KLABU 12 ZA TIMU ZA MAVETERAN KUSHIRIKI TAMASHA MAALUMU SEPTEMBA 6.

August 17, 2014
Na Elias Kimaro
KLABU 12 za timu za soka za maveterani zinazooundwa na nyota wa zamani nchini zinatarajiwa kuchuana katika michezo maalum ya Tamasha la Miaka 16 ya Home Gym, itakayofanyika Septemba 6 kwenye uwanja wa Mwenge, Dar es Salaam.
 
Kwa mujibu wa mratibu wa tamasha hilo, Andrew Mangomango, klabu zilizothibitisha kushiriki tamasha hilo ambalo litapambwa na burudani ya muziki na michezo mingine kama ya kufukuza kuku, mbio za kwenye magunia na kuvuta kamba ni pamoja na Mbagala Veterani, Boko, 501, Break Point, Survey, Mwenge na Msasani.
 
Mangomango alizitaja nyingine kuwa ni Biafra Veterani, Meeda, Mikocheni, Mbezi, Mabenzi, Segerea na Ukonga Veterani ambazo zinaundwa na nyota wa zamani wa kandanda waliowahi kutamba na timu za Simba, Yanga na Taifa Stars.
 
Mratibu huyo aliongeza kuwa, siku hiyo klabu zaidi ya 30 za Jogging toka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam nazo zitashiriki tamasha hilo kabla ya baadaye washiriki wote kujumuika pamoja kuwatembelea yatima wanaolelewa kituo cha Chakuhama kwa ajili ya kuwapeleka misaada mbalimbali.
 
"Mbali na soka la maveterani, siku hiyo pia kutakuwa na michezo ya netiboli, kufukuza kuku, kukimbia kwenye magunia, kuvuta kamba na shoo za watunisha misuli, wanyanyua vitu vizito, mabondia na watu wa karate, pia burudani ya muziki itakuwapo japo mpaka sasa hatujajua tutasindikizwa na bendi gani," alisema Mangomango.
 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »