YANGA SC YAPATA BONGE LA BEKI TAIFA STARS, MWENYEWE ASEMA YUKO NJIA MOJA JANGWANI

May 15, 2015

Mwinyi Hajji Mngwali tayari kutua Yanga
Na Mahmoud Zubeiry, RUSTENBURG
BEKI wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mwinyi Hajji Mngwali amesema yuko tayari kutua Yanga SC.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa, Mngwali anayechezea KMKM ya Zanzibar amesema amefanya mazungumzo ya awali na Yanga SC na kimsingi yuko tayari kutua Jangwani.
“Ndiyo, Yanga wamezungumza na mimi, ila hatujamalizana. Lakini niseme wazi niko tayari kutua Yanga SC,”amesema.
Mngwali yupo katika kikosi cha Taifa Stars ambacho kipo Afrika Kusini kwa ajili ya michuano ya Kombe la COSAFA.
Stars iliwasili Johannesburg, Afrika Kusini usiku wa juzi na ikalazimika kulala huko kabla ya jana asubuhi kuunganisha safari kwa basi kuja Rustenburg ambako imefikia hoteli ya Hunters, nje kidogo ya mji.
Wachezaji waliowasili na Stars hapa ni makipa: Deogratius Munish ‘Dida’ (Yanga) na Mwadini Ali (Azam), mabeki ni Shomary Kapombe, Aggrey Morris, Erasto Nyoni (Azam), Oscar Joshua, Kelvin Yondani (Yanga), Abdi Banda, Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Mwinyi Hajji Mngwali (KMKM).
Wengine ni viungo; Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo (Azam), Said Juma, Salum Telela, Hassan Dilunga (Yanga), Said Ndemla (Simba) na Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar).
Washambuliaji ni Ibrahim Hajib (Simba), Mrisho Ngassa (Free State Stars), Simon Msuva (Yanga), John Bocco (Azam FC) na Juma Luizio (ZESCO United).
Taifa Stars imepangwa pamoja na Namibia, Lesotho na Zimbabwe katika Kundi A, wakati Kundi B lina timu za Shelisheli, Madagascar, Mauritius na Swaziland.
Kila timu itakayoongoza kundi, itaungana na wenyeji Afrika Kusini, Botswana, Ghana, Malawi, Msumbuji na Zambia kwa ajili ya hatua ya Robo Fainali.
Mpinzani wa Tanzania katika hilo, anatarajiwa kuwa Zimbabwe, ambaye hata hivyo alitolewa na Taifa Stars katika mechi za kufuzu AFCON mwaka jana.
Afrika Kusini, Botswana, Ghana, Malawi, Msumbuji na Zambia zimeingia moja kwa moja katika Robo Fainali kwa sababu zipo juu viwango vya ubora wa soka vya FIFA.
Kombe la COSAFA lilianza mwaka 1997 linajumuishaa nchi 16 wanchama kutoka Kusini mwa Bara la Afrika, limekua likifanyika kwa kushirikisha nchi wanachama waliopo Kusini mwa bara la Afrika.
Nchi wanachama wa COSAFA ni Afrika Kusini, Angola, Botswana, Comoro, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Mayotte, Msumbuji, Namibia, Reunion, Shelisheli, Swaziland, Zambia na Zimbabwe, lakini katika kuiongezea ladha ya ushindani, sasa hivi zinaalikwa na timu kutoka nje ya ukanda huo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »