📌Lengo ni kuhakikisha kila mwananchi ananufaika
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaanza kutekeleza mradi wa kutandaza nyaya za umeme (wiring) kwa wananchi kupitia miradi ya kusambaza umeme inayotekelezwa na wakala kote nchini.
Hayo yameelezwa Jijini Dodoma Novemba 25, 2025 wakati wa kikao cha Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba na Menejimenti ya REA kilicholenga kujadili utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na REA.
Mhe. Salome amesema Serikali kupitia REA inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme katika vitongoji 9,000 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wananchi.
“Serikali inatekeleza mipango madhubuti itakayoleta matokeo ya haraka kwa wananchi wake kupitia Sekta ya Nishati. Ndani ya siku mia moja kupitia REA tunatekeleza ahadi ya Mhe. Rais ya kufikisha umeme kwa wananchi,” amesema Mhe. Salome.
Akizungumzia eneo la Nishati Safi ya Kupikia, Mhe. Salome amesema REA itajenga mifumo ya Nishati Safi ya Kupikia kwa zaidi ya taasisi 50 ili kuziwezesha kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati isiyo safi na salama.
“Ndani ya siku mia moja wananchi watashuhudia mabadiliko kwani tunakwenda kufunga mifumo ya Nishati safi ya Kupikia kwenye taasisi na tayari matangazo yametolewa, taasisi ziendelee kuchangamkia,” alisema.
Ametoa wito kwa wananchi hususani vijana kuchangamkia fursa zilizopo kwenye mnyororo wa uboreshaji na usambazaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia na alisema kuwa Serikali kupita REA.
Aidha, ameelekeza wakandarasi wanaotekeleza miradi ya kusambaza umeme vitongojini kuhakikisha wanakwenda na kasi ya Serikali kwa kukamilisha miradi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa hasa ikizingatiwa kuwa fedha nyingi inatumika kutekeleza miradi hiyo na kwamba Serikali haitomvumilia mkandarasi mzembe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy alibainisha hatua mbalimbali zinazochukuliwa na hali ya utekelezaji wa miradi ya kusambaza nishati safi maeneo ya vijijini.
Mha. Saidy alitoa wito kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini kuchangamkia fursa ya kujiunganisha na huduma ya umeme na kwamba Serikali inaanza kutoa ruzuku kwa wananchi kwa ajili ya kuweka mifumo ya kutandaza nyaya ndani ya nyumba (wiring).






EmoticonEmoticon