Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha Maafisa Elimu Kata kusimamia kwa ufanisi shughuli zote za elimu katika ngazi ya Kata.
Dkt. Maulid J. Maulid amesema Maafisa Elimu Kata wana wajibu wa kutambua na kutafsiri kwa vitendo maono ya Serikali kwa kuhakikisha wanakuwa wasimamizi wa kwanza wa maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya elimu kwa kuboresha Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 Toleo la 2023 na Mtaala ulioboreshwa ili kufikia lengo la Serikali la kuboresha na kuimarisha sekta ya elimu nchini.
“Mabadiliko na mageuzi yanayotegemewa kutokea kwa utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mtaala ulioboreshwa yako kwenye meza zenu kama wasimamizi wa kwanza wa shughuli za elimu katika ngazi ya Kata. Tunawaomba mwende mkasimamie ipasavyo mageuzi hayo na tuone matokeo kuanzia kwenye ngazi ya Shule na Kata kwa kwenda kutekeleza kwa vitendo yale mtakayojifunza kwenye mafuzo haya kwani hayo ndio yatakuwa dira ya kuwasaidia kufanya usimamizi fanisi wa shughuli zote za elimu katika ngazi ya Kata na hatimaye lengo la Serikali kufikiwa”. Amesema Dkt. Maulid.
Aidha, Dkt. Maulid amesisitiza Maafisa Elimu Kata hao kuitambua, kusoma, kuelewa na kutekeleza miongozo yote inayotolewa na Mamlaka zinazosimamia elimu nchini ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Kamishna wa elimu ili iwasaidie katika utekelezaji wa majukumu yao ya usimamizi wa shughuli za elimu kwenye ngazi ya Kata kwa ufanisi.
Vilevile Dkt. Maulid amesisitiza usimamizi wa nidhamu, uwajibikaji, ufundishaji na ujifunzaji mahiri wenye kuinua ubora wa elimu inayotolewa shuleni.
Nae Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Dkt. Alphonce J. Amuli amesema washiriki wa mafunzo hayo watajengewa uwezo katika maeneo ya Uongozi, Usimamizi na Utawala katika Elimu, Utawala Bora katika Elimu, Uandaaji wa Mpango wa Jumla wa Maendeleo ya Elimu Ngazi ya Serikali za Mitaa, Ufuatiliaji na Usimamizi Fanisi wa Shule, Usimamizi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Shule, Ukaguzi wa Ndani, na Ushirikishwaji wa Jamii na Utatuzi wa Malalamiko katika Elimu. Dkt. Amuli pia amesema kuwa ni dhahiri kwamba, maeneo hayo yatakayowezeshwa yatasaidia kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa shule kwa ufanisi.
Mafunzo ya Utawala Bora wa Elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa yanafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 25 – 27 Juni, 2025 ADEM Bagamoyo na yamefadhiliwa na mradi wa BOOST chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia


EmoticonEmoticon