RAS MCHATTA AWAFUNDA WATUMISHI UWEKEZAJI KWENYE MFUKO WA UMOJA WA UTT-AMIS

November 18, 2025

Na Oscar Assenga, TANGA

KATIBU Tawala Mkoa (RAS ) wa Tanga , Rashid Mchatta, amewataka watumishi wa umma kuchangamkia fursa za Mfuko wa Umoja wa Uwekezaji ( UTT-AMIS) kutokana na kwamba kwa uwezo walionao wanaweza kuwekeza na kupata mafanikio makubwa baadae.

Mchatta aliyasema hayo leo wakati akizungumza katika kikao cha utoaji elimu kwa watumishi wa Mkoa huo, kuhusu umuhimu wa uwekezaji kwenye mifuko ya uwekezaji ya pamoja inayoendeshwa na UTT-Amis.

Alisema kwamba hiyo ni fursa nzuri na muhimu kutokana na kwamba mfuko huo una mtaji mzuri wa kutosha, ulioanza na Shilingi bilioni 1, lakini kwa sasa mtaji wao umekuwa na kufikia zaidi ya Shilingi Trilioni 3.6 hivyo wakiwekeza, wanakuwa na uhakika wa kunufaika.

“Nitumie fursa hii kuwahamasisha watumishi wenzangu kuchangamkia fursa za uwepo wa mfuko wa umoja wa Uwekezaji wa UTT-Amis, ukiwekeza unakuwa na uhakika wa kunufaika na uwekezaji tulioufanya,”alisema .

Awali, Afisa Masoko Mwandamizi kutoka Taasisi ya Uwekezaji ya UTT-Amis Oliver Minja, alisema wanakutana na watumishi wa umma wakifanya uhamasishaji kutoa elimu ya uwekezaji kwenye mfuko UTT Amis, ili waweze kuitumia kuweka akiba kwa maisha yao ya sasa na badae.

Oliver alisema kwamba ni muhimu kwa watumishi waanze kuweka akiba, pamoja na na uwekezaji kwa ajili ya kutengeneza kesho yao kutokana na kwamba wanaweza kunufaika na fursa mbalimbali.

Alisema kwamba uwekezaji wa UTT ni huru na unapelekea kurugenzi ya uwekezaji izunguke sokoni kila siku na lazima ichukuliwe iende sokoni kufanya uwekezaji na hawana namna ya kulala na fedha za watu.

Alisema urahisi wa kuwekeza UTT-Amis ni mkubwa kutokana na kwamba wanaweza kupitia mabenki yaliyopo kwenye maeneo mbalimbali nchini, na hivyo kutoa urahisi wa kuwekeza na kuyafikia masoko ambayo wasingeweza kuyafikia

“Watumishi wenzangu hii ni fursa nzuri itakayotuwezesha kukidhi mahitaji yetu ya sasa na baadae hivyo hakikisheni kwenye mishahara yenu mnatoa asilimia 10 wekezeni kwa kutengeneza kesho yenu ”Alisema

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »