NEWALA KUNUFAIKA NA UMEME WA UHAKIKA

July 21, 2026



📌*Ni baada ya kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme ya kilovoti 33 Masasi - Mtwara*


📌*Mradi umeimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa Wilaya ya Newala na maeneo jirani.*


📌*MD Twange asema thamani ya mradi ni takribani shilingi bilioni 4.65*



📍Newala, Mtwara | Julai 22, 2026


Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amezindua rasmi mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 33 kutoka Masasi hadi Newala, akieleza kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na kuweka mazingira wezeshi kwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika Wilaya ya Newala.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa njia hiyo, Mhe. Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya umeme ili kuhakikisha huduma ya nishati inawafikia wananchi wengi zaidi na kuwa chachu ya maendeleo.

"Njia hii ya umeme ni msingi wa kukuza uchumi, kuongeza uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kuboresha upatikanaji wa umeme kwa Wilaya ya Newala," amesema Mhe. Ndejembi.


Aidha, Waziri Ndejembi amesema Serikali itaendelea kuhakikisha Mikoa ya Lindi na Mtwara inapata umeme wa uhakika ikiwa ni pamoja na kuiunganisha Mikoa hiyo na umeme wa gridi ya Taifa.

Akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Newala, Mhe. Mwangi Kundya amesema miradi mbalimbali imeendelea kutekelezwa Mkoa wa Mtwara.


"Mheshimiwa Waziri niipongeze Serikali kwani Vijiji vyote vya Mkoa wa Mtwara 785 vinapata huduma ya umeme". Amesema Mhe. Mwangi.



Ameongeza kuwa katika kuboresha huduma kwa wateja mkoa wa Mtwara umepokea vitendea kazi yakiwemo magari kumi na moja, bajaji nne na pikipiki tisa.

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba amesema Serikali imekuwa ikiboresha uwekezaji na upatikanaji wa umeme Mikoa ya  Mtwara na Lindi.


"Mahitaji ya Lindi na Mtwara yameendelea kuongezeka na Serikali imewekeza kwenye uzalishaji na hivi sasa Mkoa wa Mtwara tunazalisha zaidi ya megawati 50". Amesema Mha. Mramba.

Awali akitoa taarifa za utekelezaji wa mradi Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Bw. Lazaro Twange amesema ujenzi wa njia hiyo umetekelezwa kwa shilingi bilioni 4.56 kwa umbali wa Kilometa 76 kutoka Masasi hadi Newala.

"Mheshimiwa mgeni rasmi kabla ya mradi huu kutekelezwa Wilaya ya Newala ilikuwa ikipata umeme kutokea Mtwara kupitia Nanyumbu umbali wa kilometa 170, hali iliyochangia tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara". Amesema Bw. Twange.



Ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa njia hiyo ya umeme kumeimarisha upatikanaji wa umeme na kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme kwa Wilaya hiyo.



Aidha, Serikali kupitia TANESCO imetenga takribani shilingi bilioni 5.27 kwa ajili ya kujenga kituo cha kubadilishia umeme (Switching Station) kitakacho saidia kuboresha upatikanaji wa umeme na kukidhi mahitaji ya sasa na ya badaye ya wananchi na wawekezaji wa Wilaya ya Newala. 


Mbunge wa Newala Vijijini Dkt. Yahaya Nawanda kwa niaba ya Wabunge wa Mkoa wa Mtwara ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme Mkoa wa Mtwara.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »