TGNP YATAKA HALMASHAURI KUWEKA BAJETI ZA KIJINSIA KUREJESHA WANAFUNZI SHULENI

November 18, 2026

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umewataka maafisa mipango, elimu na ustawi wa jamii kutoka halmashauri mbalimbali nchini kuhakikisha wanaingiza masuala ya jinsia katika mipango na bajeti zao ili kuweka mazingira rafiki ya kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali.

Wito huo umetolewa leo Novemba 18, 2026 na Mwezeshaji na Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia, Rebeca Kisena, wakati wa mafunzo ya siku tatu yaliyofanyika katika ofisi za TGNP, yakihusisha maafisa kutoka halmashauri mbalimbali nchini kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia masuala ya jinsia katika upangaji wa mipango na bajeti.

Amesema mafunzo hayo yamelenga pia kutathmini utekelezaji wa sera ya mwaka 2021 inayotoa fursa kwa wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito, ndoa, utoro, changamoto za kifamilia na magonjwa kurejea shuleni na kuendelea na masomo.

Kisena amesema pamoja na uwepo wa sera hiyo, bado kuna umuhimu wa kufuatilia kiwango cha uelewa na utekelezaji wake katika halmashauri, kubaini changamoto zinazojitokeza na kuhakikisha wanafunzi wanaostahili wanapata fursa hiyo.

Amesisitiza kuwa usawa wa kijinsia ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, akieleza kuwa kuwanyima watoto wa kike au wa kiume fursa ya kupata elimu kutokana na mazingira mbalimbali ni kuwawekea vikwazo vinavyoweza kuathiri maendeleo yao ya baadaye.

Amesema ushirikishwaji wa maafisa mipango, elimu na ustawi wa jamii katika mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa wanahusika moja kwa moja katika maandalizi ya bajeti, usimamizi wa shule na ustawi wa wanafunzi, hivyo wanapokuwa na uelewa wa pamoja wanaweza kubaini changamoto na kupanga namna bora ya kuzitatua.

Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Elimu Maalumu katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Kanasia Nyella, amesema mafunzo hayo yatamsaidia kuboresha utekelezaji wa masuala ya jinsia katika shule za sekondari.

Amesema baada ya mafunzo hayo atashirikiana na watumishi wenzake, waratibu elimu kata, wakuu wa shule na walimu walezi ili kuwafikishia maarifa waliyoyapata na kuhakikisha yanatumika katika kuboresha mazingira ya elimu.

Naye Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Haygaru Shauri Karengi, amesema mafunzo hayo yamempa uelewa kuhusu umuhimu wa kutumia takwimu za wanafunzi waliokatisha masomo katika kuandaa mipango na bajeti za halmashauri.

Amesema hatua ya kwanza watakayochukua ni kukusanya takwimu za wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na ujauzito, utoro na changamoto za kifamilia ili kubaini mahitaji yao na kutenga fedha zitakazowawezesha kurejea shuleni.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Daudi Wengi, amesema mafunzo hayo yameongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuandaa bajeti zinazozingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya kijamii, wakiwemo watu wenye ulemavu, wazee na wanawake.

Amesema changamoto mojawapo katika upangaji wa mipango ni upungufu wa takwimu sahihi, hali inayoweza kusababisha baadhi ya mahitaji ya makundi maalumu kutokuzingatiwa katika bajeti.

Ameeleza kuwa matumizi ya takwimu sahihi yatasaidia halmashauri kupanga huduma kulingana na mahitaji halisi ya wananchi, ikiwemo ujenzi wa vyoo katika taasisi za elimu kwa kuzingatia uwiano wa wanafunzi wa kike na wa kiume pamoja na kuweka mazingira yanayozingatia mahitaji maalumu ya wanafunzi wa kike.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »