TANZANIA YAHIMIZA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KUONGEZA UWEKEZAJI WA NISHATI JADIDIFU NA KUIMARISHA USALAMA WA NISHATI

November 14, 2026


ANTALYA, UTURUKI 


Tanzania imetangaza vipaumbele vyake katika kuongeza uwekezaji wa nishati jadidifu kwa kushirikiana na nchi nyingine, taasisi za kimataifa na sekta binafsi, hususan katika upatikanaji wa teknolojia, fedha na utaalamu kwa ajili ya kuendeleza matumizi ya nishati safi na endelevu.

Hayo yameelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishato anayeshughulikia Umeme na Nishati Jafidifu Eng. Dkt. Felchesmi Mramba leo Novemba 14, 2026, jijini Antalya nchini Uturuki, katika Mjadala wa Sera kuhusu kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika nchi zilizoendelea kwa kiwango cha chini (LDCs), kupitia Ushirikiano wa Kusini kwa Kusini ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa.

Katika mjadala huo, Dkt. Mramba ameeleza kuwa Mkakati wa Taifa wa Nishati Jadidifu wa mwaka 2024-2034, umeweka kipaumbele katika kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo vya nishati ya jua megawati 804, upepo megawati 750 na jotoardhi megawati 215. Hatua hiyo inalenga kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme na kuimarisha usalama wa nishati nchini.

Aidha, ameongeza kuwa pamoja na uwekezaji katika uzalishaji wa umeme, kuna umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme, kutumia mifumo ya kisasa ya gridi za umeme (Smart Grids) na kujenga miundombinu inayoweza kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Hadi Septemba 2026, uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini ulifikia takribani megawati 4,600, huku Serikali ikiwa na lengo la kufikia megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo ameeleza changamoto za gharama kubwa za teknolojia, upatikanaji mdogo wa fedha za masharti nafuu na uhaba wa wataalamu ni miongoni mwa mambo yanayohitaji kushughulikiwa ili kuongeza kasi ya uwekezaji katika nishati jadidifu. 

Kutokana na hali hiyo, Tanzania imehimiza washirika wa maendeleo na taasisi za fedha za kimataifa kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya maandalizi na utekelezaji wa miradi, pamoja na kuimarisha uhamishaji wa teknolojia na utaalamu.

Tanzania pia imezitaka taasisi za Umoja wa Mataifa, ikiwemo Benki ya Teknolojia ya Umoja wa Mataifa (UN Technology Bank) na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Ushirikiano wa Kusini kwa Kusini (UNOSSC) kusaidia nchi za kusini kubadilishana uzoefu, kujenga uwezo wa wataalamu na kuimarisha ushirikiano katika tafiti na ubunifu. Sekta binafsi nayo imehimizwa kuongeza uwekezaji katika teknolojia za nishati jadidifu na uzalishaji wa vifaa nchini.

Tanzania imesisitiza utayari wake wa kushirikiana na nchi nyingine katika kubadilishana uzoefu wa maendeleo ya nishati jadidifu, hususan nishati ya maji, jua, upepo na jotoardhi, ili kuongeza uzalishaji wa umeme na kuendeleza sekta ya nishati inayozingatia matumizi endelevu ya rasilimali na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »