Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha kila kijiji na kitongoji kinaanzisha kitalu cha miti ili kuimarisha uhifadhi wa misitu ikiwa ni hatua ya kuunga mkono ajenda ya nishati safi ya kupikia inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kulinda afya za wananchi na mazingira.
Mhe. Kwagilwa ametoa agizo hilo leo, Novemba 28, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), katika Kikao Kazi cha Wakuu wa Mikoa kuhusu Nishati Safi ya Kupikia.
Amesema Rais Samia anaongoza ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia katika ukanda wa Afrika Mashariki na kimataifa, akisisitiza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuambatana na hatua madhubuti za kupunguza ukataji wa miti na kuimarisha uhifadhi wa misitu.
Akifafanua ukubwa wa changamoto ya uharibifu wa misitu, Mhe. Kwagilwa amesema takribani hekta 373,000 za misitu hupotea nchini kila mwaka kutokana na shughuli mbalimbali za ukataji wa miti, hali inayohitaji ushirikiano wa Serikali, taasisi na wananchi katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Amesema kuanzishwa kwa vitalu vya miti katika ngazi za mitaa, vijiji na vitongoji kutarahisisha upatikanaji wa miche na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za upandaji miti, huku akizitaka mamlaka husika kutenga maeneo maalumu na kuweka mikakati ya kuanzisha na kuendeleza vitalu hivyo.
Aidha, amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni sehemu ya jitihada za Serikali za kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa unaochangia ukataji wa miti na uharibifu wa mazingira, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza shughuli za upandaji na utunzaji wa miti ili kurejesha misitu inayopotea.
Mhe. Kwagilwa amewataka viongozi katika ngazi zote kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia, kutoa elimu kuhusu athari za uharibifu wa misitu na kushiriki kikamilifu katika kampeni za upandaji miti ili kulinda rasilimali za misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.



EmoticonEmoticon