Serikali imeendelea kupanua wigo wa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini kupitia programu mbalimbali za ruzuku, ambapo hadi sasa majiko banifu 145,659 na mitungi ya gesi ya LPG 484,410 imesambazwa, huku kaya 2,515 na taasisi 31 zikiunganishwa na mtandao wa gesi asilia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Dkt. Mha. Felchesmi Mramba, ameeleza hayo Novemba 28, 2026, jijini Dodoma, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034 katika Kikao Kazi cha Wakuu wa Mikoa kuhusu Nishati Safi ya Kupikia.
Amesema programu hizo zinalenga kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, hususan kwa wananchi wenye kipato cha chini, akibainisha kuwa hadi sasa taasisi 2,703 kati ya 31,395 zinazolengwa, zimehamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kuandaa chakula cha watu zaidi ya 100.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza programu ya uwezeshaji wa wananchi kupata vifaa vya kupikia kwa utaratibu wa malipo kupitia bili za umeme (On-Bill Financing), ambayo hadi sasa imefikia kaya 1,032, huku lengo likiwa kuwafikia wanufaika milioni moja ndani ya miaka mitatu.
Mha. Mramba amesema Serikali pia inaendelea kuimarisha miundombinu ya uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa nishati safi ya kupikia, kuandaa viwango vya ubora wa vifaa vya kupikia vinavyotumia umeme, kuratibu misamaha ya kodi na tozo, pamoja na kukamilisha Moduli ya Taifa ya Nishati Safi ya Kupikia.
Sambamba na hayo, Serikali inaendelea kuhamasisha uzalishaji wa mkaa mbadala kupitia utoaji wa mashine kwa utaratibu wa ruzuku, pamoja na kutoa elimu kuhusu matumizi salama na sahihi ya teknolojia mbalimbali za kupikia. Tayari madiwani katika mikoa ya Simiyu, Katavi na Singida wamepatiwa elimu kuhusu nishati safi ya kupikia.
Mha. Mramba amewataka Wakuu wa Mikoa kuimarisha uratibu wa programu hizo, kujumuisha ajenda ya nishati safi ya kupikia katika vipaumbele vya mikoa, kuhamasisha wananchi na taasisi kutumia nishati hiyo, pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika uzalishaji na usambazaji wake.
Amesisitiza kuwa ushiriki wa Wakuu wa Mikoa ni muhimu katika kuharakisha utekelezaji wa mkakati huo ili kufikia lengo la Taifa la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.





EmoticonEmoticon