Na Shaban Juma, WAF – Dodoma
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali imelenga kuongeza idadi ya wananchi wanaonufaika na Bima ya Afya kwa Wote hadi kufikia milioni 25 ifikapo Juni 2027, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma za afya bila kukabiliwa na mzigo mkubwa wa gharama za matibabu.
Mhe. Mchengerwa amebainisha hayo leo Novemba 05, 2026, wakati akizungumza katika semina ya Wabunge kuhusu utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, iliyofanyika Bungeni jijini Dodoma.

Amesema awamu hiyo iliyoanza kutekelezwa Oktoba 22, 2026, inalenga kuwafikia wananchi wenye uwezo wa kujilipia bima zao pamoja na kuendelea kuwagharamia wananchi wasio na uwezo kupitia Serikali.
"Serikali imeweka kifurushi cha bima ya afya cha FAHARI AFYA kwa gharama ya Shilingi 150,000 kwa kaya yenye watu wasiozidi sita, kinachowezesha wanufaika kupata huduma za afya kuanzia zahanati hadi Hospitali ya Taifa kwa kuzingatia utaratibu wa rufaa" - amesema Mhe. Mchengerwa
Amesisitiza kuwa mpango huo hauimaanishi kila Mtanzania atapata bima bure, bali wananchi wenye uwezo watachangia gharama za bima zao na familia zao, huku Serikali ikiendelea kugharamia bima kwa wananchi wasio na uwezo.
Aidha, amesema utekelezaji wa mpango huo unahitaji ushirikiano wa viongozi katika ngazi zote za Serikali, hususan Wabunge, katika kutoa elimu sahihi kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya na manufaa yake.
Mhe. Mchengerwa amebainisha kuwa mafanikio ya mpango huo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na kulinda ustawi wa familia zao.



EmoticonEmoticon