
Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Aubrey Silayo,akizungumza na waaandishi wa habari leo Novemba 17,2026 jijini Dodoma kuhusu matumizi ya mfumo wa Stempu za kodi za Kielektroniki kwenye vinywaji na bidhaa nyingine.
Na.Mwandishi Wetu – DODOMA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma imeanza rasmi kampeni ya ukaguzi wa bidhaa na kutoa elimu kwa umma kuhusu stempu za kodi za kielektroniki katika wilaya zote za Mkoa wa Dodoma.
Kampeni hiyo inalenga kuhakikisha bidhaa zinazouzwa sokoni zinatumia stempu halali za kielektroniki, kudhibiti matumizi ya stempu bandia na bidhaa zisizolipiwa ushuru, pamoja na kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu umuhimu wa kuhakiki stempu kabla ya kununua au kutumia bidhaa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 17, 2026 jijini Dodoma, Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Aubrey Silayo, amesema zoezi hilo litahusisha ukaguzi wa uhalali wa stempu zinazobandikwa kwenye bidhaa mbalimbali, zikiwemo vinywaji, bia, pombe kali, sigara na mvinyo, pamoja na kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu umuhimu wa kuhakiki stempu kabla ya kununua au kutumia bidhaa.
Silayo amesema matumizi ya stempu za kodi za kielektroniki ni sehemu ya jitihada za Serikali kuimarisha usimamizi wa kodi, kudhibiti bidhaa zisizo halali na kuhakikisha wafanyabiashara wote wanatekeleza wajibu wao wa kulipa ushuru kwa mujibu wa sheria.
“Mfumo wa stempu za kodi ulianza kutumika nchini mwaka 1998, kabla ya Serikali kupitia TRA kuanzisha mfumo wa kisasa wa stempu za kielektroniki mwaka 2018, ambao umechukua nafasi ya stempu za karatasi zilizokuwa katika mazingira rahisi ya kughushiwa,” amesema Bw. Silayo.
Ameeleza kuwa mfumo huo wa kidijitali unawezesha kila bidhaa kuwa na namba maalumu ya utambulisho pamoja na alama za kiusalama, zinazosaidia kutambua uhalali wa bidhaa na kutoa nafasi kwa watumiaji kufanya uhakiki kabla ya kuzitumia.
Silayo amesema hatua hiyo siyo tu inalenga kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, bali pia inalinda afya za wananchi dhidi ya bidhaa bandia au ambazo hazijathibitishwa ubora na usalama wake na mamlaka husika.
“Wananchi wanaweza kutumia simu janja kupakua programu ya HAKIKI STEMPU, ambayo inawawezesha kuhakiki bidhaa wanazokusudia kununua au kutumia kwa kuchunguza uhalali wa stempu iliyobandikwa kwenye bidhaa husika,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa endapo mtumiaji atabaini bidhaa yenye stempu isiyothibitishwa au inayotia shaka, anaweza kutoa taarifa kupitia mfumo huo kwa kueleza eneo alilonunua bidhaa, aina ya bidhaa na kuambatanisha picha pamoja na taarifa nyingine zitakazosaidia TRA kufanya ufuatiliaji.
Katika hatua nyingine, Silayo amewatahadharisha wafanyabiashara, watengenezaji na waagizaji wa bidhaa kuhakikisha wanatumia stempu sahihi za kielektroniki kabla ya kuingiza bidhaa sokoni, akisisitiza kuwa matumizi ya stempu bandia ni kosa linaloweza kuchukuliwa hatua za kisheria.
Amesema TRA imeimarisha uwezo wa kubaini stempu za kughushi kwa kutumia mifumo ya kiintelijensia pamoja na skana maalumu, hivyo wahusika wanaojihusisha na udanganyifu huo watabainika na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa Silayo, adhabu kwa watakaobainika kutumia vibaya stempu za kielektroniki ni faini isiyopungua Sh milioni tano na isiyozidi Sh milioni 50, au kifungo kisichozidi miaka mitatu, au adhabu zote mbili kwa pamoja.
Amesisitiza kuwa jukumu la kuhakikisha bidhaa zinazotumika ni halali halipaswi kuachwa kwa TRA pekee, bali linahitaji ushirikiano wa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla, huku akiwataka kutoa ushirikiano kwa maafisa watakaotekeleza zoezi la ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Amesema matumizi sahihi ya stempu za kielektroniki yataimarisha ushindani wa haki katika biashara, kudhibiti ukwepaji wa kodi, kuongeza mapato ya Serikali na kulinda afya za wananchi.
Hata hivyo, amewahimiza wananchi kujenga utamaduni wa kuhakiki stempu za kodi kabla ya kutumia bidhaa, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya uwajibikaji wa kila mmoja katika kulinda uchumi wa nchi na usalama wa jamii.
HAKIKI STEMPU, TUMIA BIDHAA HALALI, LINDA AFYA YAKO!

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Aubrey Silayo,akizungumza na waaandishi wa habari leo Novemba 17,2026 jijini Dodoma kuhusu matumizi ya mfumo wa Stempu za kodi za Kielektroniki kwenye vinywaji na bidhaa nyingine.
EmoticonEmoticon