
Na WAF – Dar es Salaam.
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa ametaka ndani ya siku 21 Wizara ya Afya kupitia Idara ya Huduma za Dawa na ofisi ya Mfamasia Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA) kuandaa wito wa uoneshaji wa nia (Call of Expression of Interest) ili kuvutia wawekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba.
Akizungumza mbele ya Wataalam wa Sekta ya Afya Novemba 24, 2025 katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam, Waziri Mchengerwa amesema hatua hiyo inalenga kuvutia wawekezaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini ili kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
“Tuandae ‘Call of Expression of Interest’na tuwaonyeshe yale ambayo tunaweza kushirikiana nao katika utengenezaji wa dawa lakini pia tuwakaribishe katika uwekezaji wa viwanda vingi vya dawa na vifaa tiba hapa nchini” amesisitiza Waziri Mchengerwa huku akitoa siku 21 kwa wito huo kuwa umeandaliwa na kutolewa.
Amesema kuwa uwekezaji wa viwanda vya dawa hapa nchini utairahisishia Serikali katika kusimamia ubora wa bidhaa zinazozalishwa kwa usalama wa afya za Watanzania huku pia kuipunguzia Serikali gharama kubwa ya kununua bidhaa za afya kutoka nje ya nchi.


EmoticonEmoticon