Na Dotto
Mwaibale, Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema jiji hilo limejipanga kuchukua
tahadhari zote zitakazotokana na hadhari za mvua za masika ambazo zinaendelea
kunyesha.
Chalamila
aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
Aprili 18, 2025 wakati akitoa taarifa kwa wananchi kuhusu kuchukua tahadhari
katika kipindi hiki cha msimu wa mvua za masika zilizoanza kunyesha mwezi Machi hadi mwezi Mei
2025 na mikakati iliyopo ya kukabiliana na hadhari hizo.
Mkuu huyo wa
mkoa alisema hatua ya kwanza iliochukuliwa ni kufanya malipo ya fidia mbalimbali kwa
watu wote waishio mabondeni na kuanza kwa utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya
juu kuanzia eneo la Fire hadi Magomeni na kulipa fidia kwa wakazi wa bonde la
Mto Msimbazi kwa ajili a mradi wa kuendeleza bonde hilo ili kukabiliana na
mafuriko sanjari na kuboresha matumizi ya ardhi katika eneo hilo.
Aidha,
Chalamila alitoa maelekezo kwa idara za ujenzi na uokoaji kuhakikisha
wanajipanga kwenye kuimarisha miundombinu korofi na kuwa tayari kwa kuzuia na
kufanya uokozi wa haraka pale majanga yatakapojitokeza.
“Mpaka sasa kwa mradi wa kuendeleza bonde la Mto Msimbazi gharama za mradi huo ni takribani Dola za Marekani Milioni 260 ambapo Benki ya Dunia imetoa mkopo wa Dola za Marekani Milioni 200, Serikali ya Hispania imetoa mkopo wa Dola za Marekani Milioni 30 na Serikali ya Uholanzi imetoa ruzuku ya Euro Milioni 30,” alisema Chalamila na kueleza kuwa miradi hiyo itaanza kutekelezwa wakati wowote kuanzia sasa.
Kutokana
na tahadhari hiyo amezitaka taasisi za Serikali mkoani hapa kuwa tayari
kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zitaletwa na mvua hizo.
“Mkoa wetu
umejipanga vizuri kukabiliana na changamoto hizo iwapo zitajitokeza,". alisema Chalamila.
Wakati huo
huo akizungumzia kuhusu hali ya usalama kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi oktoba mwaka huu, Chalamila amewaondoa hofu na kuwahakikishia usalama wafanyabiashara katika jiji hilo wa
kutoka nje na ndani ya nchi.
Aidha, amepongeza mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana
baada ya maboresho makubwa ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) chini ya Kampuni ya DP
Word ya Dubai.
Alisema wanasiasa wengi wanakiri Serikali imefanya kazi
kubwa ya ujenzi wa miradi mbalimbali kupitia makusanyo ya ndani ambapo
aliwahimiza wananchi kuendelea kulipa kodi ili miradi mingine ya kimkakati
ifanyiwe kazi ipasavyo.
"Kwa sasa tupo katika kipindi cha kuelekea kwenye
Uchaguzi Mkuu, hivyo inawezekana baadhi ya wafanyabiashara wakawa na hofu,
ninachoweza kuwaambia wasiwe na hofu kwani sisi kama mkoa tumejipanga
kuhakikisha utulivu na amani inaendelea wakati wa uchaguzi na baada uchaguzi,”
alisema Chalamila.
Katika tukio
jingine kwenye mkutano huo, Chalamila amewaomba wadau mbalimbali kujitoa
kuwasaidia Wasanii wafupi wakiongozwa na Tausi Degela, Pimbi na Hamisi, ili kuwapatia gari jipya wasanii hao kwa ajili ya
shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya miradi
mbalimbali inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumuombea
kura wakati kampeni za uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi okoba mwaka huu.
“Watu wenye ulemavu, wakiwemo wasanii wafupi, ni sehemu muhimu ya jamii na wanayo nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa letu na kutoa elimu sahihi kuhusu mafanikio ya Serikali,” alisema Chalamila.
Msanii
Tausi Mdegela aliwataka watu wenye ulemavu kuachana na dhana ya utegemezi na
kuanza kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali, akisisitiza kuwa ulemavu
si kikwazo cha mafanikio.
“Tumewezeshwa
kupitia mikopo na fursa nyingine. Tunapaswa kujiamini na kushiriki kikamilifu
katika kuinua uchumi wetu binafsi na wa jamii,” alisema Tausi.
Naye,
msanii Pimbi akizungumza baada ya kupatiwa nafasi na mkuu wa mkoa alitumia
nafasi hio kuhamasisha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika mchakato
wa uchaguzi mkuu huku akisisitiza kuwa ushiriki wao ni wa muhimu katika maamuzi
ya kitaifa.
“Ni wakati wetu wa kusimama na kuonekana. Tuna haki sawa kama Watanzania wengine, na tunapaswa kutumia sauti yetu ipasavyo,” alisema Pimbi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akiwa na Wananii wa kundi la Wajuu wa Mama.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akisisitiza jambo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.
EmoticonEmoticon