SAYANSI YA NYUKLIA YAFUNDISHWA KWA WANAFUNZI ZAIDI YA 9,000 TANGA

September 29, 2025

 




Na Mwandishi Wetu, Tanga


Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeendesha kampeni maalum ya kutoa elimu ya mionzi kwa wanafunzi 9,391 wa shule 10 za sekondari mkoani Tanga, ikiwa ni hatua ya kuondoa dhana potofu kuhusu teknolojia ya nyuklia na kuhamasisha kizazi kipya kuelekea sayansi.

Kampeni hiyo ilifanyika kuanzia Septemba 22 hadi 26, 2025 katika shule za Chumbageni, Galanosi, Kiomoni, Mikanjuni, Mkwakwani, Usagara, Nguvumali, Pongwe, Mabokweni na Msambweni.

Kupitia mafunzo ya vitendo, mijadala ya papo kwa papo na maonesho ya vifaa vya mionzi, wanafunzi walipata uelewa wa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia katika sekta za afya, kilimo, viwanda na mazingira.

TAEC wamesema elimu hiyo inalenga kuondoa hofu kwa jamii, kuandaa wataalamu wa baadaye na kuchangia mapambano dhidi ya saratani kupitia tiba ya mionzi (radiotherapy).

“Tunataka vijana wetu waelewe kuwa mionzi siyo silaha pekee, bali pia ni tiba, chakula bora na usalama wa mazingira. Wanafunzi hawa ndio wataalamu wa kesho,” walisema wataalamu hao.

TAEC pia imesisitiza kuwa elimu hii ni mchango katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan afya bora, elimu bora, nishati na viwanda pamoja na ulinzi wa mazingira.

Kwa kuwahamasisha wanafunzi kuchukua masomo ya sayansi, TAEC inalenga kuongeza idadi ya wataalamu katika fani za fizikia tiba, uhandisi wa nyuklia na usalama wa mionzi.

Kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa tume hiyo kuhakikisha taifa linakuwa na kizazi chenye maarifa ya sayansi ya nyuklia kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.









Share this

Related Posts

Previous
Next Post »