WAZIRI MKUU: ANZISHENI HALMASHAURI NYINGINE KILOLO

February 22, 2015

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Iringa uangalie uwezekano wa kuanzisha Halmashauri mpya katika wilaya ya Kilolo kata ya Mahenge na tarafa ya Mahenge kwa sababu ya hali ya kijiografia ya eneo hilo.

“Makao makuu ya wilaya hii yako Kilolo kule milimani. Ukitaka kuja huku ni lazima upite kwanza mjini ndipo ufike huku. Hapana! Hatuwezi kuwasaidia wananchi hawa kujiletea maendeleo kwa staili hii,” alisema Waziri Mkuu.
Alikuwa akihutubia wakazi wa vijiji vya Nyanzwa na Igunda wilayani Kilolo, jana jioni (Jumamosi, Februari 21, 2015) mara baada ya kukagua mradi wa umwagiliaji wa Nyanzwa ambao ni maarufu kwa kilimo cha vitunguu. Vijiji hivyo viko umbali wa km. 120 kutoka Ipogoro ilipo njia panda ya kwenda Iringa mjini na km. 155 kutoka Kilolo mjini yalipo makao makuu ya wilaya hiyo.
Waziri Mkuu alisema kata za tarafa hiyo ni kubwa mno kwa mtendaji kuweza kusukuma maendeleo ya wananchi. “Kata hii imeanzia Kitonga hadi huku Nyanzwa. Hivi ni mtendaji gani anayeweza kuja kuhimiza shughuli za maendeleo akitokea huko?” alihoji Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
Alisema mbali na idadi ya watu, suala la kijiografia huwa linaangaliwa wakati wa kuanzisha maeneo ya utawala. “Hili eneo ni zuri, fursa zipo lakini linakosa usimamizi ndiyo maana hata wilaya hii inaongoza kwa umaskini kuliko wilaya nyingine za mkoa huu. Acheni wilaya ibaki moja, mbunge abaki mmoja lakini Halmashauri ziwe mbili ili muweze kusukuma maendeleo ya eneo hili kwa sababu mtakuwa na madiwani wenu na bajeti yenu,” alisema.
Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mtendaji wa Kijiji cha Nyanzwa, Bw. Hekima Masanula Katemo alisema skimu ya umwagiliaji ya Nyanzwa ilijengwa mwaka 1960 wakati huo kwa kutumia banio la miti na magunia ya mchanga. Ilikuja kuboreshwa miaka ya 90 kwa ufadhili kutoka Jumuiya ya Ulaya na Serikali ya Sweden.
“Hata hivyo, skimu hii ambayo inahudumia wakulima 3,469 wakiwemo wanaume 1,662 na wanawake 1,807; inakabiliwa na uhaba wa maji kwani ni hekta 256 tu ambazo zinamwagiliwa kwa sasa wakati eneo lote la mradi ni hekta 940,” alisema Bw. Masanula.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake mkoani Iringa kwa kutembelea Manispaa ya Iringa ambako atakagua ujenzi wa maabara kwenye shule ya sekondari Kihesa, kuzindua kituo cha polisi cha Semtema, na kukagua huduma za afya kwenye hospitali ya manispaa ya iringa. Pia atakagua mradi wa machinjio ya kisasa ya Ngelewela kabla ya kutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja wa shule ya msingi Ipogolo.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »