MATHIAS CANAL AONGOZA UPATIKANAJI MIL 85 UJENZI WA KANISA KIOMBOI-IRAMBA

September 28, 2025
Mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya WAZOHURU MEDIA Ndg Mathias Canal amewaongoza Viongozi wa dini, Wadau wa maendeleo na Waumini kwenye harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania-KKKT Usharika wa St George Kiomboi Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.

Katika harambee hiyo iliyofanyika leo tarehe 28 Septemba 2025 katika eneo la Ujenzi wa Kanisa Mtaa wa Lulumba, Mgeni huyo rasmi amesimamia upatikanaji wa fedha taslimu Tsh 79,407,000 ambapo ahadi ni Shilingi Milioni 4,010,000 na jumla ya fedha zote zilizopatikana ni Shilingi Milioni 85,017,000.

Mgeni rasmi Ndg Mathias Canal pamoja na marafiki zake waliomuunga mkono amechangia jumla ya Tsh milioni 3,835,000 na mifuko 10 ya Saruji.

Akizungumza katika harambee hiyo Mathias amesema kuwa Kanisa ni nguzo muhimu ya maisha ya kiroho, kijamii na hata kiuchumi. Kupitia kanisa waumini wanajifunza misingi ya upendo, mshikamano, uadilifu na ujenzi imara wa taifa.

"Ujenzi wa kanisa si kwa ajili ya kizazi cha leo pekee, bali ni urithi wa vizazi vijavyo. Tunaposhiriki katika harambee hii, tunakuwa sehemu ya historia ya imani na mshikamano wa Kikristo, Mradi huu wa ujenzi wa kanisa la kisasa ni mfano wa kujitegemea kama kanisa, uzalendo, na dira ya maendeleo ya KKKT kwa ujumla Usharika wa St George, Jimbo la kati, na Dayosisi ya kati" Amesisitiza

Amewasihi waumini kuchangia ujenzi wa kanisa hilo kwani litakapokamilika litakuwa kanisa bora linalozingatia mahitaji ya sasa na baadaye yakiwemo ya watu wenye uhitaji maalumu na wanajamii ya Kiomboi. Kanisa linalojengwa lina uwezo wa kuhudumia waumini 2500, ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kuhudumia watu 300, ofisi 6 za viongozi, stoo ya vifaa vya meza ya Bwana, Duka la vitabu, sehemu ya kusomea, ukumbi mdogo wa chakula na vinywaji baridi kwa wakati moja.

Ujenzi huo wa kanisa upo katika awamu ya pili ya ukamilishaji wa ujenzi wa ukuta na kuanza kumwaga zege ya juu (Slab) ikiwa ni sehemu muhimu ya ujenzi katika zile awamu nne ambazo ni (1) Kujenga msingi, (2) Kujenga ukuta, (3) Kupaua jengo, na (4) kupaka rangi na umaliziaji.

Mathias ameongeza kuwa Ujenzi wa kanisa hilo unahitaji mshikamano wa dhati kati ya waumini, viongozi na wadau wote wa maendeleo hivyo amewasihi waumini kushikamana kwa moyo wa kujitolea; kwani inapojengwa nyumba ya Mungu, ni kujijengea wao na familia zao baraka zisizopimika.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »