KIDUNDAI WALILIA MAJI SAFI

December 02, 2013
WAKAZI zaidi ya 1,500 wa kijiji cha Kidundai kilichopo kata ya Vuga katika halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto wanaiomba serikali kulitafutia ufumbuzi tatizo la kukosekana kwa huduma ya maji safi kijijini humo ili nao waweze kuishi kama watanzania wengine.

Wamesema wamechoka kudhaliliaka kwa kulazimika kuchangia chanzo pekee cha maji yasiyo salama na mifugo yao kwa zaidi ya miaka 20 sasa, maji ambayo yanapatikana katika mfereji wa Mbokoi ulioko umbali wa km. 3 kutoka kijijini kwao.

Wametoa kauli hiyo walipozungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa Tanga Raha alipotembelea kijijini humo mwishoni mwa wiki.


Zuhura Shabani alisema hali ni mbaya hasa katika miaka ya hivi karibuni kwakuwa kuwepo kwa mabadiliko ya tabia nchi yaliyoleta ukame kumesababisha visima vya asili kukauka na pia kiasi cha maji kupungua zaidi katika mfereji huo.

“Wanawake na watoto hivi sasa tunalazimika kuamka saa tisa za usiku ili mtu uweze kuwahi foleni ya kuchota ndoo moja ambayo hata hivyo haiwezi kutosheleza mahiji ya familia nzima kwa siku”,alisema na kuongeza.
“Kero hii inatuathiri sana ki uchumi kwasababu mchuuzi akileta ndoo moja ya maji hadi hapa Kidndai anaiuza kwa sh. 800 kiasi ambacho mkulima wa kawaidi huwezi kuwa nacho pia kiafya kwasbabu tunalaimika kuoga kila baada ya siku nne kutokana ugumu wa kupata maji hayo ya kutosheleza mahitaji ya familia tunaomba serikali ituletee huduma ya maji kama watanznia wengine”,alisema

Naye Bashiru Semahonge alisema kukosekana kwa huduma ya maji safi kijijini hapo pamoja na kuathiri ustawi wa familia pia kumepunguza sana muda wa wanakijiji kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji hasa kilimo.

“Wanafunzi nao wameathirika ki taaluma kwasababu asubuhi wanalazimika kwenda kuwasaidia kwanza mama zao kuchota maji ambako wanatumia zaidi ya saa nne ndipo apate angalau ndoo moja kwa hiyo hali hiyo inawakosesha vipindi vyote vya asubuhi kila siku”,alisema.

Mohamed Abdala alisema wakati umefika kwa serikali kuahakikisha wanawapatia huduma ya majisafi haraka badala ya kusubiri wakati wa kampeni za uchaguzi ambapo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia kero hiyo kuwarubuni ili kujipatia kura za kuwaingiza madarakani.

“Mwaka 2005 ilifanyika Survey katika chanzo cha maji cha Kwamwente ili kuweza kutuleta maji hapa kidundai baada ya kazi kukamilika wahusika waliamua kukaa kimya badala yake baadhi ya wanasiasa wakauchukua ule mchoro”,alisema na kuongeza.

“Katika kampeni zao walituhamasisha sana na kuahidi kwamba tukiwachagua maji yatafika kwahiyo tukawapa kura zetu lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika badala yake wameturudishia mchoro wetu…. sasa sisi tukachote maji kwenye huo mchoro?”, alihoji Abdala.

Kijiji hicho kinaundwa na vitongoji vitano vya Kidundai, Kibwilo, Kweluhogo, Maili tano na Bangala chini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »