MASHUJAA BAND KUBURUDISHA KILIMANJARO MARATHON

February 22, 2015

Na Mwandishi Wetu

BENDI mpya inayotamba kwa sasa hapa nchini na ambayo imechukua tuzo mbalimbali za muziki hapa nchini Mashujaa Band Jumapili tarehe 1 Machi inatarajia kushuka mjini Moshi katika ukumbi wa Uwanja wa Chuo cha Ushirika kuwapa burudani washiriki pamoja na wananchi wote watakaofika kwenye uwanja huo kwa ajili ya mbio za Kilimanjaro Marathon 2015.

Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli alisema kuwa bia ya Kilimanjaro Premium Lager imeandaa burudani hiyo ikiwa ni mojawapo ya burudani zilizoandaliwa kwa ajili ya kuongeza msisimko katika mbio hizo.
Alisema kuwa siku ya Kilimanjaro Marathon bendi ya Mashujaa watatoa burudani hiyo kwa kushirikiana na kundi la Jambo Squad kutoka Arusha.

Kikuli aliongeza kuwa Jambo Squad pamoja na Warriors From The East la Arusha kwa pamoja wataanza kuchangamsha mji wa Moshi kuanzia usiku wa Ijumaa tarehe 27 ambapo watatoa burudani kabambe kwa wakazi wa Moshi kwenye ukumbi wa Voda House ikiwa ni burudani mahususi kuelekea Kilimanjaro Marathon.

Mbali na burudani ya muziki siku ya Kilimanjaro Marathon kutakuwa na burudani mbalimbali katika viwanja hivyo pamoja na nyama choma kutoka bar mbalimbali maarufu za Moshi ambao watachoma nyama na kuuza vinywaji uwanjani hapo.
John Addison, Mkurugenzi Mkuu wa Wild Frontiers, waandaaji wa mbio hizo alisema kuwa wanariadha wanaotaka kushiriki mbio hizo wataweza kujiandikisha tarehe 26 jijini Arusha kwenye Hoteli ya Kibo Palace na kwa Moshi watajiandikisha Keys Hotel tarehe 27 na tarehe 28 Februari 2015 kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa 12 jioni.

Aliongeza kuwa mbio ndefu la Kilimanjaro Premium Lager Marathon za kilomita 42 zitaanza saa 12.30 asubuhi kutokea uwanja wa Ushirika wakati mbio za Tigo Kili Half Marathon zitaanzia nje ya geti la Chuo cha Ushirika saa moja kamili asubuhi na kukimbia wakielekea Mweka na mbio yao itaishia hapo hapo uwanjani. Wakati huo huo mbio za walemavu za Gapco zitaanza saa 12.45 (saa moja kasorobo) kutokea uwanja wa Ushirika na huku mbio za kujifurahisha za 5 km Fun Run zikianza saa 1.45 asubuhi kwenye mzunguko wa YMCA na kumalizikia uwanjani.

Addison alisema kuwa maandalizi ya kutosha yamefanyika kuhakikisha washiriki wanafurahia mbio hizo kwani kila mdhamini atakuwa na vituo maalum vya maji ya kunywa na viburudisho na burudani nyingine katika vituo hivyo ambavyo vitakuwepo kila baada ya kilometa chache katika njia zitakapopita njia hizo”.

Mbio za Kilimanjaro Marathon 2015 zinaratibiwa na Executive Solutions kwa kushirikiana na Riadha Tanzania, Riadha Kilimanjaro na Kilimanjaro Marathon Club huku zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Tigo, GAPCO, Simba Cement, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar,  CMC Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania, Kibo Palace Hotel, UNFPA na Kilimanjaro Water.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »