WAZIRI WA FEDHA ZANZIBAR AIPONGEZA TRA KWA KUIMARISHA NA KUWEZESHA BIASHARA KATI YA TANZANIA BARA NA ZANZIBAR

November 06, 2026

    

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Juma Malik Akil ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuendelea kuimarisha na kuwezesha biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza ofisini kwake Kisiwani Unguja alipotembelewa na Menejimenti ya TRA ikiongozwa na Kamishna Mkuu Bw. Yusuph Juma Mwenda kwa lengo la kumtambulisha Kaimu Naibu Kamishna wa Zanzibar Bw. Rashid Suleiman Herikh, amesema TRA imekuwa kiungo muhimu katika kuwezesha biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Dk. Akil amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inathamini kazi inayofanywa na TRA kwa kushirikiana na ZRA huku akigusia kupaa kwa uchumi kuchangiwa na Mamlaka hizo na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kufanywa kwa fedha za ndani kwa kiasi kikubwa.

"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi wanatufundisha kujitegemea ndiyo maana Bajeti zetu zimepunguza utegemezi", anaeleza Dkt. Akil.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Fedha kwa ushirikiano wanaoutoa kwa TRA katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yake huku akiomba ushirikiano zaidi kwa Kiongozi mpya wa TRA Zanzibar.

Kamishna Mwenda amesema kwa upande wa biashara ya mafuta awali vilitolewa vibali vya kuingiza Tani 45,000 lakini ziliingizwa tani 25,000 na kuwa tani zilizosalia 20,000 zitaingizwa kati ya sasa na Desemba 31, 2026 na hii itahusisha wafanyabiashara wenye vibali pekee.

Amesema TRA inaangalia uwezekano wa kuongeza muda wa utoaji vibali vya mafuta hayo ili kuiwezesha biashara hiyo kuwa endelevu maana mahitaji ya mafuta yanafahamika.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »