Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,
Bw. Ladislaus Mwamanga akiwatambulisha watumishi wa Mfuko wa Maendeleo
ya Jamii (TASAF) kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala
Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) alipoitembelea ofisi hiyo mapema leo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) akisisitiza
uwajibikaji kwa watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
alipoitembelea ofisi hiyo mapema leo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) akisisitiza
uwajibikaji kwa watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)
alipoitembelea ofisi hiyo mapema leo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) akizungumza na
watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) alipoitembelea ofisi
hiyo mapema leo. Wengine ni waandishi wa habari walioudhuria tukio
hilo.
………………………………………………………………………………………….
Waziri Nchi Ofisi ya Rais
,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki
(Mb) ameuagiza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuendelea
kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kusaidia jitihada za serikali
za kuwaondolea wananchi kero ya umaskini.
Mhe. Kairuki amesema TASAF inayo
dhima kubwa ya kuhakikisha kuwa huduma inazozitoa kwa wananchi
zinakwenda sambamba na misingi ya uadilifu na utawala bora ili hadhi ya
mfuko huo iendelee kuwa kubwa.
Waziri Kairuki ameyasema hayo
alipotembelea Makao Makuu ya TASAF jijini Dar es salaam ambako
alizungumza na watumishi wa mfuko huo ikiwa ni mwendelezo wa ziara za
kikazi katika taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala
Bora ambayo amepewa dhamana ya kuisimamia baada ya kuteuliwa kushika
wadhifa huo na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
P. Magufuli.
“Ninawasisitiza muhakikishe kuwa,
walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wananufaika vilivyo na
fedha zinazotolewa ili hatimaye waweze kuondokana na umaskini” alisema
Kairuki.
Aidha, Mhe. Kairuki ameuagiza
uongozi wa TASAF kuweka utaratibu utakaowezesha ukaguzi wa mara kwa mara
wa walengwa wa Mpango huo nchini kote ili kuhakikisha kuwa watu
wasiostahili wanaondolewa kwenye utaratibu wa ruzuku na kupunguza
malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
Mhe. Kairuki ameonya vikali dhidi
ya uwezekano wa kuweko matumizi mabaya ya fedha kwa kutoa ruzuku kwa
watu wenye uwezo jambo ambalo amesema halipaswi kufumbiwa macho na pale
itakapobainika wahusika wachukuliwe hatua za kuwaondoa kwenye Mpango na
kisha kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Katika hatua nyingine, Waziri
Kairuki ameuagiza uongozi wa TASAF kutoa mapendekezo ndani ya siku 30 ya
namna ya kukabiliana na malalamiko yanayoelekezwa kwa watendaji wa
ngazi za vijiji,kata,na hata wilaya ambao wamekiuka taratibu za
kuwabaini na kuwaorodhesha walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini
ili hatua zichukuliwe haraka iwezekanavyo.
Awali akitoa maelezo kwa Waziri,
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga amesema Mfuko
umefanikiwa kuandikisha zaidi ya walengwa Milioni 1.1 ambao wanaendelea
kupata ruzuku na kuwa hadi kufikia mwezi Januari 2016 zaidi ya
shilingi Bilioni 204 zimetolewa kwa walengwa ambapo matokeo chanya
yameanza kuonekana hususani katika Nyanja za elimu, afya na makazi.
Bwana Mwamanga amesema licha ya
changamoto zilizopo hususani katika upatikanaye wa fedha za kukidhi
idadi kubwa ya walengwa ,Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF )umeendelea
kufanya juhudi za kutafuta fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo na
kuiomba serikali kuona namna inavyoweza kuunga jitihada hizo ili
hatimaye vita dhidi ya umaskini iweze kufanikiwa .
Kuhusu Mpango wa kunusuru kaya
maskini, Bw. Mwamanga amesema walengwa wa Mpango huu wamehamasika kwa
kiwango kikubwa huku wengi wao wakionyesha uwezo katika kufuata masharti
na taratibu za Mpango hivyo suala la upatikanaji wa fedha kwa uhakika
lina umuhimu mkubwa ili kutowavunja moyo walengwa hao.