Bajeti ya jumla ya Shilingi
Trilioni Mbili, Bilioni Mia Mbili Arobaini na Sita, Milioni Mia Saba Arobaini
na Tano, Mia Nne Arobaini na Tano Elfu (Shilingi 2,246,745,445,000)
kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake. Mchanganuo wa fedha
hizo ni kama ifuatavyo:
(i)
Shilingi Trilioni Mbili, Bilioni Mia Moja Sitini na Saba, Milioni Mia
Tano Kumi na Tatu, Mia Mbili Kumi na Tisa Elfu (Shilingi 2,167,513,219,000) sawa na asilimia 96.5 ya Bajeti yote
ya Wizara ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo, Shilingi
Trilioni Moja, Bilioni Mia Nne Sitini na Sita na Milioni Ishirini, Mia Mbili
Sabini na Nne Elfu (Shilingi 1,466,020,274,000) ni fedha za ndani na Shilingi
Bilioni Mia Saba na Moja, Milioni Mia Nne Tisini na Mbili, Mia Tisa Arobaini na
Tano Elfu (Shilingi 701,492,945,000) ni fedha za nje; na
(ii) Shilingi Bilioni Sabini na Tisa, Milioni Mia
Mbili Thelathini na Mbili, Mia Mbili Ishirini na Sita Elfu (Shilingi
79,232,226,000) sawa
na asilimia 3.5 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Kati ya fedha hizo Shilingi
Bilioni Sitini na Tisa, Milioni Mia Tisa Thelathini na Mbili, Mia Tatu na Sita
Elfu (Shilingi 69,932,306,000) ni
kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC) na Shilingi Bilioni Tisa, Milioni Mia
Mbili Tisini na Tisa, Mia Tisa Ishirini Elfu (Shilingi 9,299,920,000) ni
kwa ajili ya Mishahara (PE) ya Watumishi wa Wizara na Taasisi ya PURA.
Mheshimiwa Spika,
Kwa unyenyekevu mkubwa sana naomba tena
nitoe shukrani zangu za dhati kwako na kwa Waheshimiwa Wabunge wote
kwa kunisikiliza. Hotuba hii pia inapatikana katika
Tovuti ya Wizara kwa anuani ya www.nishati.go.tz.
Vilevile, Hotuba hii ina vielelezo
mbalimbali ambavyo vimeambatishwa kwa ajili ya ufafanuzi wa masuala muhimu
yanayohusu Sekta ya Nishati.
Mheshimiwa
Spika,
Naomba kutoa hoja.
EmoticonEmoticon