MWANASHERIA CHIPAMBA: KUJENGA JENGO BILA MIUNDOMBINU YA WALEMAVU FAINI NI MILIONI 20

April 30, 2025

 

Mwanasheria Baraka Chipamba wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT),  akizungumza na watu wenye ulemavu kutoka Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB), Mkoa wa Dar es Salaam alipokuwa  akitoa elimu kuhusu sheria ya watu wenye ulemavu Aprili 29, 2025.

.............................

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MWANASHERIA Baraka Chipamba wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT)  amesema ni kosa kisheria kujenga jengo ambalo halina miundombinu ya kuwasaidia watu wenye ulemavu na faini yake ni Sh. Milioni 20.

Chipamba aliyasema hayo Aprili 29, 2025 wakati akizungumza na watu wenye ulemavu kutoka Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB), Mkoa wa Dar es Salaam alipokuwa  akitoa elimu kuhusu sheria ya watu wenye ulemavu mafunzo yaliyoratibiwa na LRCT na kufanyika ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

 Alisema kosa hilo la kujenga jengo bila ya kuwa na miundombinu ya watu wenye ulemavu likifanywa na Serikali faini yake ni Sh. Milioni 2 na isizidi Milioni 20 na kama litafanywa na mtu binafsi ni faini isiyopungua Sh. 500,000 hadi Sh.Milioni 7 au kifungo cha mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya watu wenye ulemavu kama  wananchi wengine wanayo haki ya kuheshimiwa, kutobaguliwa, kupata ajira, matunzo na stahiki zote wanazozipata watu wengine ikiwemo elimu. 

“ Upo umuhimu wa kuwepo vyama vya watu wenye ulemavu ili kuwakilisha na kujisemea katika ngazi mbalimbali, kufanya utambuzi wa mahitaji yao pia kutathmini huduma zinazotolewa na kuchochea maendeleo yao,” alisema Chipamba.

Alisema Serikali ya Tanzania imeridhia au kuonesha nia ya kuwa sehemu ya juhudi za kimataifa ya kuwainua na kuwalinda watu wenye ulemavu kwa kuwapatia fursa mbalimbali.

“Tunatambua Tanzania imeridhia na kusaini Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD-2006 na Mkataba wa Nyongeza wa Haki za Watu Wenye Ulemavu 2009). Lakini pia tunatambua kuwa kuna mambo mengi yamekwisha tekelezwa na Serikali,” alisema Chipamba.

Mwanasheria wa Tume hiyo, Vicky Mbunde ambaye alitoa elimu ya jinsi ya kuandika wosia na kufungua shauri la mirathi alisema Watu wenye ulemavu wanayo haki na nafasi ya kujiendeleza na kupata huduma katika jamii sawa na watu wasio na ulemavu.

Alisema ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maisha ya kila siku katika jamii hauna budi kulenga katika kupunguza au kuondoa maisha ya utegemezi hivyo aliwahimiza kufanya kazi kwa bidi kama vile ujasiriamali na shughuli zingine ili kujiletea maendeleo yao badala ya kusubiri kusaidiwa.

Katika mafunzo hayo mambo kadhaa yaliibuka ikiwa ni pamoja na jinsi wanavyoitwa ni ‘Watu wenye Ulemavu au Walemavu’ ambao wanasheria wa Tume hiyo walieleza kuwa wanatambulika kama ni Watu Wenye Ulemavu na siyo Walemavu.

Akichangia mada kuhusu suala la kuandika wosia na mgawanyo wa mali zilizoachwa na marehemu kwa wanufaika baada ya kufungua mirathi, Azamu Mohamed kutoka Yombo Dovya alisema dini ya Kiislam haimtambui mtoto aliyezaliwa kwa mama mwingine nje ya ndoa jambo ambalo linawafanya wanaume wengi kuwakataa watoto hao hivyo kushindwa kupata mgao wa mali za baba zao pindi wanapofariki.

“Wanaume ule ujasiri mliotumia wa kutoka kwa wake zenu na kwenda kuchepuka na kuwapata watoto hao mnatakiwa kuuonesha kwa kuwatambulisha kwa wake zenu na ndugu ili nao wajulikane na kupata mgao huo badala ya kuwakana,” alisema.

Mweka hazina wa Jumuiya hiyo, Seif Jega, akizungumza baada ya kupata nafasi ya kushukuru kwa niaba ya washiriki baada ya mafunzo hayo aliupongeza uongozi wa Tume hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo kwa watu wenye ulemavu na kuomba yawe endelevu ikiwa ni pamoja na kuyafikisha vijijini wenzao na jamii waweze kuielewa jambo ambalo litaweza kupunguza unyanyapaa kwa kundi hilo.

Kuhusu Tume hiyo, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) ni Idara ya Serikali inayojitegemea chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Sura ya 171, na ilianza kazi rasmi tarehe 21 Oktoba, 1983. 

Kwa mujibu wa sheria, Tume ina jukumu la kufanya mapitio ya sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ziandane na mazingira ya wakati uliopo kwa maendeleo endelevu.          

Mwanasheria Vicky Mbunde wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT), akitoa elimu kuhusu namna ya kuandika Wosia pamoja na kufungua mirathi.
Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Iddi Damka, akiongoza mafunzo hayo.
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Judika Magezi akizungumza.
Mafunzo yakiendelea.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Maswali yakiulizwa kutoka kwa washiriki wa mafunzo hao.
Asha Kinyama akichangia jambo kwenye mafunzo hayo
Maswali yakiendelea kuulizwa.
Margareth Mhina, akizungumzia umuhimu wa faragha wakati wa kumuhudumia mtu mwenye ulemavu anapokwenda kupata matibabu hospitalini.
Maswali zaidi yakiulizwa.
Taswira ya mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea. 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »

EmoticonEmoticon

:)
:(
=(
^_^
:D
=D
=)D
|o|
@@,
;)
:-bd
:-d
:p
:ng