Showing posts with label habari. Show all posts
Showing posts with label habari. Show all posts

SAYANSI YA NYUKLIA YAFUNDISHWA KWA WANAFUNZI ZAIDI YA 9,000 TANGA

September 29, 2025 Add Comment

 




Na Mwandishi Wetu, Tanga


Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeendesha kampeni maalum ya kutoa elimu ya mionzi kwa wanafunzi 9,391 wa shule 10 za sekondari mkoani Tanga, ikiwa ni hatua ya kuondoa dhana potofu kuhusu teknolojia ya nyuklia na kuhamasisha kizazi kipya kuelekea sayansi.

Kampeni hiyo ilifanyika kuanzia Septemba 22 hadi 26, 2025 katika shule za Chumbageni, Galanosi, Kiomoni, Mikanjuni, Mkwakwani, Usagara, Nguvumali, Pongwe, Mabokweni na Msambweni.

Kupitia mafunzo ya vitendo, mijadala ya papo kwa papo na maonesho ya vifaa vya mionzi, wanafunzi walipata uelewa wa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia katika sekta za afya, kilimo, viwanda na mazingira.

TAEC wamesema elimu hiyo inalenga kuondoa hofu kwa jamii, kuandaa wataalamu wa baadaye na kuchangia mapambano dhidi ya saratani kupitia tiba ya mionzi (radiotherapy).

“Tunataka vijana wetu waelewe kuwa mionzi siyo silaha pekee, bali pia ni tiba, chakula bora na usalama wa mazingira. Wanafunzi hawa ndio wataalamu wa kesho,” walisema wataalamu hao.

TAEC pia imesisitiza kuwa elimu hii ni mchango katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan afya bora, elimu bora, nishati na viwanda pamoja na ulinzi wa mazingira.

Kwa kuwahamasisha wanafunzi kuchukua masomo ya sayansi, TAEC inalenga kuongeza idadi ya wataalamu katika fani za fizikia tiba, uhandisi wa nyuklia na usalama wa mionzi.

Kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa tume hiyo kuhakikisha taifa linakuwa na kizazi chenye maarifa ya sayansi ya nyuklia kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.









DKT.BITEKO AMPA POLE RAIS MWINYI,ASHIRIKI MAZISHI YA KAKA YAKE

September 27, 2025 Add Comment

 

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameungana na mamia ya waombolezaji kutoa pole kwa familia ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kufuatia kifo cha kaka yake Abass Mwinyi ambaye pia alikuwa mgombea Ubunge wa Jimbo la Fuoni kilichotokea Zanzibar, Unguja  usiku wa kuamkia Septemba 25, 2025.

Dkt. Biteko ameshiriki mazishi hayo Septemba 26, 2025 Bumbubwini Mangapwani, Zanzibar.

Ambapo ameungana na viongozi mbalimbali akiwemo Mgombea Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Ndugu Stephen Wasira, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla .

Aidha, baada ya mazishi baadhi viongozi walipata fursa ya kutoa heshima katika kaburi la Hayati Ali Hassan mwinyi lililopo Bumbubwini Mangapwani, Zanzibar.

Awali, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alifika msibani kuwafariji wafiwa na kisha kusaini kitabu cha maombolezo.

TUME YA UTUMISHI WA UMMA KUFANYA MKUTANO WA KWANZA 2025/2026 DODOMA

September 26, 2025 Add Comment

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John C. Mbisso,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Septemba 26, 2025 jijini Dodoma, kuelekea Mkutano wa Kwanza wa Tume unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 29 Septemba hadi 17 Oktoba 2025 jijini Dodoma.


NA OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA


Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, John Mbisso, amesema Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa fedha 2025/2026, unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 29 Septemba hadi 17 Oktoba 2025 jijini Dodoma, katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) eneo la Njedengwa.

Mbisso ametoa taarifa hiyo leo Septemba 26, 2025 jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema mkutano huo utakuwa ni fursa muhimu kwa Tume kupokea, kujadili na kutoa maamuzi juu ya rufaa na malalamiko mbalimbali yaliowasilishwa na watumishi wa umma ambao hawakuridhika na maamuzi ya waajiri wao, mamlaka za ajira na mamlaka za nidhamu.

