*HABARI KUTOKA TFF LEO, WANACHAMA WA TFF KUANDALIWA KATIBA MFANO YA MAREKBISHO
Kamati
ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekutana Machi 30 mwaka huu
kujadili utekelezaji wa maagizo ya TFF kwa wanachama wake kurekebisha
Katiba zao ili ziendane na Katiba ya TFF pamoja na ile ya FIFA kabla ya
Machi 30 mwaka huu.
Vyama
vya mikoa Lindi na Dar es Salaam na Chama cha Mpira wa Miguu cha
Wanawake (TWFA) viliomba kuongezewa muda wakati vingine vimeomba Katiba
mama kama angalizo lao la mabadiliko hayo. Klabu ya Simba Sports ndiye
mwanachama pekee aliyewasilisha mabadiliko ya Katiba. TFF inawapongeza
viongozi na wanachama wa klabu hiyo kwa kufanya mkutano wao kwa utulivu.
Kamati
itatangaza nyongeza ya muda wa kufanya mabadiliko hayo baada ya
kuviandalia vyama vya mikoa na vyama shiriki katiba mfano kwa ajili ya
kurahisisha shughuli hiyo.
Baada ya kupitia uamuzi wa wanachama wa Simba S.C. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeamua ifuatavyo:
(i) Kwa
kuwa pendekezo la wanachama wa Simba kubadili kipengele na 26 kuhusu
sifa za mgombea kinapingana na kipengele na 29 (4) cha Katiba ya TFF,
hivyo basi Kamati imeagiza kipengele cha Katiba ya Simba kibaki vilevile
bila kubadilishwa.
(ii) Vipengele vingine vyote vimepitishwa na vitapelekwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kwa ajili ya kusajiliwa.
(iii) Mchakato
wa uchaguzi wa Klabu ya Simba uendelee kama ulivyopangwa wakizingatia
uamuzi huu wa Kamati. TFF inaitakia Klabu ya Simba uchaguzi mwema.
Pia
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeshauri TFF kuwasiliana na
FIFA kupata mwongozo kuhusu katazo la watu wenye rekodi ya kifungo
kugombea.
TFF
imepokea ushauri huo na itaufanyia kazi na kama kuna mabadiliko yoyote
kiutaratibu yataanzia katika Katiba ya TFF kupitia Mkutano Mkuu.
*RAMBIRAMBI MSIBA WA DK HEMED MZIRAY
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
daktari wa tiba ya michezo, Dk. Hemed Mziray kilichotokea juzi jijini
Dar es Salaam.
Dk.
Mziray ambaye alikuwa mfanyakazi wa Hospitali ya Manispaa ya Temeke na
mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Tiba ya Michezo Tanzania
(TASMA) amesafirishwa kwenda kwao mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya
mazishi.
Msiba
huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti
Dk. Mziray ameshirikiana na TFF na wadau wengine wa mpira wa miguu
katika masuala ya tiba na uongozi.
Alikuwa
kiungo kati ya Uwanja wa Taifa ambapo mechi za kimataifa, za ligi na za
kirafiki zimekuwa zikichezwa na Hospitali ya Temeke kwa wagonjwa
wanaohitaji huduma zaidi, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Dk. Mziray, TASMA na wafanyakazi
wa Hospitali ya Temeke na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika
kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Pia TFF inatoa ubani wa sh.
200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina
EmoticonEmoticon