Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akipata maelekezo ya ziada
kuhusu ujenzi wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa kwenye eneo la Lakilaki
Jijini Arusha. Aneyetoa maelezo ni Afisa Mambo ya Nje na Mwansheria Bw.
Elisha Suku. Kushoto kwa Waziri Mahiga ni Nd. Hamdouny Mansour, Katibu
Tawala Msaidizi upande wa miundombinu.
Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa na ujumbe wake wakiangalia eneo
la eka 16 ambapo majengo manne ya Mahakama ya Umoja wa Mataifa
yanajengwa. Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika Mwezi Aprili mwaka 2016.
Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa akiwa na Mkuu wa Wilaya ya
Arumeru mkoani Arusha Mhe. Wilson Nkhambaku baada ya kukagua eneo hilo
na kuridhika na kasi ya ujenzi uliozingatia viwango vya kimataifa na
vile vya Umoja we Mataifa.
Mhe.
Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Kikanda na Kimataifa akiwa na ujumbe wake baada ya kumaliza
ukaguzi wa ujenzi wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa jijini Arusha.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali imeridhishwa na maendeleo na kasi ya ujenzi wa Mahakama
ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa ya Masalia ya kesi za Mauaji ya Kimbari
ya Rwanda (Mechanism for International Criminal Tribunals (MICT) katika
eneo la Lakilaki jijini Arusha, uliozinduliwa rasmi Julai mosi mwaka
huu.
Akikagua ujenzi huo na kupokea taarifa kutoka kwa wakandarasi na
wasimamizi wa ujenzi wa majengo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje,
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mheshimiwa Dkt.
Augustine Mahiga, amesisitiza kuwa ujenzi huo uzingatie viwango vya
kimataifa ili kuhakikisha usalama wa nyaraka na ushahidi utakaohifadhiwa
kwenye majengo hayo.
Alieleza kuwa ahadi ya Serikali iko palepale kushirikiana na Umoja
wa Mataifa na kuhakikisha kuwa miundombinu muhimu kama vile barabara,
umeme na maji vinapatikana kwenye eneo hilo ambapo ujenzi unaendelea kwa
kasi ya kuridhisha.
“Nimefurahishwa na maendeleo ya ujenzi huu kwani hii ilikua kazi
yangu ya mwisho nilipokuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kule Umoja
wa Mataifa, kutetea mahakama hii ijengwe hapa Arusha.
Akifafanua miundombinu iliyowekwa na Serikali ya Mkoa wa Arusha,
Katibu Tawala Msaidizi upande wa miundombinu Nd. Hamdouny Mansour
alisema kuwa kwa upande wa upatikanaji wa maji, mkoa umefanikisha
upatikanaji wa bomba maalum linaloleta maji kwenye eneo la ujenzi
mojakwamoja bila kuathiri upatikanaji wa maji maeneo mengine pembezoni
ili kutimiza azma hiyo ya Serikali.
Ujenzi huo wa Mahakama unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa
unatarajiwa kuwa na majengo makuu manne; jengo la mahakama, jengo la
uhifadhi wa nyaraka, jengo la ulinzi na jengo la ofisi za Umoja wa
Mataifa. Msimamizi wa ujenzi wa Umoja wa Mataifa alielezea teknolojia ya
kisasa itakayotumika kujenga jengo la kuhifanyia nyaraka haitahitaji
kutumia viyoyozi ili kuhifadhi uhasilia wa nyaraka.
Kwa upande wa wakandarasi wanaojenga ambao ni kampuni kutoka India
walielezea changamoto iliyopo kwenye ujenzi huo ni kutekeleza mpango wa
kupanda mti aina ya mshita-acacia, utakaomaanisha haki ambayo
kihistoria na jadi za kiafrika ilipatikana kwa mazungumzo kwenye
mabaraza ya kijiji. Mti huo wa mshita au Tree of Justice utapandwa ndani
katikati ya majengo hayo manne.
Serikali kupitia Hazina ilinunua eneo hilo la Lakilaki lenye ekari
431 na kukabidhiwa Wizara ya Mambo ya Nje ambapo limetengwa mahsusi kwa
ajili ya ujenzi wa taasisi mbalimbali za kimataifa. Taasisi nyingine
zinazotarajiwa kujengwa kwenye eneo hilo ni African Union Advisory Board
on Corruption (AUABC), African Institute of International Law (AIIL) na
African Court on Human and Peoples' Rights (ACHPR).
Ujenzi wa majengo haya ya awali kwenye eneo la Lakilaki
unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwakani. Ujenzi huo ulizinduliwa
rasmi Julai mwaka huu wa 2015 na Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
20 Desemba, 2015
EmoticonEmoticon