"Tume ina wajibu wa kisheria kupokea hoja hizo chini ya Sheria ya Utumishi wa Umma (Sura ya 298, marejeo ya 2023) pamoja na Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022,"

"Tume ya utumishi wa umma imepanga kujadili na kutoa uamuzi wa rufaa na malalamiko mbalimbali zaidi ya mia moja yaliyowasilishwa na watumishi wa umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na waajiri, mamlaka za ajira na mamlaka zao za nidhamu," amesema Mbisso

Mbisso pia ameongeza kuwa katika mkutano huo, warufani au warufaniwa walioomba watapewa nafasi kupiga hoja zao mbele ya Tume, kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu rufaa zao, kama vile inavyowekwa wazi kwenye Kanuni ya 62(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma. Aidha, taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa robo ya tatu na robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025 zitawekwa mbele ya wajumbe wa mkutano kwa majadiliano na utoaji wa mwelekeo.

Akizungumza juu ya umuhimu wa mkutano huo, Mbisso amesisitiza kwamba ni sehemu ya uwajibikaji wa Tume kuhakikisha utendaji kazi wa utumishi wa umma unafuatana na sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayoweka haki na uwazi kwa watumishi wote. Katika hafla nyingine, amefungua kikao kazi cha ndani cha Tume ambapo aliagiza mapitio ya miongozo ya ndani, akisisitiza kuwa Tume lazima iendelee kujiboresha ili kuendana na mahitaji ya wakati na changamoto zinazowakabili watumishi wa umma.

FCC YAIMARISHA USHIRIKIANO NA TUME YA USHINDANI YA AFRIKA KUSINI

FCC YAIMARISHA USHIRIKIANO NA TUME YA USHINDANI YA AFRIKA KUSINI

September 26, 2025 Add Comment

 

Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) imeingia makubaliano rasmi ya ushirikiano na Tume ya Ushindani ya Afrika Kusini (CCSA) kwa lengo la kuimarisha ulinzi wa ushindani wa haki na maslahi ya watumiaji katika nchi zote mbili.

Makubaliano hayo yalitiwa saini mwezi Septemba mwaka huu, wakati wa ziara ya kikazi ya siku tano ya viongozi wa FCC nchini Afrika Kusini. Hati hiyo ya makubaliano inalenga kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo kubadilishana taarifa, kujengeana uwezo kitaasisi, kufanya tafiti za pamoja na kuratibu utekelezaji wa sheria zinazohusu ushindani na ulinzi wa watumiaji.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, alisema makubaliano hayo yatasaidia kuongeza nguvu ya taasisi katika kulinda maslahi ya wananchi na pia kuendeleza masoko shindani barani Afrika.

Alisema ushirikiano huo utaleta mazingira bora ya biashara kwa kuchochea ubunifu, kuongeza ufanisi na kuhakikisha haki kwa wafanyabiashara na watumiaji.

“Tunatambua na kuthamini mafanikio ya Tume ya Ushindani ya Afrika Kusini. Uzoefu wao katika kushughulikia masuala magumu ya ushindani na ulinzi wa watumiaji utakuwa nyenzo muhimu kwetu tunapoboresha mifumo ya utekelezaji hapa nyumbani,” alisema Bi. Ngasongwa.

Aidha, alisisitiza kuwa MoU hiyo si makubaliano ya kiofisi pekee, bali ni daraja la kuunganisha taasisi hizo mbili, uchumi na zaidi ya yote wananchi wake katika kufanikisha lengo la pamoja la kuwa na masoko ya haki na jumuishi.

Kwa upande wake, Kamishna wa CCSA, Bi. Doris Tshepe, aliahidi mshikamano wa karibu katika utekelezaji wa makubaliano hayo. Alisema kubadilishana utaalamu na kufanya kazi kwa pamoja kutasaidia sana kushughulikia changamoto mpya zinazojitokeza katika sekta ya ushindani na ulinzi wa watumiaji barani Afrika.

“Makubaliano haya ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda. Unaonesha dhamira ya dhati ya nchi zetu mbili kuboresha mifumo ya kisheria na kuhakikisha masoko yenye uwazi na usawa, ambayo yatalinda maslahi ya watumiaji na wafanyabiashara kwa pamoja,” alisema Bi. Tshepe.

Viongozi kutoka taasisi zote mbili walieleza matumaini yao kuwa ushirikiano huu utazaa matunda ya kweli kwa Tanzania, Afrika Kusini na ukanda mzima wa Afrika kwa kuchochea uwazi, uwajibikaji na kulinda ustawi wa watumiaji.