Na Boniface Wambura, Dar es salaam
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeamua kurejesha ofisi zake Uwanja
wa Kumbukumbu ya Karume kwa vile mipango ya uendelezaji wa eneo hilo
bado haijakwenda kama ilivyopangwa awali.
Uamuzi
huo ni moja ya maazimio yaliyofikiwa kati ya Kamati ya Utendaji ya TFF
na ujumbe wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliokuwepo
nchini kwa wiki nzima kwa ajili ya kufanya mapitio (review) ya
uendeshaji wa TFF.
Akizungumza
Dar es Salaam leo (Agosti 17 mwaka huu), kiongozi wa ujumbe huo wa FIFA
uliokuwa na maofisa sita, Zelkifli Ngoufonja amesema wamepitia maeneo
mbalimbali ya uendeshaji wa TFF na mpira wa miguu kwa ujumla na
kukubaliana kufanya uboreshaji kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Ngoufonja
ambaye ni Meneja Mwandamizi wa FIFA anayeshughulikia Programu za
Maendeleo Afrika amesema kabla walikutana na wadau mbalimbali ikiwemo
Serikali kwa lengo la kuangalia jinsi watakavyochangia katika
uendelezaji mpira wa miguu nchini.
Amesema
wamekubaliana na TFF katika mpango wa utekelezaji (Action Plan) na
maazimio waliyokubaliana ikiwemo na muda wa utekelezaji wake, hivyo FIFA
watafuatilia na kutoa msaada ili kuhakikisha utekelezaji unafanyika
kama ilivyopangwa.
Maeneo
yaliyofanyiwa kazi ni utawala bora (Governance), Maendeleo ya Ufundi
(Technical Development), timu za Taifa (National teams), Mashindano na
Vitendea Kazi (Competitions and Facilities), na Utawala na Uongozi
(Administration and Management).
Maofisa
wengine wa FIFA waliofuatana na Ngoufonja ambaye ni raia wa Cameroon ni
Meneja wa Programu za Ustawi (Performance), Marco Schuepp, Ofisa
Maendeleo, Ashford Mamelodi, Ofisa Maendeleo wa Ufundi, Govinden
Thondoo, Mkufunzi wa Makocha, John Peacock na Mshauri wa Programu za
Ustawi, Ian Riley.
EmoticonEmoticon