RAS TANGA- MIKAKATI ENDELEVU SULUHISHO KUKABILI DHARURA ZA KIAFYA

March 05, 2026








Na Andrea Kadege, WAF-Korogwe

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta ameagiza kuwekwa kwa mikakati endelevu itakayoiwezesha jamii kukabiliana na majanga ya dharura yanayopelekea athari kiafya, kwa ufanisi zaidi.

Bw. Mchatta ameyasema hayo leo Machi 05, 2026 wakati akifunga kikao kazi cha tathmini ya matukio na athari za kiafya mkoani Tanga, kilichoandaliwa na Wizara ya Afya Idara ya Dharura na Maafa kwa kushirikiana na Mradi wa Usalama wa Afya Duniani unaotekelezwa na asasi zisizo za kiserikali za PATH na CIHEB Tanzania, kilichofanyika Wilayani Korogwe.

“Maazimio yote yaliyojadiliwa yawekwe katika mpango kazi wenye malengo yanayopimika, muda wa utekelezaji na mgawanyo wa majukumu kwa kila sekta” amesema Bw. Mchatta

Aidha, amesema kwa kuwa idadi kubwa ya washiriki katika kikao kazi hicho ni wajumbe wa kamati ya maafa ya mkoa hivyo, amesisitiza kuwekwa kwa mikakati endelevu na ya muda mrefu kuhakikisha kuwa majanga ya dharura yanakabiliwa ili kulinda afya ya jamii.

Katika hatua nyingine ameishukuru na kuipongeza Wizara ya Afya kwa kuandaa kikao kazi hicho, huku akitambua mchango wa ushirikiano baina ya serikali na wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali (PATH na CIHEB Tanzania) pamoja na sekta binafsi katika kuimarisha utayari wa kukabiliana na dharura.

Naye Mratibu-Udhibiti Maafa na Dharura kutoka Wizara ya Afya Dkt. Saumu Nungu amesema kwa ngazi ya mikoa, Tanga umekuwa mkoa wa nne kufanyiwa tathmini ya matukio na athari za kiafya, huku akieleza kuwa kupitia mpango kazi utakaoandaliwa, Mkoa wa Tanga utakuwa na uwezo wa mapema wa kukabiliana na dharura za kiafya pindi zitakapotokea.

Amebainisha kuwa baada ya mpango huo kuandaliwa, utawasilishwa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa kwa ajili ya mapitio kisha kusainiwa na kuidhinishwa ili utekelezaji wake uwe wa lazima na unaosimamiwa kikamilifu ili uweze kuwa wenye tija.

Kwa upande wake Mratibu wa Vituo vya Operesheni za Dharura za Afya ya Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Idara ya Afya Dkt. Ernest Kyungu ameeleza kuwa mafanikio katika kukabiliana na majanga ya kiafya yanetokana na maandalizi ya mapema, uratibu wa sekta mtambuka na uwekezaji katika elimu ya kinga kwa jamii.

Amesitiza kuwa Tanga inapaswa kujenga mfumo madhubuti unaojumuisha hatua za kabla ya janga, wakati wa janga na baada ya janga ili kupunguza madhara kwa wananchi kwa kuzingatia jiografia yake hususani mipaka ya bahari na bandari pamoja na mpaka wa nchi jirani ya Kenya.

Naye kiongozi wa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mlipuko na yaliyopewa kipaumbele kutoka Mradi wa Usalama wa Afya Duniani unaotekelezwa na asasi zisizo za kiserikali za PATH na CIHEB Tanzania Dkt. Said Sheuya, ameeleza kuwa kupitia ushirikiano uliopo baina ya Wizara ya Afya na wadau mbalimbali , wamefanikiwa kuendesha mafunzo kwa wataalam, kuimarisha mifumo ya taarifa na kuongeza upatikanaji wa rasilimali muhimu za kukabiliana na majanga.

Kwa ujumla, kikao hicho kimeweka msingi wa maboresho ya kimkakati katika sekta ya afya mkoani Tanga, huku utekelezaji wa mpango kazi utakaoidhinishwa ukitarajiwa kuwa dira ya kuhakikisha ulinzi wa afya ya jamii unaimarika na athari za majanga zinapunguzwa kwa kiwango kikubwa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »